Ndugu Rais, watu wako wamekusikia vema kwa yote uliyoyasema Novemba Mosi, 2018 katika kongamano la siasa na uchumi lililofanyika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam katika ukumbi wa Nkrumah. Wamekusikiliza tangu ulivyoanza mpaka ulivyomaliza. Sitaki nikufananishe na mtu yeyote, lakini ulinikumbusha ile hotuba kuu aliyoitoa Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere katika ukumbi wa Simba pale ilipokuwa ikiitwa The Kilimanjaro Hotel. Mwalimu Nyerere alisema, ‘’Sikujitayarisha kiasi cha kuyaandika haya nitakayoyasema, hivyo mniwie radhi kama yatakosa mpangilio kwa sababu nitalazimika kufanya yote mawili. Huku nitakuwa nasema na huku nitakuwa nafikiri’’.

Pamoja na ile hotuba aliyoitoa Mbeya hii nayo ilikuwa kati ya hotuba kuu alizotuachia Baba wa Taifa kama urithi wetu wana wa nchi hii.

Baba, hotuba yako ile, ilikuwa njema sana. Na wewe siku ile ulionekana kama hukujitayarisha kiasi cha kuiandika hivyo kama Nyerere kwa hilo, ulikuwa huku unasema huku unafikiri. Inahitajika akili kubwa.

Ulionekana mpole na mwema sana na kwa kweli ulipendeza sana kwa baadhi ya kauli zako. Ndipo likaja wazo kuwa kumbe kukaripia au kuzungumza maneno kwa hasira au kugomba na kufokafoka kunambomoa mtu mwenyewe na kupoteza maana ya yote anayoyasema na hivyo kumfanya mtu huyo aonekane kituko.

Baba kwa hotuba ile unaweza ukatunyoosha kwa upendo nasi tukanyooka. Ulizungumza vema sana. Ubarikiwe sana kwa hili. Kama vile mwanadamu alivyoumbwa kuchukia kusimangwa ndivyo alivyoumbwa kuchukia kufokewa kwa kila jambo. Umerudisha matumaini ya wengi ya kutaka kukusikiliza tena mara nyingine.

Yaliyojiri katika kongamano lile yalikuwa mengi na muhimu, lakini yaonekana kiu kwa mambo mawili haikuzimwa na hivyo kuibua fikra za wasikilizaji. Imekuwa ni kawaida sasa kila unapotajwa mradi wa Stigler’s Gorge serikali hujibu kwa nguvu na huku ikitoa vitisho.

Tulisikia bungeni, Ninja akisema, ‘’Mnaoubishia, piga ua, tutawapiga na kuwagalagaza na tutawatia jela.’’

Hivi mwananchi kuwa na mawazo tofauti ni jinai inayomfanya astahili jela? Aliyeyasema haya siyo hakimu, ni yule aliyekabidhiwa dhamana ya kulinda maisha ya wananchi na mali zao. Ndiye mmiliki wa virungu vyote vya polisi, bunduki zao na polisi wenyewe; na ndiye mwenye funguo za magereza yote. Wanajiuliza, utawala wa sheria hapo uko wapi? Mwingine kaibuka na vitisho vya kizamani enzi za marehemu Amin Dada na wenzake na kusema, ‘’Iwe jua, ije mvua mradi tutajenga.’’ Mwananchi wa kawaida ambaye hajui chochote ana sababu ya kujiuliza, nguvu na vitisho vyote hivi ni vya nini?

Kunani katika mradi huu? Ni umeme tu? Wanaobishia wanatoa athari gani kwa mradi huu? Wanakwenda kuchimbua barabara ili vifaa vya ujenzi visipelekwe huko? Kwa staili hii mpaka kuondoka mtawafunga Watanzania wangapi? Wakati wa kuondoka ukifika mtaondoka kwa ridhaa?

Wazushi katika hili hawajakosekana. Wengine wanaanza kusema eti Baba wa Taifa alikuwa na nia ya kuujenga mradi huo, lakini akakosa fedha.

