*Asilimia 90 ya Bajeti ya Wizara zapelekwa kwenye maendeleo

*Wamarekani wamwaga mabilioni mengine kwenye MCC

*Mtwara, Lindi wapendelewa, kuunganisha umeme Sh 99,000

*Wizara yasisitiza ujenzi bomba kutoka Mtwara upo palepale

 

Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, amesoma Bajeti ya wizara hiyo ya mwaka wa fedha wa 2013/2014 na kusema asilimia 90 ya fedha zinazoombwa ni kwa ajili ya maendeleo; na hivyo kuifanya kuwa ni maalumu kwa ajili ya kuiingiza Tanzania katika karne ya 22.

Ameomba Bunge liidhinishe Sh 992,212,745,000 sawa na asilimia 90 ya Bajeti yote ya Wizara kwa ajili ya kutekeleza Miradi ya Maendeleo. Kati ya fedha hizo, Sh 558,345,745,000 sawa na asilimia 56 ni fedha za ndani.

 

Matumizi ya kawaida ameomba Sh 110,216,384,000 ambazo ni sawa na asilimia 10 ya Bajeti yote kwa ajili ya matumizi ya kawaida ambako kati ya fedha hizo, Sh 14,607,640,000 ni kwa ajili ya mishahara ya watumishi wa Wizara na taasisi zake. Sh 95,608,744,000 ni kwa ajili ya matumizi mengineyo (OC) ya Wizara na taasisi zake.

 

Ametamba kwamba hii ni mara ya kwanza kwa Wizara kuomba asilimia 90 ya fedha zinazotengwa katika bajeti, kutumika kwenye shughuli za maendeleo. Mradi wa Bomba la Kusafirisha Gesi Asilia kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam. Waziri Muhongo amesema utekelezaji mradi wa bomba la kusafirisha gesi kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam , upo pale pale.

 

Mradi wa ujenzi wa bomba la hilo ulizinduliwa Novemba 8, 2012 na Rais Jakaya Mrisho Kikwete. Unahusisha ujenzi wa bomba lenye urefu wa kilomita 532 na kipenyo cha inchi 36. Pia, bomba hilo lina uwezo wa kusafirisha futi za ujazo za gesi asilia milioni 784 kwa siku.

Mradi huo pia utahusisha mitambo miwili ya kusafisha gesi asilia katika maeneo ya Mnazi Bay -Madimba (Mtwara) na Kisiwa cha Songo Songo (Lindi). Utagharimu dola milioni 1,225.3 (Sh bilioni 1,960).

 

Amesema kazi za usanifu wa mradi na ulipaji fidia kwa wananchi 3,092 waliopisha maeneo ya mradi zimekamilika. Aidha, hatua za awali za ujenzi wa mitambo ya kusafisha gesi asilia zimeanza. Hadi sasa visima viwili vya maji vyenye uwezo wa kuzalisha mita za ujazo 50 kwa saa kwa kila kimoja vimekamilika.

 

“Visima hivyo ni kwa ajili ya mitambo ya kusafisha gesi asilia katika eneo la Madimba na kwa matumizi ya wananchi. Vifaa mbalimbali vya ujenzi wa nyumba za wafanyakazi wa mradi vimewasili nchini mwishoni mwa Aprili, mwaka huu. Ujenzi wa miundombinu hii utaleta manufaa makubwa kwa Taifa. Hadi sasa Mikoa ya Lindi na Mtwara imepata manufaa mbalimbali yatokanayo na miradi ya gesi asilia ikiwa ni pamoja na tozo ya asilimia 0.3 ya mauzo ya gesi asilia, huduma za jamii kama zahanati, shule, umeme, maji na ufadhili wa mafunzo katika Vyuo vya Ufundi (VETA) na sekondari.

