Mbunge mteule Dkt John Pallangyo

Wakati Chama Cha Mapinduzi (CCM) wanashangilia ushindi wa Jimbo la Arumeru Mashariki wa mgombea wao kupita bila kupingwa ni muhimu kwa watu makini wa taifa hili kufanya tafakuri ya nguvu juu ya matukio haya ndani ya taifa letu. Na swali la msingi ni je, tunaimarisha demokrasia katika taifa letu au tunaizika demokrasia? Au labda mifumo hii tumebambikizwa tu, si utamaduni wetu?

Kwa mara ya kwanza katika historia ya taifa letu, tumeshuhudia chaguzi ndogo nyingi na wanasiasa wameweka rekodi mpya ya kuhama vyama. Fedha nyingi zinazotumika kurudia chaguzi hizi ni hasara ambayo tutaijua mbele ya safari. Tunata tusitake ni lazima ituguse na kutuumiza tu! Kwa wachambuzi na watu wanaoguswa na uhai wa taifa letu ni lazima watakuwa wanajiuliza maswali mengi sana. Kwa mfano, ni mvuto wa mtu, ni mvuto wa chama, ni umaskini, ni rushwa, au ni elimu ndogo juu ya demokrasia na ushiriki wa watu katika uongozi wa taifa lao. Pia mtu mzushi anaweza kuuliza kama kweli raia ni makini? Katika hali ya kawaida, raia makini ni lazima atambue dhana nzima ya demokrasia na ushiriki wa watu. Raia makini, akishafahamu hilo, hawezi kukubali kurudia uchaguzi wa mtu yule yule ambaye anahama chama chake na kuomba kugombea tena kwenye chama kingine kwa uwakilishi ule ule, Bunge na halmashauri ile ile labda kiti tofauti kwa kurudi upande wa chama tawala kama alikuwa mpinzani na kinyume chake.

Au wakati kuna ushahidi wa kutosha kwamba kuna wabunge ambao hawajaonekana bungeni zaidi ya miaka mitatu na bado hawajasimamishwa, inakuwa vipi mbunge ambaye alitoa taarifa za kumuuguza mke wake afukuzwe na kuvuliwa ubunge wake? Wananchi makini ni lazima wahoji na kukataa kurudia au kumpitisha mtu bila kupingwa.

Katika maana yake pana, demokrasia ni njia ya kutawala kwa msingi wa kupata ‘ridhaa ya watu’. Katika demokrasia, mawazo ya watu yanazingatiwa katika kufanya uamuzi. Raia wote wana haki ya kushiriki katika kuamua jinsi nchi inavyoongozwa. Raia wanashiriki katika  uongozi wa dola kwa kupitia viongozi wanaowachagua. Katika demokrasia, viongozi wanawajibika kwa raia. Raia wanathibitisha imani kwa viongozi wao mara kwa mara kwa kupitia uchaguzi. Pia watu hushiriki ama moja kwa moja au vinginevyo katika kufanya uamuzi unaoathiri maisha yao.

Demokrasia ni mfumo wa utawala ambapo watu huwachagua viongozi wa serikali yao wenyewe na kuainisha jinsi inavyopaswa kufanya kazi. Demokrasia hukuza ustawi wa watu wote. Kila raia ana haki ya kushiriki katika uendeshaji wa shughuli za umma na katika mambo yote yanayoathiri maisha yake. Katika kujishughulisha na masuala ya uraia, raia wanaiwajibisha serikali. Viongozi wanawasikiliza wapiga kura wao kabla ya kufanya maamuzi kwa niaba ya watu.

Uraia mwema unatanguliza ushiriki katika uwakilishi na ushirikishwaji katika uamuzi. Raia huwachagua wawakilishi wao kwa kufuata kanuni ya demokrasia ya moja kwa moja, ambapo wawakilishi waliochaguliwa hufanya uamuzi unaowafunga kwa niaba ya raia. Raia wanatazamiwa kuwa waelewa wa majukumu yao na hivyo waweze kutoa madai yao kwenye mfumo. Hata hivyo, upataji wa habari ni muhimu kwa ufanisi wa uraia.

