Upo wakati katika ndoa ambako mmojawapo anaweza akawa anataka kuuza au kubadili jina la nyumba/kiwanja bila ridhaa ya mwenzake ilhali nyumba hiyo ni ya familia.

Lakini pia nje ya hilo, kuna mazingira ambayo mtu anaweza kuwa si mwanandoa, lakini ana maslahi katika nyumba au kiwanja cha mtu fulani na anataka kuzuia nyumba/kiwanja hicho kisibadilishwe jina au kisiuzwe.   Kisheria jambo hilo linaruhusiwa na huitwa zuio (caveat).

Hili si zuio la kwenda mahakamani kama mazuio tuliyoyazoea. Hili ni zuio jingine kama nitakavyolieleza. Aidha kuzuia hati isibadilishwe kimsingi ni sawa na kuzuia nyumba isiuzwe.

Hii ni kwa kuwa hakuna namna ambavyo mnunuzi anaweza kununua kitu ambacho hakiwezi kubadilika na kuingia katika jina lake. Ikiwa mke ana wasiwasi kuwa mume anaweza kumzunguka na kuuza mali ya familia au mume ana wasiwasi juu ya uwezekano wa mke kuuza, basi wanayo ruhusa ya kuweka zuio ili hati ya nyumba isibadilishwe.

Yapo mambo mengi kuhusu hili nitaeleza baadhi.

  • Nini maana ya zuio

Zuio ni usitishwaji wa muda ambao huwekwa ili kuzuia mabadiliko yoyote katika hati. Kama maana yenyewe inavyojieleza, huu unakuwa ni usitishwaji wa muda ambao unalenga kulinda maslahi ya mtu aliyeomba zuio.

Kuitwa zuio la muda haimaanishi kuwa mtu akizuia itakuwa ni mwezi mmoja au miwili, basi, hapana. Ni zuio la muda kwa kuwa haliwezi kukaa milele lakini mtu akishaliweka linaweza kukaa hata miaka mingi kutegemeana na sababu za zuio hilo.

  • Mwanandoa kuzuia hati isibadilishwe

Lazima ieleweke wazi kuwa si kila mtu anaweza kuamua na akazuia hati ya mtu isibadilishwe. Wapo watu ambao kwa mujibu wa sheria wana haki ya kuomba hati isibadilishwe.

Kwanza mke au mume; mmoja kati yao anaweza kuweka kizuizi katika nyumba ya ndoa (matrimonial home) iwapo kuna dalili kuwa mmiliki aliyeandikishwa anaweza kuiuza au kuiweka rehani bila ya ridhaa ya mwingine.

Mara nyingi migongano katika familia inapoanza, mmoja kati ya wanandoa hukimbilia kuuza baadhi ya mali kwa ama kumkomoa mwenzake au sababu nyingine yoyote. Kwa hiyo, ili kuliepuka hilo unapogundua  kuwa  kuna  uwezekano  huo, basi  sheria  imekuruhusu  mwanandoa  kuweka  zuio  ili  hati  isibadilishwe  na hivyo kuepuka kuuzwa kwa  mali.

  • Wapi upeleke maombi ya kuzuia hatia isibadilishwe

Mamlaka za ardhi ni mamlaka ambazo hutakiwa kupelekewa maombi haya ya zuio. Mara nyingi mamlaka za ardhi huwa zipo  katika ofisi za wilaya au manispaa katika mkoa wako, isipokuwa  kwa walio Dar  es Salaam maombi hupelekwa makao makuu  pale Wizara ya Ardhi kama ni hati.

  • Hati huandaliwaje

Maombi haya si maombi kama maombi mengine yalivyo. Maombi haya ni maombi ya kisheria na huandaliwa katika ofisi za wanasheria na hupelekwa yakiwa na muhuri wa mwanasheria.

Katika maombi hayo mwombaji hueleza jina lake kwa urefu, anuani yake, uhusiano wake na yule ambaye jina lake ndilo lililoko kwenye hati, yaani anayemwekea zuio huku akieleza sababu za msingi kwanini anataka kuzuia hati isibadilishwe.

  • Lazima maombi yaambatane na nyaraka

Kwanza, picha mbili za mwombaji huku kila picha moja ikibandikwa kwenye nyaraka moja. Pili, risiti za malipo ya ada ya usajili. Maombi haya hulipiwa kiasi cha fedha lakini si kikubwa sana kwa hiyo lazima uambatanishe na risiti za malipo.

Tatu, mwombaji aambatanishe vielelezo vinavyompa haki juu ya kiwanja husika, kwa mfano cheti cha ndoa, mkataba wa mkopo na kadhalika.

Kusoma mambo mbalimbali ya kisheria tembelea sheriayakub.blogspot.com

 

By Jamhuri