Miaka 44 Gerezani

Ni mfungwa wa aina yake nchini. Ameingia gerezani vyama tawala vikiwa ni Tanganyika African National Union (TANU) na Afro-Shiraz (ASP). Chama Cha Mapinduzi kimezaliwa mwaka 1977 akiwa gerezani.

Amewekwa gerezani wakati ambao Tanzania haikujua kama itapigana na Uganda kwenye vita iliyokuja kujulikana baadaye kama ‘Vita ya Kagera’ (mwaka 1978-1979). Wala hakuona vita ya uhujumu uchumi ilivyoendeshwa na hayati Edward Sokoine. Ameingia gerezani akimjua Waziri Mkuu wa Tanzania (siyo Tanganyika) mmoja tu, Rashid Kawawa; lakini ametoka gerezani tayari Tanzania ikiwa imeshapata mawaziri wakuu 10.

Rais John Magufuli alitoa msamaha kwa wafungwa kadhaa siku ya sherehe za miaka 56 ya Uhuru wa Tanzania Bara, Desemba 9. Chagizo la sherehe hizo zilizofanyika kwa mara ya kwanza katika Uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma, ni msamaha aliowapa wafungwa wakiwamo wale ambao hawakuwa na matumaini ya kupata bahati hiyo.

Aliwasamehe waliofungwa maisha, kwa maana nyingine Rais Magufuli aliamua kwa makusudi kuwaondolea wafungwa ‘adhabu’ ya kufia katika kuta za gereza na kuzikwa huko; ndugu zao wakiambulia taarifa za misiba ya wapendwa wao.

Msamaha huo umewagusa Watanzania kwa namna tofauti. Wapo walioguswa na kuachiwa huru kwa wana muziki wawili – Nguza Vicking (Babu Seya) na mwanae, Johnson Nguza (Papii Kocha). Wapo walioguswa na kuachiwa huru kwa Mzee Mganga Matonya (85), aliyefungwa kwa makosa ya unyang’anyi.

Nami naangukia katika kundi hilo la walioguswa na maisha ya Mzee Matonya, hasa kwa namna yalivyosimuliwa kidogo na Rais Magufuli. Kilichonigusa zaidi ni umri wake. Hakuwa uraini kwa miaka 44.

Nikiwa Makao Makuu ya nchi hapa Dodoma, naamua kuuliza habari za Mzee Matonya. Hapa anaonekana si mtu anafahamika sana, lakini nikalazimika kuelewa maana wengi niliowauliza, kiumri hawafikii hata miaka aliyoishi gerezani.

Shauku yangu inakuwa kubwa zaidi baada ya kuona gazeti moja la kila siku limeandika habari zake. Nikachukua gazeti hilo na kulisoma, kichwani mwangu nikiwa nimebeba falsafa ya Gazeti la JAMHURI ya “Tunaanzia wanapoishia wengine”.

Nikawa na azma ya kufika Kijiji cha Wiliko ambako ndiko nyumbani kwa Mzee Mganga Matonya.

“Kutoka hapa mjini mpaka Wiliko ni kilomita zaidi ya 87, barabara si nzuri sana kutoka Mlowa kwenda kijijini huko…subiri nipange ratiba yangu vema, nitakupeleka,” ananiambia mwandishi aliyejua nyumbani kwa mzee huyo.

Basi, Ijumaa safari yetu ilianza kwenda kijijini Wiliko nikiwa na shauku kubwa ya kufika na kujionea mwenyewe maisha halisi ya mmoja wa wanufaika wa msamaha wa Rais Magufuli, Mzee Mganga Matonya.

Nikiwa Kijiji cha Mlowa, ambacho ndiyo njiapanda ya kwenda Kijiji cha Wiliko, naanza kuona mibuyu mikubwa. Kichwani naanza kujiuliza maswali, kwamba mwaka 1974 wakati Mganga Matonya anafanya uhalifu na kukamatwa hali ilikuwaje? Wakati nikiendelea kuwaza hayo huku gari likichanja mbuga, mara tunafika Kijiji cha Bwawani.

Tunakoelekea kunazidi kuoneana ni mbali zaidi huku miti na vichaka vifupi vikiwa ndivyo vinavyoonekana. Mawazo yangu yakaenda mbali zaidi kwamba polisi waliwezaje kumbaini na kumkamata Mganga wakati huo. Baadaye nikakumbuka kwamba nchi yetu imeundwa vizuri kimfumo.

