NINA NDOTO (28)

Tumia kichwa chako vizuri

 

Kila mtu amezaliwa na kichwa chenye ubongo  kinachoweza kufanya mambo makubwa. Akili aliyopewa mwanadamu ikitumika vizuri inaweza kufanya mambo makubwa na pia kusaidia kutimiza ndoto nyingi.

Mtu asiyeweza kutumia akili tunasema amerukwa  akili au ni mwendawazimu. Ni mwendawazimu tu ambaye hawezi kutumia kichwa chake vyema.

Ipo wazi kuwa kama wewe hujarukwa akili, basi unawezakufanya mambo mengi kama utauruhusu ubongo wako kufikiria mambo ya msingi. Kila chema au kizuri unachokiona na kukifurahia tambua kuwa kuna mtu wakati fulani alitumia akili yake vizuri.

Iruhusu akili yako itengeneze picha unayoitaka. Kama ubongo wako hauwezi kutengeneza picha, basi kichwa ulichonacho hakiwezi kuwa na ndoto yenye maana kubwa.

Ndoto nyingi huwa zinaanza kwa kuonekana kana kwamba haziwezi kutimilizika kwa sababu

watu wengi hawana picha kichwani. Watu wenye uwezo wa kutengeneza picha vichwani mwao ndio wanaotengeneza na kuvumbua vitu.

Watu wanaojenga picha kichwani ndio hufanya vitu visivyoonekana viweze kuonekana. Tumia kichwa chako kutengeneza picha nzuri ya ndoto yako.

Kila kitu huanza na picha ambayo hujichora kichwani mwa mtu. Picha hiyo ndiyo humfanya mtu awe na shauku ya kutimiza ndoto yake. Yusufu alikuwa na picha ya kuwa kiongozi mkubwa.

Unapokuwa na picha kichwani huwa unaona mwisho wa kitu na siyo mwanzo wa kitu. Kama huoni mwisho wa ndoto yako jua kwamba bado hujaruhusu kichwa chako kitengeneze picha.

Anayetaka kuanza biashara ya chakula anaanza na kuona kichwani mwake hoteli kubwa yenye viwango vya nyota tano. Anaona wahudumu wanaotoa huduma ya viwango vya juu. Anaona watu wakipishana mlangoni kila mmoja akihitaji chakula bora na kitamu kutoka katika hoteli.

Anaona jioni akifanya hesabu za fedha alizoingiza.

Mwanafunzi anayefanya vizuri darasani huwa na picha yaushindi tangu siku ya kwanza mwalimu anapoingia darasani. Huona ratiba yake nzima itakavyokuwa, huona vitabu atakavyosoma, huona watu watakaompa msaada pindi atakapokuwa amekwama.

Picha huchukua asilimia 75 ya kile ulichokibeba au unachotaka kukifanya; na asilimia 25 ni kile unachoweka katika matendo.

Mtu anayesanifu majengo huanza na kuona jengo litakavyokuwa kabla hata ujenzi wa msingi haujaanza. Anaona mpangilio wa vyumba, anajua nyumbaitakuwa na vyumba vingapi na vyenye ukubwa kiasi gani, anajua rangi itakayopakwa kutani. Anajua ni aina gani ya mabati itatumika. Hii ndiyo asilimia 75 ya picha anayokuwa nayo msanifu majengo.

Ujenzi wa jengo zima huchukua asilimia 25 tu ingawa unaweza kuwa mradi mkubwa. Ukitaka kufanya ndoto yako iwe kubwa jua ni picha gani unataka kuileta katika uhalisia.

Watu wengi hawafanyi mambo makubwa kwa sababu tu hawana picha vichwani mwao ya jambo gani wanataka kulifanikisha.

Tukikuuliza wewe, je, ndoto yako imebeba picha gani? Unaweza kutupa majibu? Hilo ndilo swali ambalo napenda ubaki unajiuliza.

Picha huja kichwani kwa kufikiria, kuchunguza, kusikiliza na kusoma. Mazingira yetu yanayotuzunguka yana vitu vingi ambayo tukivichunguza vinaweza kutupa picha ya kufanya mambo makubwa katika jamii zetu.

Kuna watu walioona nzi na mwewe wakiruka hewani wakapata picha za kutengeneza chombo kinachoweza kuruka kama wadudu au ndege hao, hapo ndipo wazo la kutengeneza ndege likaja.

Rafiki yangu Hubert Buchuma ambaye ni msanifu majengo alipoona ndege akipaa juu angani akapata picha ya jengo ambalo muundo wake ukiutazama kwa juu unaona ndege akipaa.

Kuna walioona kasi ya farasi katika kutembea umbali mrefu na kutumika kama chombo cha usafiri wakaona kuna kitu kinachoweza kuwa na magurudumu kinachoweza kutembea zaidi ya farasi, picha ya magari ikaja vichwani mwao.

Steve Jobs alikuwa na picha ya kompyuta ndogo zinazoweza kubebeka. Leo hii tuna Ipad na simu janja za Apple.

Uwezo wa kichwa chako kutengeneza picha kubwa ndio utakaochangia wewe kuwa na ndoto kubwa. Iruhusu akili yako ifunguke na kuwaza mambo makubwa. Jiweke karibu na marafiki wenye picha kubwa. Tafuta watu waliofanikiwa katika kile unachotamani kukifanya. Jenga  ukaribu nao. Soma vitabu au historia zao kama zipo.

Jenga picha ya ndoto yako kwanza. Tumia kichwa chako vizuri. Hakuna atakayefikiri kwa niaba yako. Beba wajibu wako.