Ndugu Rais, yawezekana katika maisha yetu tulishawatuma wapumbavu wengi tu. Kwa maisha yetu ya hapa duniani hao sasa ndio wanaozishikilia funguo za milango ya magereza yetu.

Kama kuna pepo na moto baada ya sisi kupita, hao ndio wanaotusafishia njia yetu iendayo Jehanamu. Kuingia katika mji ule itakuwa ni vigumu, sawa na ngamia kupita katika tundu la sindano. Mpaka Mwenyezi Mungu mwenyewe apende. Imeandikwa, hakuna chochote kinyonge kitakachoingia katika mji ule! Taa ya mji ule ni mwanakondoo. Huhitaji jua wala mwezi.

Baba, tukio la kushushiwa kipigo cha mbwa koko yule kijana maskini wa Makambako mpaka leo bado linaizungusha dunia. Baba alikosa nini lakini, yule kijana mnyonge? Umati mkubwa uliokuwa umekusanyika ulishindwa kuvumilia kuona unyama kama ule ukifanyika mbele yake, uliingilia kati kutaka kumuokoa.

Kwa bahati mbaya, ilitoka sauti kutoka juu ikiamuru kwa ukali: “Mwacheni wamshughulikie.’’ Umati ulisinyaa kuupisha unyama uendelee! Wanakosea wapi wanaotuona tumejaa hofu mwili mzima kila wakati bila sababu yoyote? Kumbe mnyonge yule alikuwa na bango lake alitaka baba yake asome ili ajue madhila yanayoisibu jamii yake kwa hila zilizokuwa zikifanywa na waliokabidhiwa mamlaka ya kugawa maji kwa wananchi.

Lakini amri ya mwacheni ashughulikiwe ilitolewa hata kabla ujumbe wake kwenye bango lake haujasomwa! Tumejaa hofu. Tusome mabango yao ili tujue shida zao. Ni dhambi gani kubwa tuliyowafanyia wananchi wa nchi hii hata itujaze hofu hivi?

Nikifikishwa hapa hukumbuka yale maandiko yasemayo: “Mjapoteswa kwa sababu ya haki, mna heri, msiogope kutisha kwao. Kwa kuwa macho ya Bwana huwaelekea wenye haki na masikio yake husikia maombi yao, bali uso wake Bwana, ni juu ya watenda dhambi, hukumu yao ni Jehanamu!’’ Abarikiwe sana dada Fatma Karume kwa ufafanuzi wake makini kwa Watanzania kuwa: “Mpumbavu ukimwita mpumbavu si kumtukana.”

Haumtukani bali unamwita kwa wadhifa wake. Ndiyo, kumbe umwiteje? Dunia bado inajiuliza, ni nani aliwatuma waliompa kisago kijana wa Makambako? Mpaka leo hawajaguswa. Baba ni kweli hata hawa hawajulikani? Wananchi wana haki ya kujiuliza, hawa wasiojulikana wanatumwa na nani? Nchi ni Rais. Serikali ni Rais. Kama hivyo ndivyo ilivyo, nani anawatuma wasiojulikana, rais hawezi kukwepa kuwa mtu wa mwanzo kutupiwa jicho!

Ndugu Rais, unapofanya jema wanao tunaona na kukiri. Kutembelea magereza baba ubarikiwe sana. Wengi wasio na hatia wamewekwa huru. Wanaosema wote walio mahakamani kwa muda mrefu kwa tuhuma zenye utata, au wahukumiwe au waachiwe huru hawatetei ufisadi wala mafisadi. Wanatetea utu wa mwanadamu.

Ili kesi ya ESCROW kwa mfano, imalizike kwa haki inayoonekana ni lazima pande zote mbili ziwepo mahakamani mbele ya hakimu. Upande wa waliokuwa nje ya kaunta wakapokea fedha na upande wa waliokuwa ndani ya kaunta wakaruhusu fedha zitolewe.

Iletwe hundi au kibali mbele ya hakimu iliyosainiwa na wote waliosaini. Tofauti na hivyo baba nia yako njema ya kupambana na ufisadi itatafsiriwa na wote wenye moyo safi na dunia kwa ujumla kama uvunjifu wa haki za binadamu. Tuogope kuwatuma wapumbavu kwa sababu tutakaohukumiwa ni sisi!