Hata hivyo kuna vikwazo vinavyojitokeza katika chaguzi za kidemorasia. Vikwazo vikubwa kwa uchaguzi wa kidemokrasia vinajumuisha umaskini, ukosefu wa usawa, ujinga, rushwa katika uchaguzi, chaguzi mbovu, siasa isiyo na maadili, kukata tamaa kisiasa, ukosefu wa ujasiri, utamaduni wa kisiasa uliolazimishwa, ubaguzi, kushauriwa, na uongozi wa mabavu.

Kwa maneno mengine demokrasia ni njia ya kutawala ambayo mawazo ya watu wote hufikiriwa katika kufanya uamuzi unaohusu umma. Ina msingi wake katika imani ya ‘utashi wa watu’. Hivyo, demokrasia husimamia ustawi wa watu wote, kwa manufaa ya watu wote.

Demokrasia pia inahusu kujitolea kwa raia wote. Raia wana wajibu mkubwa katika jamii inayojenga demokrasia.  Kwa maana hiyo ndiyo kusema demokrasia inaweza kufanya kazi pale tu ambapo wananchi wanashiriki kikamilifu katika shughuli za kisiasa na masuala ya umma. Kwa kuzingatia hilo, demokrasia ni kile wanachokifanya wananchi – na si kile wanachofanyiwa.
Hivyo  basi demokrasia hukuza uhuru, usawa na haki kwa wote. Pia inasimamia ukuzaji wa ushiriki wa moja kwa moja na wa uwakilishi kwa watu wote, wanawake kwa wanaume, vijana na kadhalika katika shughuli za umma. Katika jamii ya leo, demokrasia ya moja kwa moja inadhihirika kwa njia ya kushiriki katika chaguzi. Pia inajidhihirisha katika ushiriki wa raia katika utawala kwenye ngazi ya kijiji. Demokrasia ya uwakilishi inatekelezwa katika ngazi ya serikali za mitaa na tarafa.

Katika demokrasia, wananchi ndio wenye mamlaka. Serikali ni mtumishi wa wananchi. Uhusiano kati ya wananchi na serikali ni wa mkataba, yaani, kuna mkataba kati ya wananchi na viongozi wao. Katika jambo hili, viongozi na wawakilishi wengine wanafanya uamuzi kwa niaba ya mwananchi ambaye ni raia.

Serikali inalazimika kufuata masharti ya mkataba kati ya wananchi na viongozi na wawakilishi wengine. Mkataba huu lazima ufanyiwe mapitio kipindi hadi kipindi, kwa kutumia  chaguzi. Kwa upande wao, raia lazima waheshimu sheria zilizotungwa. Pia washiriki katika shughuli za umma na kukubali au kukataa jinsi serikali inavyofanya kazi yake.

Tunaposema kwamba raia ndio wenye mamlaka, maana yake ni kwamba raia wanapowachagua viongozi wa kuwawakilisha, hawajivui mamlaka hayo. Wawakilishi waliochaguliwa wanawajibika kwa raia, yaani wanawajibika  kwa wapiga kura wao.

Na tunaposema ‘mkataba wa kijamii’ maana yake ni namna ya kuelezea uhusiano uliopo katia ya raia na dola au serikali. Dola au serikali imekuwepo kutokana na haja ya kuanzisha na kudumisha utawala wa sheria. Ili kuweka utaratibu wa aina hiyo, raia wana wajibu wa kutekeleza kwa serikali na pia serikali ina wajibu wa kuwatendea raia. Mkataba wa kijamii unadhihirisha uaminifu na matumaini ambayo raia  wanakuwa nayo kwa wawakilishi wao ili watende kwa niaba yao.

