Simba haina tatizo ila imezungukwa na watu wenye matatizo wasiotaka mabadiliko. Ukiona taasisi inakubali kupoteza wasomi wake kirahisi ujue kuna watu hawataki klabu ipige hatua. Simba inarudi nyuma badala ya kwenda mbele. 

Baniani mbaya kiatu chake dawa. Yawezekana Mo Dewji ana mapungufu lakini ndiye ameifanyia mema klabu kuliko hao wanaojiona wakamilifu. Haipingiki Babra alikuwa pale kwa kulinda maslahi ya Mo kama ambavyo Eng. Hersi amepenyapenya mpaka kuwa rais wa Yanga ili kulinda maslahi ya GSM. 

Inawezekana kabisa kukawa kuna mapungufu katika utaratibu huo wa watoa pesa kuwa na watu wao ndani ya klabu lakini ukweli ni kuwa klabu zetu hizi pendwa zimejaa ‘wapigaji’ na hakuna namna tajiri atatoa pesa zake ‘zipigwe’ kizembe tu. 

Tufahamu mpira wa miguu hauzalishi faida kwa wamiliki wake kwa hiyo wengi wanaotia pesa zao kwenye mpira ni kwa ajili ya kujipatia furaha kwa mafanikio ya timu wa wanazozipenda na timu zikifanya vizuri walau hata matangazo yao ya biashara yanatembea vyema kwenye jezi za timu hizo. 

Kwa kuwa hakuna faida ya moja kwa moja katika kuwekeza katika klabu za mpira wa miguu hasa hizi klabu zetu pendwa ni wazi tajiri yeyote hatakubali kuweka pesa zake bila kuwa na uhakika wa usimamizi sahihi wa pesa zake na kuleta matokeo sahihi ambayo yatamfanya aone thamani ya pesa (value for money) ya kile anachokitarajia. 

Zitatolewa nyingi sana lakini ukweli kuachia ngazi kwa CEO wa Simba Barbara Gonzalez ni moshi mweusi sio tu kwa Simba bali Kwa soka letu kwa sababu uimara wa Simba na Yanga ndio unaovutia wawezekezaji kuamini wanaweza kuwekeza katika soka letu na wakaona mafanikio. 

Simba wanafanya makosa haya wakiwa wanajua matajiri wengi wa mpira wanaogopa sana kuingia kwenye hizi klabu kwa sababu ya ukigeugeu unaoweza kugharimu uwekezaji wao mbele ya safari. 

Yanga wanajua kilichowakuta baada ya kupuuza uwekezaji wa Yusufu Manji na wakaja na kejeli kibao kwamba klabu yao sio masufuria ya sherehe mpaka ikodishwe lakini ‘msoto’ waliopitia mpaka kusimama imara uliwagharimu mengi mpaka ujio wa GSM ulipokuja kuwanusuru.