Sasa Mtera alijenga kwa mikono? Kwanini fedha alizojengea Mtera hakuzipeleka huko? Kama mradi huu ni kwa faida ya nchi na Watanzania wote kwanini usijengwe kama inavyojengwa miradi mingine bila kutisha wananchi? Ni busara kwa baadhi ya viongozi wetu wakaziheshimu fikra sahihi za Baba wa Taifa pale aliposema, ‘’Wananchi wanapoonyesha uamuzi wa kipumbavu, wanatumia haki yao ya kiraia. Wanaponung’unika kwa uamuzi ambao si wa kipumbavu wanaweza wakaelekezwa mpaka wakaelewa kwanini uamuzi ule ulifanyika, na faida zake ni nini” Uk. wa 128-129 katika kitabu cha nukuu za Kiswahili za Mwalimu Nyerere.

Ilitamkwa katika kongamano kuwa Katiba mpya ni hitaji la Watanzania wengi. Kutambua kiu ya Katiba mpya walionao wananchi wengi, lakini tukawataka wananchi hao hao waendelee wachape kazi kwa Katiba iliyopo ambayo inalalamikiwa kuwa ina upungufu ni kuongeza ukubwa wa kiu ya Katiba mpya kwa wananchi hao.

Kusema sitarajii kutenga fedha kukidhi matakwa ya wananchi walio wengi katika nchi zinazoendeshwa kidemokrasia kunaweza kuzua tafrani kubwa. Nchi ni mali ya wananchi. Siyo mali ya viongozi. Matakwa ya wananchi ndiyo matakwa ya nchi.

Kukataa kutii matakwa yao ni kuikataa kazi tuliyokabidhiwa. Mtu unapoteza sababu ya kubaki kuwa kiongozi. Tuna maana gani tunapowataka wengine kuwa wazalendo huku wenyewe tukiwa hatutarajii kutekeleza matakwa ya nchi na ya wale waliotuweka madarakani? Tumeona katika nchi nyingi bila katiba njema amani inapotea. Amani ikipotea katika nchi utakuzaje kilimo wakati wakulima wametawanyika? Amani ikishatoweka ni nani atabaki anafyatua matofali ya kujengea Stigler’ Gorge? Kwa hili yatupasa kujitafakari upya. Ndugu Mwakyembe aliwahi kusema bungeni kuwa Watanzania siyo mabwege. Wanaweza kuja kutujibu 2020.

Baada ya kufuatilia kongamano mwanamwema mzee mstaafu kutoka Iringa alinitumia ujumbe ufuatao, ‘’Profesa Rwekaza Mukandala alitimiza wajibu wake kwa jamii. Mukandala ni Mhaya. Naishi Iringa, lakini kwa kabila mimi ni Mhaya. Kwao anakotoka Mukandala wana methali isemayo, bagambila balinsi, ab’eigurukuhulililaho. Akaniambia maana yake ni kwamba unapowaonya walioko ardhini walioko juu ya ardhi wanasikia.’’

Akasema walio na masikio ya kusikia wamesikia.

Akitoa mada juu ya utawala na siasa kwa mtindo wa maswali matano msomi wa sayansi na siasa Mukandala alimtaka kila mshiriki ampe alama ndugu Rais anazoona anastahili katika maeneo hayo matano. Aliuliza je, kumekuwa na uelewa wa ulimwengu na changamoto zake pamoja na kuainisha matatizo ya mfumo huu wa kimataifa? Kumekuwa na uelewa na uchambuzi wa hali ya nchi yetu, changamoto zake na jinsi ya kuzitatua?

Akahoji, ‘’Rais kama kiongozi mkuu wa siasa ameweza kuongoza kuwa mstari wa mbele kwa mawazo na vitendo? Ameweza kuhamasisha wananchi wamfuate, je ameweza kubuni lugha mahsusi na muafaka inayochangamsha na kujenga upendo, utashi na utiifu kwake? Katika uongozi ni lazima kuangalia madaraka yanatumiwa vipi, kwa manufaa ya nani na kwa kufuata sheria na katiba au la.

Wengi walimshangilia aliposema, ‘’Baba anaweza kuleta chakula nyumbani kila siku, lakini mama na watoto wakawa hawana raha, hivyo hawezi kusema kuwa ana mafanikio wakati familia haina raha’’.

Baba tunyooshe kwa upendo na si vinginevyo. Tutanyooka tu!

By Jamhuri