Na Mwandishi Wetu,JamhuriMedia,Dodoma

Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), umekabidhi kwa Tume ya Utumishi ya Walimu jumla ya majina 78 ya walimu waliobainika kughushi nyaraka mbalimbali za wategemezi wao pamoja na matumizi mabaya ya kadi za matibabu.

Walimu hao wamehusika kwa nyakati mbalimbali kughushi nyaraka za vyeti vya kuzaliwa, vyeti vya ndoa kwa lengo la kutaka kuthibitisha uhusiano wao na wahusika hao ili waweze kusajiliwa na Mfuko.

Makabidhiano hayo ya majina yamefanyika leo Machi 1, 2023 Makao Makuu ya NHIF jijini Dodoma wakati wa kikao kati ya Menejimenti ya Mfuko na ya Tume ya Utumishi wa Walimu. Katika kikao hicho ilitolewa ripoti inayoonesha namna Walimu hao walivyohusika katika vitendo vya udanganyifu pamoja na hasara waliyoisababisha kwa Mfuko.

Akizungumza katika kikao hicho, Mkurugenzi wa NHIF, Bw. Bernard Konga alisema Mfuko umeshachukua hatua mbalimbali kwa watuhumiwa hao ambao walikiri kutenda makosa hayo. ikiwemo kuwafungulia kesi, kuwafungia matumizi ya kadi na kuwataka kurejesha fedha ambazo zilitumika kuhudumia wategemezi wasio halali.

“Tunachukua hatua nyingi kwa watuhumiwa wa udanganyifu na mpaka sasa kuna kesi zinaendelea katika Mikoa ya Geita, Dodoma na Dar es Salaam, kadi za matibabu za watuhumiwa hao zimefungiwa pamoja na kuwaandikia barua za onyo hivyo tunaomba tushirikiane katika hili ili kukomesha vitendo hivi ambavyo vina madhara makubwa kwa Mfuko,” amesema Bw. Konga.

Naye Katibu wa Tume ya Utumishi wa Walimu, Mwalimu Paulina Nkwama alisema kuwa vitendo vilivyofanywa na Walimu hao haviwezi kukubalika kwa kuwa ni ukiukwaji wa maadili ya utumishi wa umma hivyo kupitia mamlaka ya tume hiyo hatua zitachukuliwa.

Aidha alikubali tume hiyo kushirikiana na mfuko kwa karibu katika kupambana na wimbi hilo la udanganyifu unaofanywa na walimu pamoja na kuelimisha madhara ya kughushi au kufanya udanganyifu wowote kupitia kadi ya matibabu.

Awali akiwasilisha taarifa ya uchunguzi wa udanganyifu uliofanywa na Watumishi wa Umma, Meneja wa Kitengo cha Kupambana na Udanganyifu cha NHIF Dkt. Rose Ntundu alisema kuwa kati ya Watumishi wa Umma 99 waliobainika kufanya udanganyifu, 78 ni Walimu wa Shule za Serikali za Msingi na Sekondari.

“Udanganyifu ambao wamekuwa wakiufanya ni pamoja na kughushi nyaraka kwa lengo la kutaka kuthibisha kuwa ni wategemezi wao lakini pia kutumia vibaya kadi zao kwa kuchukua dawa katika hospitali mbalimbali kwa kutumia kadi zao na kula njama na baadhi ya vituo vya matibabu kwa kusaini fomu za matibabu na wao kupewa fedha kidogo na vituo hivyo kuwasilisha madai kubwa kwa Mfuko,” amesema Ntandu.

Mfuko umejipanga kupambana na udanganyifu kwa kushirikiana na vyombo vya sheria, kuimarisha mifumo kwa kutumia TEHAMA yake kwa lengo la kudhibiti udanganyifu na hivi karibuni Mfuko utaanza matumizi ya mfumo wa kuwatambua wanachama wake kupitia sura zao au alama za vidole wanapokwenda kupata huduma.

By Jamhuri