Maisha ni urafiki. Mwanafalsafa mwenye asili ya Kiafrika Martin Luther Jr. King alipata kusema hivi, “Ukimya wa marafiki zetu unaumiza kuliko kelele za madui zetu”.  Rafiki wa kweli ni rafiki siku zote. Mwenyezi Mungu ni rafikiwa kweli katika maisha yetu ya kila siku. Anatulinda. Anatupenda. Anatubariki.
Anatuongoza katika njia iliyo takatifu. Tukumbuke jambo moja ambalo ni la mhimu sana: Hatuwezi kufanikiwa kiroho, kimwili, kiuchumi, kimaadili, kifamilia, kama hatumtazami Mwenyezi Mungu kama rafiki yetu mwema na muumba wetu.
 
Yesu Kristo aliwahakikishia wanafunzi wake upendo wake kwao kwa kuwaita rafiki. Tunasoma hivi katika maandiko matakatifu, “Siwaiti tena watumwa, kwa sababu mtumwa hajui kazi za Bwana wake. Badala yake ninawaita rafiki, kwa kuwa nilichojifunza kwa Baba yangu nimewajulisha (Yoh 15:15).”
Huu ni urafiki usioweza kuelezeka kwa maneno bali kwa upendo tu. Yesu Kristo ni rafiki yetu. Ni kaka yetu. Ni mkombozi wetu.
Usithubutu kumuacha Mungu kwa ajili ya chochote, bali acha chochote kwa akjili ya Mungu, kwa sababu katika maisha chochote chaweza kukuacha wakati wowote. Lakini Mungu atakuwa nawe siku zote za maisha yako.
Siri kubwa ambayo unatakiwa kuifahamu ni kwamba; Mwenyezi Mungu ni rafiki yako mwema hata pale unapokabiliwa na nyakati ngumu katika maisha.
 
Kuna mtu ambaye aliota ndoto. Ndoto yake ilimuonesha kwamba alikuwa anatembea kando ya bahari yenye michanga. Alipokuwa na furaha alitazama nyuma na kuona nyayo za watu wawili. Alipokuwa na shida alitazama nyuma na kuona nyayo za mtu mmoja. Ndoto hii ilimtatiza.
Akiwa bado kwenye ndoto yake alimuuliza Mungu maana ya ndoto yake. Mungu alimjibu kwa kumwambia: “Unapokuwa na furaha tunakuwa pamoja”. Mtu huyo alidadisi tena na kuuliza: “Mbona wakati wa shida naona nyayo zangu peke yangu?” Mungu alimjibu kwa kumwambia: “Wakati wa shida nakubeba mgongoni ndiyo sababu unaona nyayo za mtu mmoja.”
 
Urafiki ni uhusiano wa nafsi mbili wa kimapendo au wa matashi mema. Kwa tafsiri hiyo, nafsi hizo zinaweza kuwa za jinsia moja au tofauti. Urafiki ni uhusiano mwema baina ya mtu na mtu, nchi na nchi au jamii na jamii. Mwenyezi Mungu ametuumba ili tuwe marafiki.
Tunasoma hivi katika maandiko matakatifu, “Tazama jinsi ilivyo vema na kupendeza ndugu kukaa pamoja kwa umoja. Ni kama mafuta mazuri kichwani, yanayoshuka ndevuni, ndevu za Haruni. Ni kama umande wa Hermon, unaoshuka mlimani pa Sioni. Maana ndiko BWANA alipotawaza Baraka naam, uzima hata milele (Zaburi133:1-3).”
 
Kwa nini Mwenyezi Mungu anapenda tuishi maisha ya urafiki? Sababu kuu ni hii. Mwanadamu ni kiumbe pekee aliyeumbwa kama Mungu. Mwanadamu ameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Kuumbwa kwa sura na mfano wa Mungu ni hadhi kubwa sana.
Hadhi hii haina ufananisho na kitu chochote kile. Tunasoma hivi katika maandiko matakatifu, “Mungu akaumba mtu kwa mfano wake, kwa mfano wa Mungu alimuumba mwanamume na mwanamke aliwaumba (Mwanzo1:27).”
 
Chimbuko la urafiki wa Mungu na mwanadamu ni kwamba mwanadamu anashiriki sifa za Kimungu. Urafiki ni tunu katika maisha. Tunahitaji kuuanzisha, kuuboresha na kuuweka katika mazingira mazuri ya kustawi.
Urafiki wa kweli haupatikani kwa njia ya magendo au mrungura, wala kununuliwa kwa fedha, bali unajengwa. Bila urafiki, mbingu ingekuwa haina ladha na dunia ingegeuka na kuwa jehanamu.
 
Maisha ni urafiki. Kati ya zawadi nzuri ambazo tumepokea kutoka kwa Mwenyezi Mungu ni zawadi ya urafiki.  Mke wako ni rafiki yako. Mume wako ni rafiki yako. Mtoto wako ni rafiki yako. Mzazi wako ni rafiki yako. Kaka yako ni rafiki yako. Dada yako ni rafiki yako. Jirani yako ni rafiki yako.
Naomba kutoa ushauri huu. Nidhahiri na ni kweli kwamba ili uwe rafiki mwema na msikivu kwa wengine ni lazima kwanza uwe rafiki mwema kwa nafsi yako na familia yako. Kama umeoa au umeolewa fahamu kwamba rafiki yako wa kwanza ni mke/mme wako.
 
