Ustaarabu wetu adhimu wa Kiafrika turiourithi kutoka kwa wahenga unatutaka vijana kuwa na heshima na kufanya maamkizi kwa wakubwa – 'shikamoo komredi Zitto Kabwe'.
Nakuandikia barua hii nikifahamu pasi shaka yoyote kuwa kamwe hutaishangaa.
  Kama ujuavyo, uandishi wa barua za namna hii una historia ndefu tangu zama za Uyunani za mwanafalsafa Plato na hata karne nyingi kabla yake. Nakuandikia barua yangu hii kuendeleza utamaduni huu jalili.
  Jambo pekee linalotia mshawasha mkono wangu kuandika barua hii, ni kiu yangu ya kutoa maneno yenye kufaa, maneno ya kuwatia moyo na kuwahamasisha wanyonge kama zinavyofanya barua nyingi katika historia ya ulimwengu. Mifano ya barua hii ipo mingi na bila shaka mwanafalsafa wa aina yako lazima unazifahamu.
  Ni imani yangu kwamba kwa barua ya Patrice Lumumba, kiongozi wa Kongo kwenda kwa mkewe, Pauline, akiwa chini ya udhibiti wa waasi kabla ya uhai wake kupokwa kinyama  kwa msaada wa mabeberu wa ng'ambo ambao sasa ndiyo wahubiri wetu wakubwa wa haki za binadamu, unaifahamu.
  Katika barua yake alieleza bayana siku itakuja ambako wana wa Afrika wataandika historia yao badala ya ile feki inayoandikwa kwa kalamu feki za Washington, Brussels na London.
  Unadhani barua ya Patrice Lumumba yalikuwa maneno matupu na ndoto ya mchana ambayo haitatimia kamwe?
Unadhani Bara la Afrika, licha ya kuwa na utitiri wa waitwao wasomi, litaendelea kuwa likizo kifikra na kusubiri  mustakabali wake upikwe kutoka ughaibuni?
  Ikumbuke pia ile barua ya komredi Vladimir I. Lenin, mwanafalsafa na mwanamapinduzi  wa Kirusi kabla ya mauti haijamkuta. Aliandika kuhusu mustakabali wa Urusi ambao uliwatetemesha kwa hofu kubwa viongozi wa Urusi akina Joseph Stalin.
  Kumbuka barua za Mahatma Gandhi, Baba wa Taifa la India, akiwa mwanasheria machachari Afrika Kusini kwenda kwa mwanafalsafa wa Kirusi, Leo Tolstoy. Sote tunakumbuka kuwa utaratibu huu wa kuandikiana barua kati ya Gandhi na Tolstoy ndiyo ulionoa makali ya Gandhi katika falsafa ya uasi wa jamii dhidi ya mfumo kandamizi (civil disobedience).
 Pia mwandishi wetu nguli wa Kiswahili, Shaaban Robert, aliandika katika barua zake kati ya 1931-1958 kwenda kwa nduguye Yusuph Ulenge zilizochapwa kwenye kitabu chake cha 'Barua za Shaaban Robert'.
  Hata ile barua ya komredi Jenerali Ulimwengu kwenda kwa Rais Jakaya Kikwete baada ya kuukwaa ukuu wa nchi mwaka 2005 nadhani unaikumbuka. Naweza kusema huyo alikuwa Jenerali Ulimwengu katika kilele cha ubora wake –  that was Jenerali at his best.”
  Kuna raha gani ya kijana kama mimi mwenye hamu ya kuleta mapinduzi kwenye jamii zaidi ya kufuata njia kama hii aliyosafiri nayo Gandhi? Nijuze Tolstoy wangu. Mimi ni kinda la ndege ambalo haliwezi kumfundisha mama yake kuruka.
  Nimekuwa mfuatiliaji wa kazi zako nyingi tangu uingie bungeni mwaka 2005, umekuwa shujaa na mwanamapinduzi wa hali ya juu sana kwa kutetea maslahi ya wanyonge na Taifa kwa ujumla.
