Ndugu Rais tumwombe Mwenyezi Mungu asikae mbali na sisi maskini wake, bali atukaribie! Mavuvuzela yamesimama mbele yetu, ona wanayotufanyia.
Muumba usifiche uso wako wakati wa taabu zetu; wakati tunapolia sana! Sikia maombi ya watoto wako ushuke, tunaangamia. Shuka utusaidie.
Tunapotafakari uwezo wako Mungu, wewe ni baba yetu na una kila kitu! Ni nani asiyejua heshima yako na uwezo wako jinsi ulivyo? Mavuvuzela wanaulizana, hawa maskini Mungu wao yuko wapi? Kisha wanatutema mate.
Wakati wanaendelea kukudharau na kukufanya kama vile haupo tunasema kwa nguvu kubwa kuwa, uonyeshe ulimwengu kama wewe upo na sisi masikini ni waja wako. Kama umande mzuri unyesheavyo shamba, ndivyo Mungu wetu anavyotupenda. Ndugu Rais, hakuna mwingine wa kuwaunganisha Watanzania waliosambaratika ila ni wewe kiongozi mkuu. Tuunganishe
tuwe kundi moja na wewe ukiwa mchunga mmoja. Tuunganishe wote tuwe sisi na wala wao wasiwepo.
Ndugu Rais tunapoushangilia u-vuvuzela wetu wananchi wanauliza ni akili gani inayotumika kutumia mabilioni yote haya kwa chaguzi za marudio?
Wananchi hawana dawa katika hospitali zao. Nchi nzima inalia kilio cha kukosa maji. Wengine hata hawajui kula yao ya siku itatoka wapi.
Wamekata tamaa na kusawajika. Idadi ya watakaochagua mtu badala ya chama 2020 itakuwa kubwa. Huyu aliandika, “Huwa nasoma makala yako nikiwa na amani moyoni, hongera sana mzee wangu. Mavuvuzela
wanashangilia ushindi kwa kubebwa. Siku inakuja ukweli utasimama! Watanzania kuna siku watasema NO MORE UVUVUZELA. Mungu amrehemu Jwan Mwaikusa, aliandika shairi, THINKING IS PROHIBITED. Summons, ilikuwa miaka ya 60, sasa tunazuiwa leo! Siku njema mzee wangu.”
Ningekuwa karibu na wewe baba ningekuambia uachane na hadithi ya viwanda, hangaikia uvuvuzela huu wa chaguzi za marudio. Kukata mzizi wa fitna weka refarii ambaye hana kadi ya chama chochote ili achezeshe mchezo kwa haki. Kuogopa tume huru hakuna maana nyingine yoyote zaidi ya kutaka kuendeleza ushindi wa dhuluma. Huo ni uvuvuzela!
Mwanamwema kaja na dukuduku akisema, “Ndugu Mwalimu Mkuu niliposoma makala yako juu ya Stiegler’s Gorge nilipata uelewa tofauti na niliokuwa nao. Miaka yote nilidhani Mwalimu Nyerere hakujenga umeme Stiegler’s Gorge kwa kuwa alikosa fedha kumbe sivyo!”