Ngoja niwafunulieni siri ya kuwa na furaha ya kudumu maishani. Anzisha utaratibu huu katika maisha yako. Kwa wanandoa asubuhi unapoamka kutoka kitandani muoneshe mke/mme wako tabasamu la upendo mwambie: “Nakupenda sana mme/mke wangu, bila urafiki wangu na wewe nisingefika hapa nilipo.” Kisha mbusu, busu takatifu.
Kisha munong’oneze kwa kumwambia, “Kazi njema mke/mme wangu”. Jioni baada ya mihangaiko ya kutafuta riziki unaporudi nyumbani sahau magumu uliyokutana nayo. Epuka kuzileta hasira za kazini nyumbani kwako. Unapofika nyumbani mwoneshe mke/mme wako tabasamu la upendo mwambie:
“Nakupenda sana mke/mme wangu”. Kisha mbusu, busu takatifu. Halafu mkaribishe mwenzako nyumbani kwa kumwambia, “Pole kwa kazi mke/mme wangu, karibu tena nyumbani.”
Kabla  watoto wako hawajalala usiku waite huku ukiwaonesha uso uliojaa tabasamu la upendo na kuwambia maneno haya: “Nawapenda sana wanangu”. Kisha wabariki wakalale.
Kwa Padre, Mtawa na Askofu asubuhi unapoamka kutoka kitandani inyanyue mikono yako juu na kumtazama Kristo kuhani wako mkuu, kisha mwambie: “Ninaomba kuwa Mchungaji mwema na rafiki mwema wa kondoo ninaowachunga.”
 
Sisi binadamu tuliumbwa ili tupendwe na tupende. Mwenyezi Mungu alituumba hivi ili tuwe na mawasiliano na urafiki, ndiyo maana binaadamu hawi mkamilifu kama hana mawasiliano ya karibu na wengine.
Mwanateolojia William Backlay alipata kufafanua kwamba, “Msingi mkubwa wa furaha ya mtu duniani inalala katika uhusiano na wengine”. Unapopata fursa ya kuishi tambua kwamba hiyo sio tu fursa ya kuishi bali ni fursa pia ya kujenga urafiki na muumba wako, pasipo kusahau jamii ya watu inayokuzunguka.
 
Tufafanue kidogo namna ya kumpata rafiki wa kweli. Jambo moja tunalotakiwa kuzingatia ni kwamba tunapoingia katika uhusiano wa kirafiki basi tujitahidi sana kuishi maisha ya ukweli na uwazi ili tusiharibu uhusiano wetu na Mungu wetu ambaye anajifunua kwetu kila siku kwa njia ya marafiki zetu. Mwandishi Kahlil Gibran anasema, “Unaweza kumsahau yule ambaye mnacheka pamoja, lakini huwezi kumsahau yule ambaye mmelia pamoja.”
 
Rafiki mwema ni yule ambaye anashiriki kwa ukaribu nyakati zote unazopitia katika maisha. Tunapoingia katika maisha ya urafiki tusitangulize maslahi fulani, badala yake tutangulize upendo kwanza kama nguzo kuu ya kuimarisha urafiki wetu. Urafiki wa kweli ni nadra kupatikana. Unaweza kuniuliza:
“Kwa nini urafiki wa kweli ni nadra kupatikana?”  Sababu kubwa ni hii: “Ni watu wachache sana duniani wenye hadhi ya kupenda na kupendwa bila masharti.” Sababu ni kwamba watu wengi wanatafuta urafiki wa kupokea kuliko kutoa.
 
Ukitaka kumpata rafiki wa kweli mpime kwanza ndipo umruhusu kuwa rafiki yako, usiharakishe kumuamini kwa sababu ya maneno yake matamu ama umaarufu alionao katika jamii au cheo chake au urembo wa sura aliyonayo. Kwa sababu kuna rafiki wa kudumu na kuna rafiki wa kukimbia wakati wa dhiki.
Tuepuke urafiki wa kinafiki. Tuwaepuke marafiki wanaotushawishi kutenda dhambi. Ikiwezekana punguza idadi ya marafiki ulionao, sio busara kuwa na marafiki wengi, lakini wanafiki. Inatosha kuwa na marafiki wachache lakini wenye upendo wa dhati.
 
Kuna umuhimu wa kufanya utafiti wa kina wa marafiki hao. Kwa sababu ukiwa tajiri kwa mfano, au mwenye kujiweza kimaisha, utapata marafiki wengi tu, lakini ukiwa maskini, mgonjwa, mwenye shidashida hauwezi kuwapata marafiki. Waswahili wana msemo unaosema kwamba, “Mkono mtupu haulabwi”. Sababu ya hayo yote ni kwamba binaadamu ana upendo wa kimaslahi.  Baadhi ya watu wanasita kuwaonesha masikini upendo badala yake wanawaonesha matajiri pekee upendo. Utamaduni huu si sahihi.
 
 Mwandishi E. Fromm anaeleza kwamba, “Kama nampenda mtu mmoja kwa dhati basi nawapenda watu wote, naupenda ulimwengu, nayapenda maisha. Kama naweza kumwambia mtu mwingine ‘nakupenda’ basi ni lazima niweze kusema, nahitaji kuwapenda watu wote bila kuwabagua.”
Tatizo kubwa na sugu ambalo linawakumba watu wengi ni kwamba wengi tunaanzisha urafiki pasipo kumshirikisha Mwenyezi Mungu. Ifahamike wazi kwamba ni katika Mungu tu ndipo watu wanaweza kujenga urafiki wa kweli na wa undani kabisa. Mungu akusaidie upate kuyaishi uliyoyasoma katika makala hii.

By Jamhuri