  Kwa muda wako wote ukiwa Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Mashirika ya Umma (POAC) na ukiwa Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), umefanya kazi kubwa ambazo si rahisi kuzitaja zote.   Ulionesha umahiri mkubwa sana kuwatetea wananchi waishio kandokando ya Mgodi wa Dhahabu wa Buzwagi ili kupata stahiki zao sehemu ambayo si hata jimbo lako.
  Katika Bunge la tisa ilikuwa Septemba 3, 2008; ulionesha umahiri mkubwa sana katika sakata la Akaunti ya Madeni ya nje (EPA) na Kampuni ya Richmond.
  Hata katika Bunge la 10 umeonesha ushujaa wa hali ya juu sana ukiwa kama Mwenyekiti wa PAC ndani na nje ya Bunge kwa kukagua miradi ambako pesa za umma zinatumika na pia  katika sakata la Tegeta Escrow.
  Pia umeonesha umahiri mkubwa sana katika kutetea na kusaidia watu kujiunga na Mifuko ya Hifadhi ya Jamii barani Afrika hasa wakulima, wavuvi, wachimbaji wadogo wadogo wa madini, wasanii na wachezaji wa mpira, na kwa kulitambua hilo Umoja wa Mifuko ya Jamii kwa nchi za Afrika Mashariki na Kati (ECASSA) Oktoba 30, 2014, walikutunuku tuzo yao ya kwanza ya kuwa Mtetezi Bora wa Huduma ya Mifuko ya Jamii barani Afrika, hafla iliyofanyikia Hoteli ya Zambezi ya nchini Zambia.
  Umefanya hivyo kwa kutambua umuhimu wa mifuko hiyo katika kukuza uchumi wa nchi hasa kwa wakulima ambao asilimia 80 ya wananchi wa Kitanzania ni wakulima. Umesaidia sana kwa kupitishwa hoja iliyosababisha kutungwa kwa sheria maalum bungeni itakayoisaidia Serikali kupata gawio la kodi la Ongezeko la Mtaji (Capital Gain Tax).
  Mwandishi wa kimapinduzi Frantz Fanon kwenye kitabu chake cha 'The Wretched of the Earth' amesema 'ni lazima kila kizazi kiutambue wajibu wake halafu kiutekeleze au kiusaliti'.' Hakika umetekeleza.
Kwanza, nataka nikuhakikishie kwamba siku yaja vijana wasomi wasio na ajira, wafanyakazi waliofukarishwa na wakulima wanyonywao (mfano pamba), watafumbua macho na kung'amua kuwa mfumo uliopo hauwezi kutoa majibu kwa changamoto zao.
  Hili lina mifano chungu tele katika nchi nyingi barani Afrika, ufagio wa umma umesafisha Ikulu ya Burkina Faso kwa kumwondoa madarakani aliyekuwa Rais wa nchi hiyo, Blaise Compaore, ambaye aliingia madarakani kimabavu baada ya kumuua rafiki yake, Kapteni Thomas Sankara, kwa kushindwa kutimiza matakwa ya wananchi.
  Tunisia pia yalitokea kwa sababu ya kupuuza suala la ajira kwa vijana. Tanzania kwa sasa ukosefu wa ajira kwa mujibu wa takwimu ni asilimia 10.7 kiasi ambacho ni kikubwa kwa Taifa changa kama letu.
  Hatuwezi piga hatua kubwa kiuchumi kama tukilipuuza suala la ajira kwa sababu asilimia kubwa ya nguvu kazi (labour force) hawana kazi. Sote tunajua jinsi uchumi wa Uhispania ulivyokuwa ukisuasua mwaka 2011 wakati ukosefu wa ajira ulipokuwa asilimia 24.7, kiasi kikubwa kuwahi kutokea duniani na vivyo hivyo kwa Ugiriki ilikuwa. Pili, mikataba ya uwekezaji inaligharimu sana taifa.