 

“Manufaa mengine yatakayopatikana ni pamoja na ujenzi wa viwanda mbalimbali vikiwamo Kiwanda cha Saruji cha Kampuni ya Dangote ambacho ujenzi wake umeanza, kiwanda cha mbolea, mtambo wa kufua umeme wa MW 400 kupitia Kampuni ya Symbion pamoja na ujenzi wa njia ya usafirishaji umeme ya msongo wa kV 220 kutoka Mtwara hadi Songea.

 

“Aidha, Kampuni ya Schlumberger ya Houston, Marekani imejenga karakana kubwa Mtwara ambayo itakuwa inatengeneza vifaa vya uchimbaji, utafutaji na uendelezaji wa rasilimali za mafuta na gesi badala ya kupeleka nje ya nchi.

“Taratibu za kupata umiliki wa maeneo ya ujenzi wa viwanda (Industrial Park) vyenye kutumia gesi asilia zinaendelea katika mikoa ya Lindi na Mtwara. Ujenzi wa viwanda hivyo utaongeza fursa za ajira kwa Watanzania pamoja na mapato kwa Serikali,” Profesa Muhongo aliliambia Bunge.

Marekani kumwaga fedha nyingine za MCC

 

Profesa Muhongo aliliambia Bunge kwamba, kwa mara nyingine, Serikali ya Marekani imeichagua Tanzania kuendelea kupata ufadhili wa miradi ya maendeleo kupitia Millenium Challenge Corporation (MCC).

 

“Mheshimiwa Spika, baada ya nchi yetu kukamilisha Awamu ya Kwanza ya miradi ya MCC kwa ufanisi mkubwa, naomba kulitaarifu Bunge lako Tukufu kuwa Tanzania imechaguliwa tena kuendelea kupata ufadhili kutoka MCC katika Awamu ya Pili ambayo itaanza Mwaka 2013/2014. Kwa sasa, MCC inaendelea na uchambuzi wa kina wa miradi itakayofadhiliwa ili kujua kiasi halisi cha fedha kitakachotolewa.

 

“Maeneo ya kipaumbele katika awamu hiyo ni pamoja na upelekaji wa nishati jadidifu katika shule, zahanati, na vituo vya afya vijijini; ujenzi wa Kituo cha Malagarasi chenye uwezo wa kufua umeme wa MW42; na ujenzi wa njia ya umeme ya msongo wa kV 132 kati ya Morogoro na Mtibwa,” alisema.

 

Awamu ya Pili ya REA kunufaisha Wilaya 13

 

Waziri huyo alisema tathmini ya zabuni za kuwapata makandarasi wa kutekeleza Awamu ya Pili ya Mpango Kabambe wa Usambazaji Umeme Vijijini (REA) itakamilika mwishoni mwa mwezi huu.

Alisema Gharama za utekelezaji wa mradi wa Awamu ya Pili ya Mpango huo zinakadiriwa kuwa Sh bilioni 881 ambazo ni sawa na dola milioni 550 za Marekani.

 

“Serikali ya Norway kupitia Shirika lake la Maendeleo (NORAD) itachangia Krona za Norway milioni 700, sawa na takriban Sh bilioni 192 katika Mfuko wa Nishati Vijijini. Chini ya mpango huo, umeme utapelekwa katika makao makuu ya wilaya 13 ambazo hazina umeme kwa sasa na baadhi ya maeneo ya vijijini.

 

“Wilaya hizo ni Buhigwe, Busega, Chemba, Itilima, Kakonko, Kalambo, Kyerwa, Mkalama, Mlele, Momba, Nanyumbu, Nyasa na Uvinza. Gharama za upelekaji wa umeme katika Wilaya hizo zinakadiriwa kugharimu Sh bilioni 70 na kiasi cha fedha kilichobaki cha Sh bilioni 122 kitatumika kupeleka umeme vijijini,” alisema.