Nilichomjibu ni kwamba sikuwapo katika mawazo ya Mwalimu Nyerere wakati ule. Ninachokifanya sasa ni kufikiri tu. Kwa kuwa wote wanaojua wanajua bila
kuwa na shaka yoyote kuwa sehemu ile ya nchi yetu ilikubaliwa kuwa ni urithi wa dunia, basi tunajua kuwa yalifanyika makubaliano kati ya dunia kwa upande mmoja na nchi yetu kwa upande mwingine. Dunia iliridhia na nchi yetu wakati huo ni Baba wa Taifa Mwalimu Julius
Kambarage Nyerere akaridhia. Mpaka mzee wa watu anaingia kaburini hakuwahi kuwaambia Watanzania na wala kuiambia dunia kuwa hakubaliani makubaliano hayo. Anapotokea wa kutokea na kutuambia kuwa Nyerere
alikuwa na mawazo ya kuujenga umeme katika sehemu ile ile aliyoikubalia dunia kuwa itakuwa ni kwa ajili ya urithi wana wa dunia yote, mwogopeni. Wa kale walisema mwenye nguvu mpisheni. Lakini Watanzania wote walijua kuwa Nyerere na roho yake hakutawaliwa na tamaa ya mali nyingi. Ukiuita huu mradi kwa jina la Mwenyeheri Julius, halafu wakatokea watu wakasema huko ni kumtukana marehemu, nitapata wapi
sababu za kuwakatalia? Wako wanaoona huko ni kutaka kuishusha heshima kubwa anayopewa Mwalimu Nyerere na dunia. Kwa hili tumwachie Mwenyeheri mwenyewe. Akishakuwa Mtakatifu utetezi wake utakuwa ni laana kwao.
Nafarijika sana kila ninaposikia kuwa Bwana Nape analia bungeni. Wananchi wa Mtama ni wangapi wanaoweza kuifikia youtube ili wamuone mbunge wao anavyowalilia bungeni? Kilio chake bungeni sawa na kilio cha samaki. Machozi yake yanaenda na maji. Hakuna walichosema wa kale wakakosea. Walisema, “Mchimba kaburi, huingia mwenyewe!” Tumuulize ni nani aliyechimba kaburi lilimozimwa Bunge? Huu si wakati wa kulia. Ni wakati wa kujutia maovu tuliyoyasimamia tukidhani uchungu wataupata wengine tu. Panga haliijui shingo la aliyelitengeneza.
Ndugu Rais, wananchi wanafarijika sana kuona viongozi wao wakuu wakisambaa katika nchi kuona miradi ya maendeleo na kuwasikiliza.
Katika hili baba, Serikali ya Awamu ya Tano inastahili pongezi. Ni kweli elimu ya darasani huko vijijini ni ndogo, lakini hii haimaanishi kuwa wananchi wa vijijini ni wajinga kiasi cha kushindwa kuelewa kile wanachoambiwa na viongozi wao. Mama yetu mpendwa Makamu wa Rais ni
mwanasiasa kwa asilimia mia moja. Alipoenda Kigoma aliingia kanisani kulikokuwa kunafanyika shughuli za kidini kwa asilimia mia moja.
Katikati ya ibada akaanza siasa kuwataka waumini akisema, “Msichanganye dini na siasa”. Mwanasiasa kuhutubia kanisani tena wakati wa ibada, ni kufanya nini kama siyo kuchanganya siasa na dini.
Hizi hotuba za kuandikiwa ni muhimu msomaji mwenyewe kwanza akaelewa vizuri kile alichoandikiwa kabla hajawasomea wananchi. Kama huko siyo kuchanganya dini na siasa ni kuchanganya nini na nini? Au kuchanganya dini na siasa ni zile nyaraka za viongozi wa dini zilizowataka viongozi wa siasa kuzingatia utawala wa sheria na kuheshimu haki za binadamu? Zilizowataka kuwakamata watu wasiojulikana. Hawakuwa mashetani waliotoka kuzimu. Tusiwape wengine sababu ya kuhoji uwezo wetu wa kuelewa.
Ndugu Rais, historia ikikandamizwa kwa fikra jadidi hutoa majibu yote ya kesho tena kwa usahihi kabisa. Tokea siku ya kwanza ilipotolewa tu ahadi ya Sh milioni 50 kwa kila kijiji, historia ilionyesha wazi kuwa hazilipiki na hazitalipika. Leo kiongozi anasema kupanga ni kuchagua.
Watalipa, lakini siyo kulipa kama walivyoahidi. Waliosema ahadi ni deni walikuwa ni watu wenye akili kubwa. Na hao hao ndiyo waliotuambia kuwa dawa ya deni ni kulipa. Kama kupanga ni kuchagua tusijifanye tumejua
leo. Tulipaswa kujua tangu siku ile ile tuliyokuwa tunaitoa ahadi.
Wakitujua kuwa ndiyo tumejua leo, ah! Watatucheka watu!
Viongozi wetu sasa kila wanapopita mawazo yao ni uchaguzi mkuu 2020. Utamsikia kiongozi anawaambia wamachinga na akina mama maneno ya kuwapa faraja. Na kwanini sasa kama siyo kampeni za mapema zinazotokana na hofu ya kutojiamini?

 

.tamati….

Please follow and like us:
Pin Share