Ndugu Rais, umetamka maneno ya mwenyeheri: “Sitaki kutawala nchi ya machozi.’’ Mungu akuinue! Umesema katika kipindi chako cha utawala usingependa kuona unatawala wananchi ambao wamejawa machozi kwa kuwa unaamini, machozi hayo yatakuja kukuumiza. Hautaki kutawala nchi ya watu wanaosikitika waliopo kwenye unyonge!

Ukiwa katika Gereza la Butimba ulitabiri kuwa wewe na sisi ni wafungwa watarajiwa! Wengine tuliamini kuwa tu marehemu watarajiwa, kumbe hata kufungwa tutarajie! Kwa kuithamini amani na upendo kati ya wananchi, watu wa mataifa mbalimbali walikaribishwa Kongwa kupigania amani. Tusiwasukume wananchi wetu kwenda kuitafuta Kongwa nyingine duniani.

Baba kama ikikupendeza, kwa nini tusinunue ndege mbili badala ya tatu ulizosema ili fedha za hii moja tuwawekee wananchi dawa katika zahanati na hospitali zao? Majukwaa yote yamejaa tambo za mabilioni yaliyotengwa kwa ajili ya afya ya wananchi huku katika zahanati na hospitali zao hakuna dawa wala vifaa vya tiba.

Wanataka dawa, siyo zimetengwa bilioni ngapi. Kuna nini baba katika ununuzi wa ndege? Wananchi walishirikishwa katika kuamua kipi kianze? Ni wazazi gani ambao watoto wao 342 watakuwa wamerundikwa sakafuni katika darasa moja, bila madawati wala vitabu kama wale wa Shule ya Msingi Msowola, Wilaya ya Kilosa mkoani Morogoro watamwelewa anayewaletea hadithi za ndege? Imekifu kusikia majukwaani mabilioni yasiyoonekana yaliyotengwa kwa ajili ya elimu.

Baba umesema waliogombea ubunge na Job Ndugai wote uliwateua katika nafasi mbalimbali. Ajira siku hizi mpaka uteuliwe. “Wengine wakurugenzi na Ma – DC. Nitawashangaa sana kama mwaka 2020 watakuja kugombea hapa. Wakija wajue U-DC, ukurugenzi hawatauona tena na nalisema hili kwa dhati.’’

Bila mbeleko ya hongo watumia magongo hawachaguliki. Natafakari hali ya aliyepigwa gongo la kichwa hadi kuzimia; malipo haya yanamtosha asirudi tena kugombea? Huwezi kujua, anaweza akaja kuwa spika naye akawa anatibiwa India. Mahitaji ya msingi na muhimu kwa Watanzania ni kuwa na kiongozi bora. Kamwe, abadani, bilikuli, katu, asilani wananchi hawatamchagua yeyote mwenye fikra za kuwa mtawala wao! Baba, tunajinywesha sumu, tukitegemea wafe wengine!

Mwaka 1994 pensheni yangu ilikuwa Sh 6,200 kwa mwezi. Baba akaongeza zikawa Sh 20,000. Alipokuja baba mwingine akaniongezea zikawa Sh 50,000. Yakaribia miaka kumi sasa tangu wewe baba yangu haujaniongezea hata thumuni. Du! Nasema mimi lakini haya ndiyo machozi ya wazee, wazazi wetu wastaafu. Wanasali tupite haraka. Wafanyakazi tumeona kule Mbeya wakati wa Mei Dei, machozi yakiwamwagika! Walimu wamejaa machozi. Wakulima wa korosho na sasa wa pamba wamejaa machozi. Wauguzi na madaktari wamejaa machozi.

Walioshindwa kukomboa miili ya wafu wao kwa ukubwa wa kikombozi wamejaa machozi. Wafanyabiashara, wamachinga na mama nitilie, wamejaa machozi. Baba hawa ndio wananchi unaowatawala. Unaitawala nchi iliyojaa machozi ya mama zetu, dada zetu na binti zetu na machozi ya vichanga vyao wanavyojifungulia sakafuni.

By Jamhuri