Hivyo basi viongoziu wa kidemokrasia huwasikiliza wapiga kura wao kabla ya kufanya uamuzi kwa niaba yao. Hivyo ndivyo inapaswa kuwa, ingawa wakati mwingine inakuwa kinyume.  Uongozi wa  kidemokrasia uko wazi. Hauna chochote cha kuficha. Unapaswa kutoa taarifa jinsi unavyofanya shughuli zake na kuwa tayari kujibu maswali yatokanayo na ushauri wa rai pamoja na matatizo yao. Serikali lazima ifanye kazi kama mtumishi wa wananchi na lazima ishauriane nao kama wadau wakuu wa sera za maendeleo.

Raia kwa upande wao wanapaswa kuvumilia tofauti zilizopo kati yao. Maana ya uvumilivu wa kisiasa ni mtu kuwatambua wapinzani wake kisiasa, na kutambua kwamba wapinzani hao wana mawazo na maoni tofauti, na kuwa wana haki ya kuyatetea mawazo na maoni yao katika mchakato wa kisiasa. Hii inapunguza uhasama unaojitokeza katika vyama. Maana lengo si kuleta uhasama, lengo ni kujenga taifa letu kwa pamoja. Taifa lenye watu wenye maoni tofauti, lakini lengo moja la kujenga na kuleta maendeleo. Hivyo haina maana yoyote mtu kuhama kutoka chama kimoja kwenda kingine kama mtu huyo tayari yuko kwenye mfumo wa uongozi unaotambuliwa kisheria. Anayemshawishi na yeye anayekubali, wote wanahitaji shule!

Ni lazima kabisa wanachama wa chama tawala na wa upinzani wanatakiwa wajadiliane kwa pamoja juu ya masuala yanayolihusu taifa kulenga kupata muafaka. Raia makini ni yule anayeutafuta muafaka pale panapotokea tofauti! Si kukimbia chama kimoja kwenda kingine, ni kutafuta muafaka.

Uongozi wa kidemokrasia unatambua utawala wa kisheria. Unatambua kwamba watu ndio wanaoshika hatamu. Unajumuisha watu wote kufanya mashauriano na kufuata kanuni za demokrasia. Kinyume cha uongozi wa kidemokrasia ni uongizi wa mabavu ambao huwafanya viongozi washike hatamu. Uongozi wa mabavu haushauriani na wananchi. Daima unawaweka raia pembezoni na hauna uvumilivu kwa mawazo pinzani na hauukubali kukosolewa, ni uongozi ambao kawaida hauna dhamana ya haki za kisiasa na kiraia.

Hivyo, raia makini ni lazima afahamu kwa undani ubora wa demokrasia na ushiriki wa watu. Pia atambue ubaya wa uongozi wa mabavu. Kwa njia hii raia makini anaweza kutumia kura yake vizuri kuwachagua viongozi wake. Maana raia akisha kutambua kwamba ni wajibu wa serikali kutoa na kusimamia huduma za jamii, kama vile elimu, afya na maji. Wakati  huohuo, serikali ina haki ya kukusanya kodi kutoka kwa raia ili kuhimili utoaji wa huduma. Na kwamba kwa upande wao, raia wana wajibu wa kulipa kodi, kupeleka watoto wao shule na kuzilinda mali za umma dhidi ya uharibifu au wizi na kwamba pia, wana haki ya kuiwajibisha serikali kwa matumizi mabaya ya fedha za umma zilizotengwa kuhudumia huduma za jamii, ni lazima kila raia  mwenye umri wa kupiga kura atafanya hivyo.

Je, wananchi wanafahamu kwa kina maana ya uchaguzi na kura yao, maana ya demokrasia na ushiriki wao, maana ya utawala wa kidemokrasia? Je, wanafahamu misingi ya katiba, haki za raia na utawala bora? Haya ni maswali ambayo yanahitaji majibu hasa kwa wakati huu.

