Hakika hakuna kama Morocco kwa Afrika wala kwa nchi zote za kiarabu baada ya kufanikiwa kutinga hatua ya nusu fainali ya Kombe la Dunia mwaka 2022 huko nchini Qatar. 

Morocco ndio nchi ya kwanza toka Afrika kutinga katika hatua ya nusu fainali ya Michuano ya Kombe la Dunia toka dunia iumbwe lakini Morocco wanafanya hivyo ikiwa ni mara yao ya kwanza kutinga hatua ya robo fainali katika michuano kisha wameishangaza dunia kwa kutua hatua ya nusu fainali ya Kombe la Dunia. 

Katika timu nne zilizofuzu hatua hiyo ya nusu fainali ya michuano hiyo ni Morocco na Ufaransa pekee ambao wamefuzu kwenda hatua ya nusu fainali kwa ushindi wa ndani ya dakika tisini baada ya kuifumua Ureno kwa goli 1-0 na kufutilia mbali ndoto za Cristian Ronaldo kutwaa taji hilo katika maisha yake ya soka. 

Morocco waliotinga hatua ya robo fainali ya Michuano ya Kombe la Dunia kwa kuitoa Hispania kwa penati imekuwa timu ya kwanza toka Afrika kupata mafanikio makubwa kwenye Kombe la Dunia ikiwa na kocha mzawa, Walid Regragui, ambapo kabla ya hapo hakuna timu toka Afrika imewahi kufanya lolote la maana kwa kumtumia kocha mzawa. 

Morocco hawataondoka Qatar mpaka Michuano ya Kombe la Dunia itakapofika tamati yake kwa kucheza fainali ili kumpata bingwa ikiwa wataifunga Ufaransa na kuingia fainali lakini pia watasalia ili kucheza mechi ya kumtafuta Mshindi wa tatu wa michuano hiyo ikiwa watashindwa kuingia fainali.

 Hii historia kubwa imeandikwa kwa bara la Afrika na nchi zote za kiarabu baada ya timu hiyo kutinga nusu fainali ikiwa haijapoteza hata mechi moja toka michuano hiyo ianze huko Qatar. 

By Jamhuri