Ndugu Rais, sasa ‘ruksa’ mtumishi akapumzike

Ndugu Rais, naandika kutoa ushuhuda ili wote wanaopitia katika majaribu magumu watambue kuwa wanaomtegemea Mungu hawatafadhaika kamwe.

Alhamisi iliyopita Aprili 25, 2019 nilikuwa Ifakara High School kushiriki katika mahafali ya wahitimu wa kidato cha sita, binti yangu alikuwa miongoni mwao. Shule ile imejengwa vizuri. Zilikuwapo tetesi kuwa ilijengwa na Wacuba miaka ya 1960. Imejengwa katika mandhari na mazingira yaliyo bora kabisa kuwawezesha wanafunzi kusoma kwa nafasi. Wanasema iko porini na kweli iko porini lakini kule ndiko iliko elimu ya kweli. Nikazikumbuka siku zangu za shule.

Seminari zote zilijengwa porini kabla miji haijazifuata baadhi. Ifakara High School imefanyiwa ukarabati mkubwa. Kwa kuwa imejengwa kwa ustadi mkubwa, sasa inavutia sana. Katika risala tulisikia jina lako baba likitajwa. Alisema: “Shule hii imekarabatiwa kwa fedha nyingi sana ambazo kwa upendo tu zilitolewa na Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, John Magufuli.”

Wakati wazazi tunaanza kukupigia makofi tulikatizwa alipoendelea kusema:  “Shule hii huenda ikabadilishwa jina na kuitwa Ifakara Shule ya Kunguni. Alisema kuna kunguni kila mahali; katika mabweni, madarasani, maktaba, sehemu za

chakula mpaka vyooni. Ilionekana dhahiri kuwa kilio chao hicho ni cha muda mrefu wahusika wameziba masikio yao. Baba katika mambo makubwa unayoifanyia nchi yetu hili la Ifakara High School ni la kupigia mfano.

Lakini kuna baadhi ya watendaji wako wa wilaya na mikoa ambao yaonekana mambo makubwa unayoifanyia nchi hii au hawataki yafurahiwe na wananchi wako au wamejisahau. Wameitia najisi kazi kubwa uliyoifanyia shule hii. Suala la kunguni halikuwa lazima mpaka likufikie wakati wapo. Wangekuwa wamelitatua. Wanasema vitanda vingi ni vibovu. Vitabu havikidhi mahitaji. Hizi ni kero ambazo ni lazima zimfikie mkuu wa nchi? Wangekuwa makini baada ya kusoma haya niliyokuandikia wangeenda mbio kuinusuru shule yako kabla hujawatuma watu wako. Hawa wanangoja uwasukume. Baba, wakemee.

Binti yangu amemaliza lakini siwezi kunyamaza kwa sababu wanaobaki na watakaokuja pia ni wanangu kwa kuwa nao ni watoto wa taifa hili! Kwa aliye timamu atagundua kuwa walimu wale wanafundisha kwa moyo wa kujituma. Tofauti kubwa ukilinganisha na walimu wengi wa shule za serikali. Wanahitaji kutiwa moyo zaidi kwa kuwapatia motisha. Mwalimu Nyaori Chacha na walimu wenzako Mwenyezi Mungu awatangulie. Nimeliona hili kwa matokeo ya binti yangu. Ametunukiwa tuzo nne. Ameshinda kwa kiwango cha Excellent katika somo la Kemia, Excellent katika somo

la Fizikia, Excellent katika soma la Advanced Mathematics na kuibuka mshindi wa kwanza wa jumla wa tahasusi (combination) ya PCM. Nilimsikia mtangaza matokeo akisema: “This is the best student.”

Baba, maandiko katika Biblia Takatifu yanasema: “Mpumbavu hujisemea moyoni mwake kuwa hakuna Mungu.’’ Kwa hili Mungu wangu amejidhihirisha uwepo wake kwangu. Mwanangu ameniinua pa kubwa. Kila alipotangazwa mpaka mara nne nilimfuata jukwaa kuu kumpongeza. Mwishoni kila niliponyanyuka kwenda kumpongeza wazazi wenzangu walinishangilia mimi.

