Na Mwandishi Wetu,JamhuriMedia

Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), limetangaza kuanza kampeni kabambe ya kukusanya madeni kwa wapangaji wa nyumba zake waliopo na waliohama ili kuhakikisha wanakusanya madeni hayo yanayofikia kiasi cha shilingi bilioni 26.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Oktoba 30,jijini Dar es Salaam Meneja wa habari na Uhusiano Shirika la Nyumba NHC ,Muungano Saguya amesema NHC ilikuwa ikidai madeni yaliyofikia sh.bil.26 ambapo kati ya hizo sh.bil.5 zilikusanywa huku sh.bil.21 bado hazijakuswanywa.

Amesema pia katika madeni hayo kuna sh.bilioni 6 ambazo haziwezi kulipika kutokana na wadaiwa kufariki ama kampuni ilizokuwa zikidaiwa kufilisika.

Mkuu wa Kitengo cha Habari na Uhusiano NHC,Muungano Saguya (katikati) akizungumza na waandishi wa habari kuhusiana na kampeni ya miezi miwili kwa wadaiwa sugu na kulia ni Elias Msese Kaimu Mkurugenzi Usimamizi Miliki (NHC) na kushoto ni Meneja wa Kukusanya madeni (NHC) Levinico Mbilinyi.Mpigapicha Wetu

“Kutokana na kampeni hiyo ambayo itadumu kwa miezi miwili kuanzia Novemva Mosi hadi Desemba 30 tunawaomba wenye madeni kulipa haraka kabla ya sheria hijachukua mkonodo wake.

“Pia tunawatahadhirisha wale wote ambao walikuwa wapangaji wa NHC na wamehama kinyema tutahakikisha kuwa tunawakamata kwa kushirikiana na vyombo maalumu kutoka serikalini na pia orodha ya majina sugu ya wadaiwa itawekwa hadharani,” amesema.

Hata hivyo ameongeza kuwa wapangaji waliopo kwenye nyumba (Active tenants) ambao hawatalipa madeni yao kwa kipindi hicho, Shirika linakusudia kuvunja mikataba yao na kuwaondoa kwenye nyumba ikiwa ni pamoja na kuchukua mali zao kwa ajili ya kufidia madeni yao.

“Kwa waliokuwa wapangaji ambao wamehama na kuacha madeni (Ex-tenants) wanayodaiwa, wanatakiwa kufika katika ofisi za Shirika zilizo karibu nao na kupewa utaratibu wa malipo ikiwemo (Control number) ili walipe kwani NHC itarajia kuchapisha majina ya wadaiwa sugu kwenye vyombo vya habari,” amesema Bw. Saguya

Alisema kuwa kitendo cha wapangaji kukimbia na madeni ya nyumba ni sawa na kuhujumu uchumi hivyo NHC haitawavumiliwa na kwamba Shirika linaenda kuwasaka popote walipo kwa kutumia mbinu mbalimbali.

Levinico Mbilinyi Meneja wa Kukusanya madeni (NHC) (kushoto)akisisitiza jambo kwa waandishi wa habari kuhusiana na madeni sugu kutoka kwa wapangaji na katikatikani Mkuu wa Kitengo cha Habari na Uhusiano NHC,Muungano Saguya na Elias Msese Kaimu Mkurugenzi Usimamizi Miliki NHC.

Ameongeza kuwa NHC inawashukuru wapangaji wote wanaotimiza wajibu wao wa kulipa kodi ya nyumba kwa wakati kama mikataba ya upangaji inavyoelekeza aidha, ametoa shukurani kwa wapangaji walioitikia wito wa shirika hilo kwa kulipa madeni yao.

Meneja ukusanyaji madeni kutoka NHC,Levinico Mbilinyi amesema kuwa NHC inapokea maombi mengi ya wapangaji ambapo kwa kumekuwapo na maombi mapya kiasi cha 200 kila mwezi sawa na maombi 2,400 kwa mwaka.

“Maombi haya ambayo hata hivyo hayawezi kutimizwa na shirika kutokana na nyumba kuwa chache, yanaonyesha Watanzania wengi wanazihitaji nyumba hizi za Shirika. Kwa hiyo uhalali wa wapangaji kuendelea kuwa katika nyumba za Shirika la Nyumba utakuwepo tu kwa kutimiza wajibu wao wa kulipa kodi kwa wakati.

Kampeni hii ya miezi miwili itaongozwa na Kauli mbiu ya “LIPA KODI YA NYUMBA KWA MAENDELEO YA TAIFA LETU’’.