Rais Dk. John Magufuli akiwa na Balozi wa Sweden nchini, Anders Sjoberg wakizindua mradi wa ujenzi wa njia kuu ya kusafirisha umeme KV 220 kutoka Makambako hadi Songea pamoja na vituo vya kupooza umeme KV 220/33 katika sherehe zilizofanyika Songea mkoani Ruvuma.

Ziara ya Rais Dk. John Pombe Magufuli mkoani Ruvuma imebadili mawazo ya wananchi baada ya kero zao kujibiwa lakini ikaacha majonzi kwa wananchi wilayani Songea Mjini kutokana na mkutano wa Rais kutekwa na mawaziri na kukatishwa na mvua kubwa iliyomkaribisha mkoani humo.

Ikiwa ni ziara yake ya kwanza mkoani Ruvuma tangu aingie madarakani Novemba 2015, Rais John Magufuli alileta hamasa kubwa kwa wananchi ambao walijitokeza kwa wingi, jambo ambalo kama si umahiri wa walinzi, ingemchukua muda mrefu kufika kituo cha mikutano, maana wananchi walionekana kutaka kuwa naye muda wote.

Wakati mwingine walinzi walilazimika kubadilisha mwelekeo, kwa kuwa rais kuna wakati alikuwa anawapiga chenga na kuwafuata wananchi, wadadisi wa mambo wanasema Ikulu inamkosesha kukutana na watu kwa urahisi.

Ziara hiyo imebadili mawazo ya awali ya wananchi mkoani Ruvuma ambao walikuwa wanasema kuwa wao ni yatima, hawana baba, lakini sasa wameondoa mawazo hayo na kusema kuwa Rais Magufuli ni mlezi bora kama bata anayetanguliza vifaranga mbele na yeye anabaki nyuma kuwalinda wasinyakuliwe na mwewe.

Awali wananchi mkoani Ruvuma mioyo yao ilikuwa chini kutokana na baadhi ya kero kama vile kupanda kwa bei ya pembejeo za kilimo, kutokuwepo kwa soko la uhakika la mazao yao yakiwemo mahindi na kahawa, umeme wa REA wananchi vijijini kutozwa Sh 270,000 badala ya Sh 27,000, kufufuliwa kwa kiwanda cha tumbaku Songea, kufutwa kwa vyuo vikuu Ruvuma, asilimia 10 inavyokwamisha miradi ya maendeleo Ruvuma na hatima ya fidia ya EPZ Mwengemshindo na eneo la Soko la mazao Namanditi Songea kutopatiwa majibu.

Wafanya biashara wadogo walikuwa na uelewa tofauti kuhusu nani anastahili kupewa kitambulisho kinachouzwa Sh 20,000 kwani fikra zao zilikuwa kama vile muuza mbogamboga mwenye mtaji wa Sh 2,000 au Sh 5,000 hatakiwi kuwa na kitambulisho, hivyo utaratibu huo kwao waliona kama manyanyaso.

Waendesha pikipiki (bodaboda) walikumbwa na ombwe hilo hilo kama na wao wanastahili kupewa vitambulisho hivyo, kwani biashara yao ina utaratibu tofauti, hivyo kulazimishwa kuchukua vitambulisho hivyo kwao walishindwa kupata majibu na kubaki njia panda.

Yalikuwepo manung’uniko ya kutotembelewa na rais, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) huku wakiamini kwamba Mkoa wa Ruvuma ni ngome ya CCM.

Akijibu kero za wananchi mkoani Ruvuma, Rais Magufuli anasema vitambulisho vya wafanyabiashara ndogondogo vina manufaa kwani vitachochea kukua kwa biashara yao pamoja na kuwawezesha kubuni biashara nyingine na kwenda kuuzia mahali popote, jambo ambalo pengine lilikuwa linakwamishwa na ushuru uliokuwa unaambatana na kamatakamata ya mgambo wa halmashauri.