Haitoshi mtu kupiga kura. Ni lazima mtu afahamu ni kwa nini anapiga kura. Ni muhimu mtu kufahamu ni kitu gani kinafuata baada ya kupiga kura. Ni jambo la msingi mtu kufahamu uwezo na nguvu ya kura yake.

Uanzishwaji wa demokrasia ya vyama vingi umechochea ushindani mkali wa kisiasa, umeongeza haja ya kuwa na elimu ya upigaji kura. Elimu hii itamsaidia mpiga kura kuwa na maarifa na ufahamu kuhusu masuala ya mchakato wa uchaguzi ili aweze kuwa makini kwenye uchaguzi. Elimu hii inampatia habari kumwezesha raia kuelewa vyema haki na wajibu wake katika mchakato wa uchaguzi, inajenga pia uelewa kwa raia kwamba kudura ya mstakabali wake inategemea kura yake.

Elimu ya uraia inasaidia kutoa mawazo ya uhasama unaojitokeza katika vyama. Kwa sababu ya kutokuwa na elimu juu ya mambo haya watu wamekuwa wakichukiana na wakati mwingine kugombana kwa vile wako kwenye vyama viwili tofauti. Na wanasiasa wamekuwa wakishambuliana badala ya kuelezea sera zao kwa wananchi. Matokeo yake vinakuwa si vyama vya kisiasa tena bali ni makundi ya watu wanaotaka kuingia madarakani.

Kawaida ni kwamba vyama vyote vinalenga kutoa huduma kwa raia. Chama chochote kinachofanikiwa kushinda, kinaunda serikali iliyowekwa madarakani na raia, na serikali hii inawajibika kwa wananchi. Tanzania inatumia mfumo wa uchaguzi ambao mgombea anayepata kura nyingi ndiye mshindi. Pia, Tanzania inatumia uwakilishi wa nusu uwiano katika uchaguzi wa wawakilishi wa wanawake katika Bunge. Uchaguzi Mkuu Tanzania hujumuisha uchaguzi wa rais, wabunge na serikali za mitaa. Haya yakiwa wazi kwa wapiga kura, haiwezekani kutokea vurugu.

Hivyo baada ya  kupata elimu ya kupiga kura raia aliye makini anafahamu ampigie kura nani, apige kura kwa masuala  gani na anakuwa anajua jinsi  ya kuwawajibisha viongozi wake, maana yeye ndiye anakuwa amewaweka madarakani. Na mwanachi huyu makini, hawezi kuruhusu mtu kupita bila kupingwa kama ilivyotokea Arumeru.

Raia makini ni lazima ajue na kutambua kwamba madhumuni ya uchaguzi ni kuwawezesha watu kuchagua wawakilishi na viongozi ambao watasimamia shughuli za umma kwa masilahi ya wapiga kura. Na kwamba wakishindwa kusimamia vizuri masilahi ya wapiga kura wanaweza kuondolewa.  Mpiga kura akijua hiivyo  hawezi kuuza kura yake na kulazimishwa kumchagua mtu ambaye hafai, akifanya hivyo akakubali kuuza kura yake anakuwa anajua kwamba kwa huru wake mwenyewe anajitia kitanzi.

Raia makini ni lazima atambue kwamba chaguzi ni muhimu kwa kuchagua viongozi wazuri, kuhakikisha utawala bora, kuwajibisha serikali kwa matendo yake, kuunda serikali inayopendwa na watu na kuboresha mfumo wa kisiasa na kwamba Tanzania imekuwa ikifanya uchaguzi mkuu kwa kuzingatia Katiba na Sheria ya Uchaguzi.

La msingi hapa ni kusisitiza kwamba wakati CCM inasherehekea kulipata Jimbo la Arumeru Mashariki bila kupiga kura, ukizingatia misingi ya demokrasia na uwakilishi wa wananchi, wakumbuke kwamba kupita bila kupingwa  ni dalili za kuizika demokrasia,  na hizi si dalili nzuri kwa taifa letu.

+255754633122

[email protected]

Please follow and like us:
Pin Share