 

Katika hatua nyingine, alisema Serikali kupitia REA imeendelea kupeleka umeme katika Makao Makuu ya Wilaya na maeneo ya vijijini. Katika kipindi cha Mwaka 2012/2013, upelekaji umeme Makao Makuu ya Wilaya za Namtumbo na Nkasi ulikamilika. Mradi wa Namtumbo uligharimu Sh bilioni 3.87 na mradi wa Nkasi uligharimu Sh bilioni 5.58. Serikali kupitia REA imeendelea kuwezesha utekelezaji wa Mradi Kabambe wa Awamu ya Kwanza wa Kusambaza Umeme Vijijini katika mikoa 16 ya Tanzania Bara.

 

“Gharama za mradi huo ni Sh bilioni 129. Kati ya fedha hizo, takriban Sh bilioni 30 ni mchango kutoka Serikali ya Sweden . Mradi huo unatarajiwa kukamilika Mwaka 2013/2014 badala ya Desemba, 2012 kutokana na kuongezwa kwa maeneo mengine kwenye awamu ya kwanza ya mradi,” alisema.

 

Mtwara, Lindi kuendelea kufaidi punguzo la umeme

Waziri Muhongo alilitaarifu Bunge kwamba punguzo la wananchi kuunganishwa umeme ambalo lilikuwa liishe Juni, mwaka huu, limesogezwa mbele.

 

“Kwa kuzingatia usikivu wa Serikali ya CCM na baada ya kupokea maombi kutoka kwa viongozi wa mikoa ya Lindi na Mtwara, Serikali imekubali punguzo hilo liendelee hadi Juni 30, 2014. Tunawaomba wananchi wa Mtwara na Lindi wajitahidi kutumia fursa hii kuhakikisha wanaunganishiwa umeme kwa bei hii nafuu,” alisema.

 

Alisema mwaka 2012/2013 mradi wa kusambaza umeme katika mikoa hiyo ulitekelezwa katika maeneo ya Wilaya za Kilwa, Lindi, Masasi, Mtwara Mjini, Nachingwea, Newala, Ruangwa na Tandahimba. Mradi huo unafadhiliwa na Mfuko wa Nishati Vijijini (REA) kwa gharama ya Sh bilioni 5. Utekelezaji wa mradi upo katika hatua mbalimbali ambako katika Mkoa wa Mtwara kilomita 24.78 kati ya 47.53 za njia za usambazaji umeme zimejengwa na transfoma saba kati ya 24 zimefungwa. Wateja 277 wameunganishiwa umeme.

 

“Katika Mkoa wa Lindi, kilomita 11.28 kati ya 28.2 za njia ya umeme ya msongo wa kV 33 na kV 11 zimejengwa. Aidha, ujenzi wa kilomita 59.5 kati ya 72.3 za njia ya umeme ya msongo wa kV 0.4 umekamilika na transfoma 5 kati ya 25 zimefungwa. Wateja 132 wameunganishiwa umeme.

 

“Aidha, wateja katika Mikoa ya Lindi na Mtwara wataendelea kunufaika kuunganishiwa umeme wa njia moja (single phase) kwa gharama ya Sh 99,000 tu ikilinganishwa na kiasi cha Sh 177,000 wanazotozwa wateja kwenye maeneo mengine ya vijijini nchini kupata huduma hiyo,” alisema.

 

Mipango ya kupunguza gharama za kuunganisha umeme

 

Profesa Muhongo amesema wananchi wameonyesha mwitikio mkubwa wa kuunganishiwa umeme baada ya Wizara ya Nishati na Madini kupunguza gharama za shughuli hiyo.

 

“Katika hotuba yangu ya Mwaka 2012/2013, Serikali iliahidi kupunguza gharama za kuunganisha umeme katika maeneo ya vijijini na mijini ili kuweza kufikisha huduma hiyo kwa wananchi wengi zaidi. Napenda kulitaarifu Bunge lako Tukufu kuwa, ahadi hiyo imetekelezwa kuanzia Januari, 2013. Lengo la Serikali ni kuhakikisha kuwa asilimia 30 ya Watanzania wanaunganishiwa umeme ifikapo mwishoni mwa Mwaka 2014/2015,” alisema.