Na kuhusu waendesha bodaboda, Rais Magufuli anasema wasibughudhiwe kwa kukataa kulipia vitambulisho, hivyo kwa kuwa wao wana utaratibu unaokwenda sambamba na sheria ya kumiliki chombo cha moto.

Kimsingi biashara ni matangazo, hivyo ujio wa rais umeleta hamasa kwa wawekezaji kwani vyombo vya habari vimeweza kuutangaza mkoa na fursa zilizopo kama vile madini, mvua ya uhakika, maeneo mazuri ya kilimo, utalii, maeneo ya kujenga viwanda kutokana na kuwepo kwa umeme wa uhakika wa Grid ya Taifa – kikwazo ambacho kwa miaka mingi kilikwamisha uwekezaji mkoani Ruvuma.

Kwa upande wao umoja wa wafanyabiashara mkoani Ruvuma wanalia na makadirio ya mapato kutoka TRA, ambao mara nyingi biashara zao wanawategemea sana wakulima, hivyo wakulima wakifeli kuuza mazao yao basi na biashara inakwama.

Mwenyekiti wa umoja huo, Titto Mwilamba, amethibitisha kilio hicho ambacho hakijapata majibu kufuatia ziara ya rais, ambapo walitegemea kiu yao hiyo ingepatiwa majibu katika Uwanja wa Majimaji lakini wameishia kubaki na mshangao.

“Kwa hakika tangu mwaka 2016 hadi 2018 biashara mkoani Ruvuma ilikuwa ngumu hadi imesababisha maduka zaidi ya 1,400 yamefungwa na kwa Songea peke yake ni zaidi ya 600 yamefungwa kutokana na makadirio ya TRA kuwa juu kuliko hali halisi ya kibiashara, kwani wao wanawategemea wakulima ambao wakikosa na wao hakuna biashara,” anasema Mwilamba.

Anasema wao walidhani ujio wa rais ungewapatia majibu ya hasara waliyoipata wakulima kwa miaka mitatu  mfululizo tangu 2016 hadi 2018 kutokana na mazao yao kukosa soko la uhakika, kwa mfano hadi wakauza mahindi kwa hasara Sh. 150 kwa kilo, hivyo walitegemea kusikia pengine wanapewa tena mbolea ya ruzuku ili kufidia hasara hiyo, lakini hadi sasa wamebaki na mizigo yao ya kero.

Mwilamba anasema kufika kwa umeme wa gridi ya taifa mkoani Ruvuma kungekuwa na manufaa makubwa lakini umeme huo bila wakulima kuzalisha malighafi kama vile mahindi kwa wingi kwa ajili ya viwanda vya kuchakata sembe, watu watajenga viwanda na kukaanavyo, jambo ambalo walitegemea rais angezungumzia lakini wameishia kuwasikia mawaziri na mbwembwe zao badala ya kumwachia rais ambaye ndiye alikuwa anasubiriwa kwa hamu azungumze.

Anasema kwa kweli mawaziri wanapaswa kuwaomba radhi wananchi wa Songea Mjini kwa kitendo chao cha kuuteka mkutano wa rais na kummalizia muda wake wa kuhutubia wananchi, ikizingatiwa Songea Mjini ni kitovu cha Mkoa wa Ruvuma, hivyo ilipaswa kabisa rais akate kiu ya wananchi wa hapo.

“Mawaziri wana uwanja wa ndani kwenye vikao vyao vya baraza la mawaziri lakini pia wana magari na bajeti za kutembea kwenye mikoa na kuyasema yale waliyoyasema, sasa kitendo cha kuuteka mkutano wa rais na kusababisha asikate kiu ya wananchi wao wanajisikiaje?” anahoji mmoja wa wananchi.

Mmoja wa wananchi hao, Nathaniel Lugongo, mtaalamu wa ujenzi wa line kubwa na ndogo, upimaji line za umeme na ukaguzi wa mita ngazi ya kanda Kurugenzi ya Mto Pangani anasema wananchi Songea hawajafurahishwa na ujio wa rais kwa sababu hakukata kiu yao ya maendeleo ya uchumi wa kati na viwanda.