Punde, tunafika Kijiji cha Wiliko na kuelekea moja kwa moja nyumbani kwa Mzee Mganga Matonya. Tunafikia nyumbani kwa kijana wake mkubwa ambako ndiko alipokuwa amefikia baada ya kutoka jela.

Tukiwa pale tunawakuta akina mama kadhaa. Mmoja anasema, “Mzee hayupo hapa tena, tayari amehamia nyumbani kwake, si mbali sana kutoka hapa. Ni pale chini kidogo.”  Wakati tunaisogelea nyumba yake, basi Mzee Matonya naye akawa anatoka ndani akiwa ameshika kigoda. Anatabasamu na kutukaribisha nyumbani kwake.

Mwenyeji wangu ambaye alikuwa anafahamika vizuri na familia hiyo, anaanza kutoa salaam kwa lugha ya Kigogo.  Tunakaribishwa katika vigoda.  Tunakaa na kuanza mazungumzo huku familia nzima ikiwa imetuzunguka.

Ninaanza kwa kujitambulisha kwake. Naye anatabasamu na kusema, ‘Bora umekuja, natamani kupata msaada kutoka kwa Watanzania wenzangu, maana ni dhahiri sasa nimeanza maisha mapya tena katika uzee wangu.”

Matonya ambaye ametoka Gereza la Mtego wa Simba mkoani Morogoro na kurudi kijijini kwao Wiliko, Wilaya ya Chamwino, anasema hadi sasa anahisi kama anaota kwa kuwa hakuwahi kuwaza kutoka gerezani.

Kijiji cha Wiliko kipo umbali wa kilomita 87 kutoka katikati ya Mji wa Dodoma katika barabara ya kwenda Iringa. Kijiji hicho kipo mpakani mwa wilaya hiyo na Jimbo la Isimani lililopo mkoani Iringa.

Mchakato wa kutoka gerezani

Mzee Mganga Matonya ameliambia Gazeti la JAMHURI, kwamba katika kipindi cha miaka zaidi ya 30 amekuwa akiandika barua za kuomba msamaha kwa marais watatu waliopita.

Anasema katika maisha yake ya gerezani aliishi kwa hofu kubwa hasa katika kipindi cha Rais Ali Hassan Mwinyi. Anakumbuka namna unyongaji ulivyokuwa ukitekelezwa kwa vitendo. Anamkumbuka Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere kwa kumwondolea adhabu ya kunyongwa, badala yake akapewa adhabu ya kifungo cha maisha.

“Nakumbuka wakati huo nikiwa gerezani walinyongwa wenzangu wanne- mmoja akiwa ni Saidi Mwamwindi, aliyetiwa hatiani kwa kumuua aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dk. Wilbert Kreluu. Hapo nilikuwa bado niko mahabusu, kesi yangu ikiwa haijanza kusikilizwa.

“Baada ya kesi yangu kusikilizwa katika Mahakama Kuu, Kanda ya Dodoma, hatimaye nikahukumiwa kunyongwa hadi kufa na Jaji Dan Petro Mapigano. Sikuisumbua Mahakama maana nilikamatwa na vidhibiti vyote. Kwa kweli kufungwa maisha sikuwa nimeonewa hata kidogo,” anasema.

Mzee Mganga Matonya, ameliambia JAMHURI; “Niliua baada ya kuona mwenye wale ng’ombe anatuletea ugumu katika kutimiza azma yetu. Mwenzetu mmoja alipigana naye kwa fimbo na jamaa akaonekana alikuwa mahiri sana. Hivyo sisi sote wanne tukamvamia tukamuua na tukachukua ng’ombe 12.

“Wakati nikiwa kijana nilikuwa na tabia ya wizi wa mifugo, hasa ng’ombe. Nakumbuka tuliiba ng’ombe maeneo mengi. Lakini siku ya tukio lililosababisha nifungwe, nilikuwa mimi na rafiki yangu Muyeya Nyagalu (naye ametoka kwa msamaha wa Rais) na Wamaasai wawili. Tulikuta ng’ombe wale wazuri sana, tukapiga hesabu zetu zikakubali.

“Baada ya mapambano makali na huyo mwenye ng’ombe katika Kijiji cha Mlowa Bwawani, tulifanikiwa kumuua maana pale kama tungezembea, basi mmoja wetu angekufa. Tulipomuua tuliondoka na ng’ombe na utaratibu wa kugawana ukafanyika na hatimaye kila mtu akaondoka na fungu lake.