 

Alisema kutokana na punguzo hilo la gharama za kuunganisha umeme, maombi yameongezeka na kufikia wastani wa maombi 15,673 kwa mwezi ikilinganishwa na maombi 11,718 kwa kipindi hicho kabla ya punguzo. Ongezeko hilo ni sawa na asilimia 33.8.

 

“Kutokana na ongezeko hilo , changamoto kubwa imekuwa ni upatikanaji wa vifaa kama nguzo na mita kwa wakati ili kukidhi mahitaji. Kati ya Januari, 2013 hadi Machi 2013, wateja 35,405 wameunganishiwa umeme. Ili kuhakikisha wateja wanaunganishiwa umeme kwa wakati, vifaa muhimu vya kuunganishia wateja umeme vilivyoagizwa na TANESCO kuanzia Januari, 2013 ni kama ifuatavyo: nyaya zenye urefu wa kilomita 22,880, nguzo 133,800, mita 265,000 na transfoma 2,100.

 

“Kumekuwa na malalamiko kutoka kwa baadhi ya wananchi kuhusu uagizaji wa nguzo za umeme kutoka nje ya nchi, hususan Afrika Kusini , Uganda na Zambia . Hata hivyo, ukweli ni kwamba bei ya nguzo zinazozalishwa na kampuni za Tanzania ni ghali ikilinganishwa na bei ya nguzo kutoka nchi nyingine.

 

“Mfano, bei ya nguzo hapa nchini pamoja na usafiri ni kati ya Sh 224,000 hadi Sh 749,000 wakati nguzo za Afrika Kusini ni kati ya dola 138 hadi 420 za Marekani, sawa na kati ya Sh 219,000 hadi Sh 672,000.

 

“Baadhi ya wasambazaji wa nguzo wa ndani wamekuwa wakifanya kazi kwa mazoea (business as usual). Niwasihi sana wabadilike ili wanapopata kazi, waheshimu mikataba,” alisema.

Alisema katika mwaka 2012/2013, Serikali imekamilisha utayarishaji wa nyaraka za zabuni kwa ajili ya ununuzi wa vifaa na ujenzi wa miundombinu ya umeme katika wilaya za Kilombero (Morogoro) na Mbozi (Mbeya).

 

“Kazi hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa Mradi wa Mfano wa Usambazaji Umeme kwa Gharama Nafuu (Low Cost Design Standards). Gharama za mradi huo unaofadhiliwa na Benki ya Dunia kupitia ‘Sida Trust Fund’ zinakadiriwa kuwa Sh bilioni 16, ambapo takriban wateja 20,000 wataunganishiwa umeme. Utekelezaji wa mradi huu unatarajiwa kupunguza gharama za usambazaji umeme katika maeneo hayo,” alisema.

 

Futi za ujazo za gesi nchini sasa ni trilioni 41.7

Profesa Muhongo alisema katika Mwaka 2012/2013, kampuni za utafutaji mafuta ziliendelea kutekeleza mipango kazi kama ilivyoainishwa kwenye mikataba yao .

 

“Katika kipindi hicho, Kampuni za BG/Ophir na Statoil/ExxonMobil zilifanikiwa kuchoronga visima vinne (Zafarani – 2, Lavani – 2, Tangawizi na Jodari North) kwenye kina kirefu cha maji baharini ili kutathmini kiasi cha gesi asilia kilichopo.

 

“Kisima cha Tangawizi kimegundulika kuwa na kiasi cha futi za ujazo kati ya trilioni 4 hadi 6 wakati kisima cha Jodari kimegundulika kuwa na futi za ujazo trilioni 4.1 badala ya futi za ujazo trilioni 3.4 zilizotangazwa awali.

 

“Aidha, kisima cha Zafarani – 2 kimegundulika kuwa na futi za ujazo trilioni 6, wakati Kisima cha Lavarani – 2 kimegundulika kuwa na futi za ujazo trilioni 4.7. Hadi sasa kiasi cha gesi asilia kilichogundulika nchini ni takriban futi za ujazo trilioni 41.7,” alisema.

Please follow and like us:
Pin Share