Anasema katika ziara hiyo walitegemea Rais Magufuli atazungumzia kufufuliwa kwa kiwanda cha tumbaku Songea ambacho kilikuwa kinaajiri wafanyakazi zaidi ya 3,000 na hivyo kuufanya mji wa Songea kuwa na mzunguko mzuri wa fedha.

Lugongo anasema wananchi walitaka kusikia kauli ya rais kuhusu soko la uhakika la mazao yao, ikiwemo mahindi ya ziada ambayo ndiyo yanauzwa na wakulima wa Songea miaka yote na huwa wanajivunia zao hilo kwa kuongeza uzalishaji ili kukidhi soko la ndani na nje ya nchi.

Pia walitaka kusikia rais anasema nini kuhusu kufutwa kwa vyuo vikuu mkoani Ruvuma ambavyo takriban zaidi ya miaka 46 tangu uhuru, Ruvuma haijawahi kuwa na chuo kikuu na ndiyo maana hata mwamko wa kielimu ulikuwa duni hadi miaka ya kuanzia 2013 hadi sasa wananchi walianza kupata mwamko wa kuwa na matamanio ya watoto wao kufika chuo kikuu baada ya kuhamasika kuwaona wenzao wakiwa vyuoni.

“Unajua panapokuwa na chuo kikuu ina maana kuna kitu ambacho kinatakiwa kuondolewa kama ilivyo Ruvuma kulikuwa hakuna mwamko wa elimu ya juu ya vyuo vikuu na huo ndiyo upekee ‘uniqueness’ ambao unaondolewa na uwepo wa vyuo vikuu,” anasema Lugongo.

Wakati huo huo pango la nyumba wanachuo hao walikuwa wanalipa wastani wa Sh milioni 30 kwa mwezi jambo ambalo endapo serikali ingekuwa inafuatilia kodi iitwayo “withholding tax” kwa mwezi serikali ingeweza kukusanya wastani wa Sh milioni 3 bila kujumuisha idadi ya wanachuo cha SAUT tawi la AJUCO Songea, ambacho kilikuwa na zaidi ya wanachuo 1,000 kabla ya kusitishiwa udahiri, yaani kuandikishwa wanafunzi wapya kwa zaidi ya miaka miwili sasa.

Katika ziara hiyo ya rais, wananchi na waumini walishangazwa na kitendo cha Mhashamu Askofu Mkuu Damian Dallu wa Jimbo Kuu la Songea kutotoka nje au kanisani kusalimiana na rais, ambaye alisali misa ya kwanza katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Mathias Mulumba Kalemba lililopo mjini Songea.

Baadhi wa waumini wa Kanisa Katoliki wameliambia Gazeti la JAMHURI kwamba kitendo cha askofu kutoshiriki ziara ya rais kimeacha doa. Askofu Damian Dallu hakupatikana kuzungumzia suala hilo.

“Kibaya zaidi, rais akiwa uwanjani mbele za watu lukuki aliitwa mara tatu Askofu wa Jimbo Katoliki au mwakilishi wake kwa ajili ya kutoa dua ikawa kimya wakati madhehebu mengine yalishiriki ziara hiyo, hii ni hatari sana,” wanasikika wakisema waumini hao.

Jambo jingine ambalo liliacha tashwishwi kwa wananchi ni kutoonekana kwa Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Christina Mndeme, ambaye kwenye ziara yote ya rais hakuwepo na majukumu yake yalikaimiwa na Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Godfrey Zambi.

Kumekuwepo na minong’ono kuhusu kutokuwepo kwa Mndeme, huku baadhu wakisema ametumbuliwa kimya kimya, wengine wakisema yuko kwenye matibabu na wengine wanasema amepangiwa majukumu mengine na rais.

Uchunguzi uliofanywa na Gazeti la JAMHURI umebaini kwamba Mkuu wa Mkoa huyo wa Ruvuma wakati wa ziara ya Rais Magufuli alikuwa Dar es Salaam kwa ajili ya uchunguzi wa kitabibu.

Please follow and like us:
Pin Share