“Tulipogawana wale ng’ombe walionona mimi nilishika njia na kuelekea mnadani, nadhani hapo ndipo nilipojichanganya maana nikiwa pale mnadani nasubiri wateja, walikuja askari na kunikuta nikiwa na ng’ombe sita.

“Nilibahatika kuwachomoka askari na kuwakimbia nikarudi nyumbani kwangu, lakini serikali ina mkono mrefu – siku tatu baadaye nilikamatwa na kundi la watu waliozingira nyumba yangu na wakati huo nilikuwa juu ya nyumba yangu ya tembe nikiendelea kuezeka udongo kwa kuwa msimu wa mvua ulikuwa umekaribia.”

 

Matonya ni nani?

Mganga Matonya ni baba wa watoto sita, wajukuu 34 na vitukuu tisa ambao wanaishi kijijini hapo.

Ni miongoni mwa wafungwa 8,157 waliopata msamaha wa Rais Magufuli, lakini akiwa mfungwa mzee kuliko wote huku akidumu gerezani kwa miaka 44 ambayo aliishi katika magereza ya Isanga (Dodoma) na Mtego wa Simba (Morogoro). Asili yake ni Mvumi kabla ya kuhamia Kijiji cha Wiliko wilayani Chamwino.

Hadi anapelekwa gerezani alikuwa na watoto wawili, na akamwacha mkewe akiwa mjamzito. Bada ya kutokana gerezani amekuta familia imeongezeka- akiwa na wajukuu na vitukuu.

“Ni lazima katika familia yangu tupate mtoto atakayeitwa Magufuli, maana amenitendea mambo makubwa sana huyo mtani wangu. Haitakuwa ajabu ‘sisi wagogo’ kwenye ukoo wangu tukipata mtoto atakayekuwa na jina hilo, bila shaka atakuwa na huruma kama aliyonayo mtani wangu,” amesema Matonya.

Maisha ya gerezani

Tangu Oktoba 1974, Matonya alikuwa katika mahabusu ya Gereza la Isanga. Miaka sita baadaye alihukumiwa kunyongwa hadi kufa.

Anasema ushahidi usio na shaka uliwatia hatiani yeye na rafiki yake Nyagalu ambaye hata baada ya kupata msamaha alikwenda naye mpaka Kijiji cha Wiliko kabla ya kuchukuliwa na ndugu zake kutoka Mpunguzi.

Anasema amekuwa mfungwa kwa miaka 44 kwa kosa ambalo anakiri kulifanya na anajutia.

“Kutokana na hukumu ya Jaji Mapigano, nilijua nitanyongwa muda si mrefu na hivyo nilianza kukata tamaa ya maisha na sikuwa nawaza chochote zaidi ya kuagiza mke wangu aje aniage.

“Gerezani nilikuwa nafanya kazi za nguvu, kwa kweli mimi nimefanya kazi nyingi sana gerezani nilizotumwa na ambazo sikutumwa, hiyo ndiyo sehemu ya kujiliwaza maana ukifanya kazi ngumu unachoka na ukilala basi unalala fofofo,” ameliambia JAMHURI.

Mzee Matonya anasema anaukumbuka mwaka 1983 alipopewa taarifa na mkuu wa gereza, ambaye hamkumbuki kwamba Rais wa wakati huo, Mwalimu Julius Nyerere alikuwa amemsamehe adhabu ya kunyongwa hadi kufa na badala yake atumikie adhabu ya kifungo cha maisha.

“Ndiyo maana nasema kama mtu akinipeleka kwenye kaburi la Nyerere ningeinama na kumshukuru sana mzee huyu, maana asingefuta adhabu ya kifo huenda huyu wa sasa (Magufuli) asingenikuta hai.

“Wakati nasubiri kunyongwa na siku zikiwa zinasogea, nilianza kujipa matumaini kwamba pengine nitaweza kuishi hata miaka mitano kabla ya hukumu yangu kutekelezwa, lakini sikuwahi kuwaza kurejea uraiani,” anasema.

Anasema baada ya kubadilishiwa adhabu yake, alikaa Gereza la Isanga mkoani Dodoma kwa mwaka mmoja na baadaye akapelekwa Gereza la Mtego wa Simba mkoani Morogoro ambako ameishi kwa miaka 33.

“Maisha ya mahabusu yalinifanya nimkumbuke Mungu wangu. Mwaka 1975 nilibatizwa katika madhehebu ya Kanisa la Anglikana. Hiyo ilikuwa sehemu ya faraja kaika maisha yangu mapya,” anasema.

