Home Makala Mafanikio Yoyote Yana Sababu (2)

Mafanikio Yoyote Yana Sababu (2)

by Jamhuri
Kufikiria vizuri ni sababu ya mafanikio. Tazama mbele ufikiri. Papa Fransisko alisema kuna lugha tatu: ya kwanza fikiria vizuri, ya pili hisi vizuri, ya tatu tenda vizuri.  Kufikiria vizuri ni msingi wa mafanikio. Kuna aina mbalimbali za kufikiri.
Kwanza ni kufikiria kwa ‘kufokasi’. Fokasi ni mahali miale ya nuru ikutanapo. Kuwa makini na lengo lako. Mambo ambayo si muhimu yanayokuondoa katika lengo lako usiyatilie maanani.  Kuwa na faili ya mambo muhimu mezani kwako yafuatilie kila siku. Fanya unalolifanya.
Kuna aliyeulizwa siri ya mafanikio alisema hivi: “Ninaposimama, nasimama; ninapokwenda, nakwenda; Ninapokaa; nakaa; ninapozungumza, nazungumza; ninapokula, nakula.” Mtu aliyemuuliza alisema, “Sawa kabisa, hayo ndiyo kila mmoja wetu hufanya. Lipi la zaidi unalofanya?”
Alijibu tena: “Ninaposimama, nasimama; ninapokwenda, nakwenda; Ninapokaa; nakaa; ninapozungumza, nazungumza; ninapokula, nakula.” Tena mtu yule yule aliyeuliza alisema: “Lakini hayo ndiyo tufanyayo.”
Naye alisema: “Hilo si kweli. Unaposimama, tayari unafikiri namna ya kukaa. Unapokwenda, tayari unafikiri juu ya kuwasili. Unapozungumza, tayari unafikiri yale utakayofanya. Na unapokula, huko tayari kutoka chumbani.”
Pili, ni kufikiria kiuhalisia. Wajibu wa kwanza wa mtu anayeelekea kwenye mafanikio ni kubainisha uhalisia. Uhalisia unakupa msingi wa kujenga.  Ngamia na mtoto wake walikuwa wakizungumza siku moja. Mtoto wa ngamia akauliza, “Mama kwa nini tuna miguu yenye vidole vikubwa vitatu?
Mama yake alijibu “Ili kutusaidia kutembea kupitia kwenye mchanga mwororo wa jangwa bila kuzama.” Mtoto wa ngamia aliuliza swali jingine, “Kwa nini tuna kope nzito na ndefu?” “Ili kuzuia mchanga usiingie machoni.” Alijibu mama ngamia.
Mtoto wa ngamia aliendelea kuuliza maswali, “Je kwa nini tuna nundu au kibyongo mgongoni?” Mama alijibu, “Nundu inatusaidia kutunza mafuta katika safari ndefu ya jangwani na pia tunaweza kusafiri mwendo mrefu bila maji.”
Mtoto wa ngamia alianza kushangaa na kusema, “Nimekuelewa vizuri sana mama kila kitu tulichonacho kinatusaidia kuishi jangwani kama ni hivyo tunafanya nini hapa kwenye zoo, bustani ya wanyama na hili sio jangwa.” Je, upo mahali unapaswa kuwa?
Tatu, ni kufikiria kimkakati. Watu wengi wanatumia muda mwingi wakipanga namna ya kufurahia kipindi cha mapumziko kuliko kupanga juu ya maisha yao. Kutenda wema unaweza kuwa mkakati wa mafanikio. Kuna mtu ambaye alikodi teksi siku nzima. Baada ya kuzunguka jiji zima, alitoa pochi yake kumlipa dereva wa teksi.
Dereva alikataa kupokea malipo. Dereva alisema: “Nimekuwa nikiendesha teksi kwa muda wa miaka 20 sasa. Katika miaka hiyo umekuwa mtu wa kwanza kunitakia “Asubuhi Njema,” kabla ya kupanda teksi yangu. Kwa hiyo nimeamua kutokutoza hela kama namna yangu ya kushukuru heshima yako.”
Nne, ni kufikiria kiubunifu. Jiulize maswali haya: kwa nini jambo lifanyike namna hii tu? Nini chanzo cha tatizo hili? Ni masuala gani yanalizunguka tatizo hili? Hili linanikumbusha nini? Nini kinyume chake? Ni ishara gani au taswira gani inalielezea vizuri? Kwa nini ni muhimu? Nani anamtazamo tofauti katika hili? Jambo gani litatokea kama hatulitatui?
Kuna wanafunzi walioulizwa. Nusu ya nane ni ngapi? Mmoja alijibu ni tatu. Alichekwa. Mwingine alijibu ni ziro. Alichekwa. Wa mwisho alijibu ni nne. Alishangiliwa. Aliyejibu kuwa ni tatu. Alijitetea. Alisema ukichukua umbo la nane ukalikata katikati wima una tatu mbili zinatazamana. Alifikiria kiubunifu.
Aliyejibu kuwa ni ziro alijitetea. Alisema kuwa ukichukua umbo la nane ukalikata katikati una ziro juu na ziro chini. Bila shaka aliyevumbua ndege chombo cha usafiri alimtazama dege anayeruka angani.

You may also like