Kwa haya makubwa aliyonitendea Muumba wangu, sasa nasema, Bwana anaweza kuniruhusu mtumishi wake niende nikapumzike kwa amani. Bwana sasa anaweza kuniruhusu niutoke ulimwengu huu wa mateso nikaungane na wazazi wangu katika furaha ya milele ile Bwana aliyowaandalia waja wake wote wanaomsujudia! Aleluya! Mwenyezi Mungu ni mwema!

Wanawema kama kuna mtu amenifanya niishi maisha ya shinikizo la damu katika hiki kipindi cha miaka kumi na mitano inayoishia sasa ni huyu binti yangu. Kila nilipofikiria ni elimu ya aina gani nitampatia mwanangu kwa kipato changu cha pensheni ya Sh 50,000 nyongo hunikata ini. Ukimtegemea Mungu hatakuacha kamwe. Amenijalia, binti yangu amesoma chekechea kwa miaka mitatu, shule ya msingi miaka sita na sekondari miaka minne katika shule za watakatifu ambazo malipo yake ni mamilioni ya shilingi kila mwaka. Nilikuwa nalipaje, sina maelezo.

Naikumbuka safari yangu katika nchi ya ahadi, Israel. Tulifika katika kilima ambapo Bwana Yesu aliulisha umati mkubwa wa watu kwa vipande vitano vya mkate na samaki wawili. Kila wanafunzi wake walipochukua na kuwagawia watu, walipoangalia katika kikapu waliona bado vipo vilevile. Ndivyo ilivyokuwa kwa malipo ya ada ya mwanangu. Kila nilipodhani sasa mwanangu elimu yake basi kwa kukosa ada walitokea wasamaria hata nisijue walitokea wapi, mwanangu aliendelea  na masomo mwaka uliofuatia.

Baba imeandikwa kuwa Mwenyezi Mungu akikupa chakula kigumu, hukupa pia na meno magumu. Hata alipofika darasa la sita nikampeleka akafanyiwe majaribio ya kuingia kidato cha kwanza  bila kupita darasa la saba.

Walimu walimfurahia kwa kufanya vizuri sana kwa muda mfupi sana, wakampokea kwa kidato cha kwanza. Tukiwa katika mkweche wangu tunarudi nyumbani alinisikitikia kwanini sikumpeleka alipokuwa darasa la tano kwani angeyaweza yote yale. Sikuwa na jibu la kumpa lakini nakiri udhaifu wangu kuwa nilichelewa kujua uwezo mkubwa alionao binti yangu.

Katika yote haya namshukuru Muumba wangu. Alipokuwa kidato cha nne alinichekesha aliposema anataka anisaidie

kulipa ada. Nilipomuuliza haya yatawezekana vipi, aliniambia kuwa baba nitajitahidi kusoma kwa bidii sana ili nifaulu vizuri kiasi kwamba wanaochagua walazimike kunipeleka katika shule ya serikali kwa masomo ya kidato cha tano na sita. Na kweli alifaulu vizuri sana na ikawa hivyo, mzigo wa ada akawa amenipunguzia. Safari hii ameniahidi kuwa shida zangu zitapungua. Amesema: “Nitafanya kama alivyokuwa anafanya marehemu Akwilina Akwilini. Mkopo wa elimu ya juu, tutakuwa tunakula hizohizo.’’ Hata sijui kama atapata mkopo wenyewe, lakini mawazo yake yanatia faraja sana!

Viongozi wetu waelewe kuwa vijana wetu wa leo si wajinga sana. Wana uwezo wa ‘kuanalaizi’ mambo na kuyachambua. Tupime maneno yetu kwa kuwa mtoto umleavyo ndivyo akuavyo. Wakati wa viongozi waliotangulia bungeni paliitwa mahali patakatifu. Maneno ya walevi wa pombe za kienyeji ya kule vilabuni yalikuwa hayapati nafasi. Kudai kuwa

Godbless Lema anadai au anadaiwa ni kuonyesha udhaifu wetu kifikra, tusiwapatie watoto. Wanajua kuwa ni hatari kupokea zawadi ya nguo kutoka kwa mtu aliye uchi!