Kuna kitu kinaendelea katika mechi za Kombe la Shirikisho la Azam ambacho hata mashabiki wa soka hawakifurahii ingawa kwa nje kinaonekana kizuri kwa timu zao. Azam wameshinda 9-0 dhidi ya Malimao FC, Simba nao wameshinda 8-0 na Ihefu nao wakaishindilia Mtama Boys 9-0 lakini haijawa stori kubwa kwa sababu ni ‘ushindi wa Twaha Kiduku dhidi ya Mandonga’. 

Nimejaribu kutafakari ikiwa TFF na Kamati zake walifikiria kuhusu hali ya ushindani katika hatua hii ya pili ya Michuano ya Kombe la Shirikisho la Azam? Michuano imekuwa rahisi sana kwa timu za ligi kuu kwa sababu timu za ligi kuu zina wachezaji wa ndani na nje wenye uzoefu na maslahi makubwa wanayopata klabuni kwao tofauti na timu wanazokutana nazo toka madaraja ya chini. 

Kamati zinazosimamia Mashindano ya Kombe la Shirikisho la Azam zinatakiwa kufikiria kuhusu kanuni za mashindano hayo ili kuleta ushindani wenye tija kwa faida ya soka la nchi yetu. Inahitajika mipango madhubuti itakayoleta ushindani sahihi kwa faida ya taifa letu. 

TFF wanatakiwa kujua mashindano yale yanatoa mwakilishi wa mechi za kimataifa na hivyo ni vizuri michuano hiyo ikiwa na ushindani sahihi na sio kuwa kama mechi za ‘bonanza’ kwa afya ya soka letu hasa ushindani sahihi kwa timu za ligi kuu na timu za madaraja ya chini. 

TFF inapaswa kuweka kanuni katika idadi ya wachezaji wa kigeni katika michuano hiyo ili wazawa wapate nafasi ya kucheza kwa faida ya soka letu, vilevile TFF wanaweza kuweka kanuni ya timu hizo za ligi kuu kutumia wachezaji wa timu za vijana walau watatu mpaka wanne uwanjani ili kuweka chachu ya kukuza vipaji kwa faida ya taifa letu. 

Ikiwa TFF itaacha mechi hizi ziende tu bila kanuni ya kuweka vizuri mizania ya ushindani wenye tija basi timu za madaraja ya chini hazitaona umuhimu wa kutumia gharama kubwa kushiriki michuano ambayo wanajua wanakwenda kushindwa vibaya. Vipigo vya magoli 8 mpaka 9 sio vya ajabu kutokea lakini inapotokea katika mechi tatu mfululizo ni lazima TFF itafakari hii vita ya Mandonga na Twaha Kiduku.