Nianze kwa kuwatakia heri ya Pasaka pamoja na Sikukuu ya Wafanyakazi. Wiki mbili zilizopita ambazo zimekuwa na siku za mapumziko nyingi, zimenipa nafasi ya kutafakari kuhusu namna Rais Dk. John Magufuli anavyofanya kazi zake.

Wiki moja kabla ya Pasaka rais alikuwa ziarani mkoani Ruvuma. Kwanza nimpongeze kwa kufanya ziara ambayo kwa hakika imeponya mioyo ya Wana Ruvuma kwa kiasi kikubwa. Si nia yangu kuzungumzia ziara ya rais mkoani Ruvuma na sasa yupo Mbeya.

Ziara hizo za rais mikoani zimekuwa zikionyesha dhahiri kwamba kuna ombwe la uongozi, ama wananchi wanatamani kuona Rais Magufuli akishughulikia kero na changamoto zao yeye mwenyewe. Baadhi ya kero katika ziara za Rais Magufuli mikoani ni pamoja na migogoro ya ardhi, baadhi ya maeneo kutopata maji na polisi kuwa kero kwa wananchi – kwa uchache.

Ukiwasikiliza kwa makini wananchi ambao kwa hakika wamekuwa wanajitokeza kwa wingi kumsikiliza Rais Magufuli ikiwa ni pamoja na kumweleza kero zao, utagundua kwamba wananchi wamekosa sehemu ya kupeleka malalamiko yao ili yashughulikiwe, ama viongozi katika ngazi ya wilaya na mkoa wamekuwa miungu watu.

Utaratibu wa Rais Magufuli wa kuambatana na baadhi ya mawaziri ambao kwa uzoefu, kumekuwa na maswali mengi yanayohusu wizara wanazoziongoza kutoka kwa wananchi, wamekuwa wanatumia fursa hiyo kujibu kero za wananchi.

Wananchi ndio waajiri wa serikali iliyopo madarakani. Pengine ziara za Rais Magufuli zingekuwa zinampatia furaha zaidi kama wananchi wangekuwa wanamweleza kuhusu serikali yake inavyowahudumia. Kuna kila sababu ya viongozi wetu kujitafakari.

Hivi ni sahihi rais kuulizwa swali kuhusu maji, wakati kwenye wilaya husika katika ofisi ya mkurugenzi kuna mhandisi wa maji, achilia mbali mkoani na hata wizarani? Wananchi wanashtaki kwamba hawapati maji na kwamba kama yamepatikana basi ni kwa sababu rais ametembelea eneo husika na wahusika wana hofu ya kutumbuliwa, basi wanapeleka maji kwa wananchi.

Wakati mwingine ninajiuliza, hivi viongozi wetu hao wanamdanganya nani? Kama eneo husika halipati maji ni busara likatengenezewa mkakati na kutengewa bajeti ili wananchi waendelee kufaidi matunda ya uhuru. Lakini hali imekuwa tofauti, waliopewa hizo dhamana wanaona kuwatendea wananchi wema ni kama hisani.

Ni wakati muafaka sasa viongozi katika ngazi zote kusimamia suala la maendeleo ya wananchi, ikiwa ni pamoja na kutatua kero zao. Viyoyozi ndani ya magari na ofisini visiwapofushe na kuwasahau wananchi wanyonge ambao hata kusoma kwenu kumechangiwa na kodi zao.

Simfagilii, lakini acha niseme tu. Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi, amekuwa akifanya mambo kwa kweli mpaka ninamuonea wivu. sitamani kuwa waziri, isipokuwa namna anavyohangaika na kero za wananchi kwenye ardhi, hasubiri kuzijibu katika ziara za rais.

Wengine wanaojaribu kutatua kero za wananchi, wanazitatua na kurusha kwenye mitandao ya kijamii, pengine ndiyo ile kauli ya ‘biashara matangazo!’ Lakini hivi kweli ile kauli ya ‘tenda wema, nenda zako’ bado inafanya kazi katika kizazi cha viongozi ambao wanafanya kazi ili waonwe na mamlaka za uteuzi?

Ninafikiri kama tungekuwa na utaratibu wa viongozi kurudi kwenye nafasi zao kwa kuhusisha kura ya maoni kwa wananchi anaowaongoza, sijui ni wangapi wanaweza kurudi. Viongozi mlioaminiwa tumieni karama zenu za uongozi katika kuwaletea wananchi maendeleo.

0756 394 119

Please follow and like us:
Pin Share