Mara nyingi nimeandika kuhusu mirathi, lakini zaidi nimegusia habari ya usimamizi wa mirathi. Leo nimeona ni muhimu kueleza mgawo wa mirathi kwa kuangalia nani anapata nini kupitia sheria ya mirathi ya Serikali.

Mgawo ukoje ikiwa mume amefariki?
Kama mume amefariki na akaacha mjane na watoto, basi moja ya tatu (1/3) ya mali za marehemu zilizo kwenye mirathi anatakiwa apewe mke wake. Mbili ya tatu (2/3) ya mali hizo itaenda kwa watoto wake.

Kama kuna mjane
Kama hakuna watoto walioachwa na marehemu katika familia husika, lakini kuna mjane, mali za marehemu hugawanywa katika mtindo ambao ndugu hupewa nusu (1/2), na mjane hupewa nusu ya mirathi ya marehemu. Hii ni sawa kwa sawa.
 
Mgawo ukoje iwapo marehemu hakuacha ndugu wala mtoto, isipokuwa mjane tu?
Kama marehemu hakuacha ndugu wala mtoto au watoto, basi mali yote huchukuliwa na mjane. Ndugu hapa ni kwa maana ya hapa ni kaka, dada, mama mzazi wa marehemu au baba na kadhalika.
 
Kama mke amefariki na kamuacha mume, watoto?
Hapo juu tumeona mume akifariki akamuacha mke na watoto, mke huchukua moja ya tatu na watoto au mtoto mbili ya tatu. Hali iko vivyo hivyo, kwa mume naye ana haki kama alizo nazo mke wake yaani kupata mirathi kutoka katika mali za marehemu. Kwa maana hiyo, mume hupata moja ya tatu (1/3) ya mali za marehemu mkewe na mbili ya tatu (2/3) huenda kwa watoto.
 
Mgawo ukoje ikiwa mke kafariki na kumuacha mume bila watoto?
Kama mke amefariki amemuacha mume, lakini hakuna watoto, inaangaliwa kama kuna ndugu. Ikiwa kuna ndugu basi ndugu hao wa mke hutakiwa kupata nusu ya mali (1/2) na nusu inayobaki huenda kwa mume. Kwa hiyo, ndugu wa mwanamke ambaye ni marehemu hupata sawa kwa sawa na mume wake aliyeachwa.
 
Mgawo ukoje ikiwa mke amefariki na hakuacha ndugu isipokuwa kuna mume tu?
Ikiwa mwanamke ndiye aliyefariki na hakuacha ndugu yeyote wala mtoto yeyote isipokuwa kamuacha mume wake tu, basi mume huyo huchukua mali zote za mkewe.
 
Mgawo wa mali ukoje iwapo wazazi wote wamefariki ila wamebaki watoto/mtoto?
Sheria inasema kwamba kama wazazi wote wawili wamefariki, basi mali za marehemu hupewa watoto wao. Kama mtoto ni mmoja na yuko peke yake hutakiwa kuchukua mali zote peke yake. Nasisitiza hapa kuwa hii ni bila kujali mali ni nyingi kiasi gani, kama mtoto yupo peke yake atachukua yote. Hapo hakuna ndugu wala wazazi wa marehemu. Pia kama wapo wengi, basi watoto hao hugawana mali hizo sawa kwa sawa bila kujali ni mwanamke au mwanaume.
 
Mgawo ukoje ikiwa baba, mama wamefariki na hata watoto wao wamefariki?
Kama wazazi wote — baba na mama — wamefariki, lakini pia na watoto wao wote nao wamefariki, mali huenda kwa wajukuu. Bila kujali mjukuu ni wa kike au wa kiume, mgawo hutakiwa kwenda sawa kwa sawa.
 
Mgawo ukoje ikiwa mtoto mwenye mali amefariki na kuacha wazazi?
Wakati mwingine huwa inatokea wazazi wana mtoto hajaoa/hajaolewa na wala hana mtoto, lakini ana mali. Mtoto huyu akifariki mali zote huenda kwa wazazi wake. Mgawo huu ni kwa mujibu wa sheria ya Serikali.

By Jamhuri