Na Joe Beda Rupia,JamhuriMedia

Mwaka 2017, Mamlaka ya Mapato nchini (TRA) ilitangaza zaburi ya kimataifa ya usambazaji, ufungaji na uendeshaji wa mfumo wa stempu za ushuru za kielektroniki.

SICPA, kampuni ya Uswisi inayomilikiwa na familia iliyoiasisi, ilipata zabuni hiyo na kupewa kazi ingawa haimo kwenye orodha ya soko la hisa.
Mwaka uliofuata, 2018, mfumo huo wa stempu za ushuru wa kielektroniki ukaanza kufanya kazi katika viwanda vya tumbaku, mvinyo (wines), vinywaji vikali (spirits), vinywaji baridi, maji na vingine kadhaa.

Hata hivyo, maofisa wa viwanda husika hawakuufurahia mfumo huu, wakilalamikia gharama kubwa za stempu hizo walizopaswa kuzinunua kwa ajili ya kila bidhaa waliyoitengeneza au kuiagiza kutoka nje ya nchi.

Kwa upande mwingine, hesabu za haraka zinaonyesha kuwa, kati ya mwaka 2018 na 2021, SICPA walikusanya walau Sh bilioni 100 kwa mwaka!
Bila shaka fedha zote hizo zililipwa na viwanda husika; lakini ukweli ni kwamba, aliyeumia zaidi au aliyelipa fedha hizi ni Mtanzania wa kawaida (mlaji/mteja) ambaye ndiye mtumiaji wa mwisho wa bidhaa za viwandani.

Huenda TRA ama waliliona hilo au walishinikizwa kutokana na malalamiko ya wenye viwanda na wateja, hivyo wakaamua kutafuta suluhu walau kupunguza gharama, ndiyo maana Februari mwaka huu wakatangaza zabuni nyingine.

Vigezo vya zabuni hii mpya havikutofautiana sana na vile vya mwaka 2017, ingawa hadi sasa, pamoja na kupita siku 120 zinazotakiwa kisheria, mshindi hajapatikana au tuseme hajatangazwa.

Hali hii inatia shaka na kusababisha kuwapo kwa tetesi kwamba kuna dalili ya zabuni kurejeshwa kwa kampuni ileile (SICPA).

Taarifa hizi si njema hata kidogo kwa Mtanzania wa kawaida, pia haziwafurahishi wawekezaji na wamiliki wa viwanda nchini, hasa kwa kuwa wengi wanafahamu kwamba mmiliki wa SICPA anafanyiwa uchunguzi akihusishwa na vitendo vya rushwa.

Uchunguzi huo unafanywa na Kitengo cha Kudhibiti Rushwa ndani ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu (OAG) nchini Uswisi; makao makuu ya SICPA.

Kwa mujibu wa gazeti la mtandaoni linalojihusisha na masuala ya uhalifu wa kiuchumi, Gotham City (gothamcity.ch), mmiliki na Mkurugenzi wa SICPA, Philippe Amon, amejumuishwa katika uchunguzi uliofunguliwa mwaka 2015 na OAG dhidi ya kampuni yake.

Uamuzi wa kupanua wigo wa uchunguzi hadi kumfikia ‘mmiliki na ofisa mtendaji mkuu (CEO) wa sasa wa SICPA’ ulifanyika Juni 2021.

Ofisi ya Mashitaka ya Uswisi imesema, ingawa bado hajapatikana na hatia, Philippe Amon, anachunguzwa kwa tuhuma za kuwahonga maofisa wa kigeni wa mataifa mbalimbali yakiwamo Brazil na Colombia.

Si jambo la kawaida hata kidogo kwa ‘kigogo’, mmiliki na CEO wa kampuni kubwa iliyopo Uswisi kufunguliwa uchunguzi wa rushwa na makosa ya jinai ya kimataifa, ndiyo maana Watanzania wengi wanaofuatilia masuala ya kimataifa wanapata shaka juu ya uadilifu na sifa ya SICPA kufanya biashara nchini.

Wakati wigo wa uchunguzi unapanuliwa Juni mwaka jana hadi kumfikia Philippe Amon, nchini Brazil (asili ya bilionea huyu) ambako kampuni yake inahusishwa katika kesi kubwa ya rushwa, kulitangazwa makubaliano ya ushirikiano yaliyosainiwa na SICPA na mamlaka za serikali.

Katika makubaliano hayo yaliyotangazwa Juni 6, 2021, SICPA ilikubali kulipa faranga milioni 135 (sawa na Sh bilioni 325) kumaliza taratibu za kisheria na kupata haki ya kushiriki katika zabuni mpya zinazotangazwa nchini Brazil.

Mamlaka za kiserikali jijini Brasilia zinasema, SICPA; “imechukua hatua ya kumuomba Mdhibiti Mkuu (CGU) na Mwanasheria Mkuu (AGU) kuzungumzia makubaliano ya ‘kuonewa huruma’.

“SICPA imeleta kwetu taarifa, nyaraka na ushahidi wa ukiukwaji (wa sheria) uliogunduliwa wakati wa uchunguzi wake wa ndani.”

Siku moja baadaye, yaani Juni 7, 2021, kampuni hii ilitoa taarifa kwa vyombo vya habari kuhusu suala hilo, ikikiri kuhusika kwake katika “makosa yaliyofanywa katika malipo kadhaa”, lakini inakataa kwamba “mikataba inayohusishwa ilipatikana kwa njia za ulaghai.”

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, inasema: “Kwa upande wa SICPA hakukuwa na uhusika, ufahamu, au nia (mbaya) iliyogundulika katika malipo yaliyofanyika Brazil.”

Ni vema ikafahamika kwamba Mamlaka za Mapato za Brazili hazikuuhuisha (renew) mkataba uliosababisha SICPA kufanyiwa uchunguzi nchini humo.

Vifaa vyao vyote vilivyofungwa viwandani viliondolewa (au kuzimwa) huku viwanda vya vyakula na vinywaji vikirejea katika mifumo ya zamani ya uwajibikaji katika uzalishaji.

Ndiyo maana sasa, sekta ya tumbaku na vinywaji, pamoja na walipa kodi wa Tanzania, wanaitazama TRA kwa matumaini kwamba hakutakuwapo gharama zilizofichwa nyuma ya ushuru wa stempu, huku wakitaka kujua gharama zinazohusu mfumo mpya.
0679 336 491

By Jamhuri