Maisha ndani ya kuta nne za gereza

Mzee huyo mchangamfu na ambaye anajinasibu kwamba bado ana nguvu za kufanya mambo yake ya maendeleo, ameliambia JAMHURI kwamba katika kipindi chote cha miaka 44 jela, hatayasahau matukio mawili makubwa.

Moja likiwa limemtokea kati ya mwaka 1976-1977, anasema aliugua na hata kudhani kwamba adhabu ya kifo inakwenda kutekelezwa kabla ya siku ya hukumu yake.

“Nilivimba miguu yangu yote miwili kuanzia kwenye unyayo mpaka mapajani, nimehangaika nayo kwa miaka miwili. Ilifikia hatua mpaka nikakitamani kifo kutokana na maumivu niliyokuwa nayapata.

“Tukio jingine lilinitokea 1997 baada ya mtoto wangu wa mwisho ambaye wakati nafungwa nilimwacha mama yake ana mimba ya miezi minane, alikuja Gereza la Mtego wa Simba kuniona. Sikuwa namfahamu isipokuwa baada ya kumwona nilijua ni ndugu yangu.

“Akajitambulisha kwangu, nililia sana siku hiyo. Nakumbuka nilimtemea mate kichwani, maana kutokana na hali halisi nilishaanza kuona kama sina ndugu kabisa ambao wangeweza kusimama pamoja nami. Baada ya yeye kuja ndipo hata ndugu zangu wengine walianza kuwaleta.

“Nikapata matumaini mapya kabisa…maana alianza mpaka kuniletea wajukuu zangu huko huko jela, pamoja na jitihada hizo nilikuwa na kinyongo moyoni kwamba kuna siku nitakufa na nitazikwa jela maana hiyo ndiyo ilikuwa hukumu yangu,” anasema Matonya.

Kitu gani anatamani maishani?

Kwa sasa Mganga anatamani kupata nafasi ya kuwa mshauri wa vijana na watu wenye tabia za wizi na udokozi, akisema kuwa hazilipi hata kidogo zaidi ya kuwarudisha nyuma.

Kazi hiyo alikuwa akiifanya tangu alipokuwa gerezani na anasema baadhi ya watu aliokuwa akiwapa ushauri huko walikuwa wakirudi uraiani wanakuwa raia wema kiasi cha kumtembelea gerezani kwa ajili ya kumshukuru.

Ombi lake jingine ni kwa jamii pamoja na Serikali kumwonea huruma na kumwezesha walau kitu chochote cha kuanzia maisha na mkewe ambaye anasema kwamba alikuwa mvumilivu wakati wote licha ya kuzaa watoto watatu nje ya ndoa yao, lakini bado aliwaandika kuwa katika ukoo wake na alivumilia kuishi na familia yake hadi mwisho.

Anasema hawezi kurudia kosa la aina yoyote zaidi ya kuishi kwa kumtegemea Mungu na kujikita katika kilimo ili mvua zikinyesha apate chakula cha familia yake.

Alipataje taarifa ya kuachiwa?

Anasema siku ya sherehe za Uhuru akiwa na wenzake na kwa sababu ya umri wake alikuwa amelala kivulini, huku wafungwa wengine wakisikiliza na kuangalia televisheni.

Anaeleza kuwa, ghafla mfungwa mwenzake anayemtaja kwa jina moja la Mlyuka mwenyeji wa Njombe alimfuata na kumwambia kuwa majina yao yametajwa kwamba wamesamehewa.

“Nilimwuliza Mlyuka kama ni kweli akasema ni kweli tumetajwa,” anasema mzee Mganga na kuongeza kuwa baadaye wafungwa wenzake waliwapongeza kabla ya askari wa gereza kuwaita na kuwaambia wajiandae ili siku inayofuata waruhusiwe.

Mabadiliko aliyokutana nayo uraiani

Kutokana na kuishi gerezani muda mrefu, anasema hata kijiji chake anaona si kile alichokiacha, zaidi akikumbuka miti mikubwa michache aliyoiacha.

“Wakati narudi nyumbani nimeona mabadiliko makubwa sana, hata barabara zenyewe, watu wamejenga sana. Si kama kipindi cha miaka ya 1970 wakati naingia matatizoni.

Kwa mujibu wa mzee huyo hata jua anaona linatokea upande ambao halikuwa likitokea na wakati mwingine anahisi kuwa hayuko katika dunia ya sasa.

Mzee Matonya anafurahi kuwa anaongea na watu kwa uhuru mpana tofauti na wakati ambao alikuwa anaongea na nduguze akiwa gerezani kwa kuhesabiwa dakika.

Jambo jingine lisilomfurahisha ni namna ambavyo mazingira yameharibiwa zaidi kijijini kwao huku idadi ya watu ikiwa imeongezeka na nyumba ni nyingi.

Simulizi ya mkewe

Mke wa Mzee Mayonya, Nyendo ni mama wa watoto sita. Wawili hao walioana mwaka 1963 na kupata mtoto mmoja ambaye bahati mbaya alifariki dunia kabla ya kupata shida ya uzazi hadi alipopata ujauzito miaka sita baadaye.

Mama Nyendo anasema maisha yaligeuka haraka sana baada ya mumewe kuwekwa mahabusu akisubiri kesi iliyomkabili. Anakumbuka ilikifia kipindi alilazimika kwenda kuomba vibarua kukoboa mahindi na mtama.

Katika kila debe moja alilokoboa kwa mikono, yeye aliambulia ‘makimbo’ matano tu. Hivyo bidii yake ndiyo ilikuwa suluhu pekee ya kutafuta chakula cha watoto ambao walikuwa wadogo.

“Nilikuwa nakwenda kuomba vibarua vya kukoboa mahindi na mtama kwa kutwanga kwenye kinu…nimeifanya kazi hiyo sana hapa Wiliko maana sikuwa na namna nyingine ya kuwahudumia watoto.

“Wakati huo nilikuwa na watoto wawili tu, huku nikiwa mjamzito, kuna wakati nililazimika kuwakorogea uji ili walale. Maisha yakawa magumu sana. Sikuwaza kurudi nyumbani maana kwa mila za Kigogo nilitakiwa kuwaacha wanangu wote kwa ndugu wa mume. Sikutaka watoto wangu walelewe na mtu mwingine nikiwa hai.

“Ninaamini sasa baada ya mume wangu kurudi maisha sasa yatarudi katika hali ya kawaida, japokuwa sasa ni mzee…ametumikia kifungo chake jela. Nitahitaji kusaidiana naye katika kujenga familia yetu,” anasema Mama Nyendo.

Utamaduni wa wagogo

Baada ya Mzee Matonya kutoka gerezani alifikia kwa mwanaye mkubwa anayeishi jirani na ilipokuwa himaya ya baba yake. Mzee Matonya amekaa hapo kwa siku nne kabla ya kurejea kwake rasmi.

Uchunguzi wa Gazeti la JAMHURI umebaini kuwa kipindi hicho kilikuwa maalum kwa nyumba ya Mzee Matonya ‘kuwekwa sawa’, hasa ikizingatiwa hakuwapo kwa miaka 44. Baada ya taratibu hizo za kimila kukamilika ndipo Mzee Matonya aliporuhusiwa kuingia katika himaya yake Alhamis, Desemba 14.

Kuomba radhi

Mzee Matonya anasema Alhamis iliyopita alifanya ibada maalum ya kumshukuru Mungu na kumwombea Rais John Magufuli. Ibada hiyo ilihudhuriwa na ndugu zake kutoka maeneo mbalimbali. Iliendeshwa katika Kanisa la Anglikana kijijini hapo.

Akijibu swali kuhusu yeye kufanya ibada ya kumshukuru Mungu bila kwenda kuiomba radhi familia ya mtu aliyeshiriki kumuua, anasema tangu alivyofika kijijini hapo amekuwa anauliza kama ndugu zake wapo. Amesema yuko tayari kukutana nao na kuwaomba radhi.

“Niko tayari kuomba radhi hata kama ni kwa wajukuu zake…hapo nitakuwa na amani katika nafsi yangu. Lakini katika kuulizia nimeambiwa ndugu zake ambao walikuwa kijiji kingine walishahama, naendelea kuwatafuta,” anasema.

Mwito wa Matonya

Pamoja na kutamani kuwa mshauri wa vijana na watu wenye tabia za wizi na udokozi, anaiomba jamii na Serikali kumwonea huruma kwa kumwezesha walau kitu chochote cha kuanzia maisha na mkewe ambaye anasema kwamba alikuwa mvumilivu wakati wote licha ya kuzaa watoto watatu nje ya ndoa.

“Mimi napenda kulima, naomba kama ikitokea mtu yeyote akawiwa, anipatie jembe la kukokota kwa ng’ombe (plau) ili linisaidie kufanya shughuli zangu za kilimo,” anasema.