  “Taifa lilifanya makosa makubwa sana kuruhusu wawekezaji kuvuna rasilimali za nchi huku Serikali ikiwa siyo sehemu ya wamiliki na kutegemea mapato yatokanayo na kodi pekee kwani kwa kufanya hivyo wawekezaji ndiyo wanaonufaika zaidi,” Ludovick Utouh, CAG mstaafu (Nipashe; Septemba 19, 2014 uk.5). Alishauri kwa kusema; “Ni lazima tuwe sehemu ya wamiliki katika uwekazaji wa gesi, mafuta na madini”.
   Tanzania si nchi ya kwanza kugundua gesi, mafuta na madini. Kuna nchi nyingi Afrika ambazo rasilimali hizo zinapatikana, lakini kutokuwa na sera thabiti rasilimali hizo zinageuka kuwa laana (resources curse) kwa kusababisha mauaji ya binadamu na vita.
  Nigeria waligundua mafuta miaka 1960 iliyopita, Afrika Kusini wamekuwa na dhahabu, Siera Leone, Angola na Burkina Faso wote hawa wamekuwa na madini miaka mingi, lakini je, wananchi wa kawaida wana hali gani kiuchumi?
  Sierra Leone miaka ya 1997, wananchi wake waliuawa sana kwa sababu ya almasi. Hata hapa kwetu Tanzania maeneo mengi yanayozunguka migodi mikubwa ya dhahabu mfano North Mara migogoro kati ya wawekezaji na wananchi haiishi. Hili suala linahitaji tujipange. Mwisho, ubinafsishaji kwa iliyokuwa ya Benki ya Umma ya Taifa ya Biashara (NBC) imetugharimu.
  Huwa nawapongeza rafiki zetu wa jadi, China, kwa kazi yao nzuri sana katika kuyawezesha mabenki yao ambayo kwa mujibu wa takwimu za jarida la Forbes mwaka 2014 ndiyo benki kuu tatu zenye mitaji na thamani kubwa zaidi duniani kwa sasa yaani ICBC, China Construction Bank na Agricultural Bank China kwa kuziengua benki zilizokuwa na nguvu miaka mingi JP Morgan, Bank of America, HSBC Holding na BNP Paribas.
  Imechukua miaka 30 tu China kufika hapo walipo leo. Mabenki haya leo hii China yanaajiri asilimia kubwa sana ya nguvu kazi yake. Lakini kwetu Tanzania zaidi ya mashirika 200 yalibinafsishwa katika Awamu ya Pili na ya Tatu ya uongozi, miaka ya 1980 hakukuwapo na tatizo la ajira kwani mashirika haya ndiyo yaliyokuwa yakitoa ajira asilimia kubwa kwa Watanzania.
  Kwa kuwa tuliamua kufuata ushauri zaidi wa vyombo vya Magharibi (IMF na WB) kuhusu ubinafsishaji, leo hii Tanzania tumeiangamiza kwa Ebola ya Ajira. Nina mashaka na uwepo wa viongozi ambao watakuwa na uamuzi mgumu kwa dhati ya mioyo yao kwa kuwa tayari kusimamia misingi ya kiuchumi ili kututoa hapa tulipo.  Prof. Hirji anashauri; ili vijana wasomi wafanikiwe katika mapambano ya kuleta mabadiliko katika jamii, ni lazima waishike misingi muhimu; mosi, kuwa na mioyo halisi ya kupigania haki za wanyonge badala ya kufanya hivyo ili kupata vyeo au manufaa binafsi kutoka katika vyama vya siasa.
  Pili, kushirikiana na watu wa kawaida kwenye shuguli zao. Huwezi kuleta mabadiliko wakati umejitenga na jamii yako. Tatu, lazima pawepo na umoja miongoni mwa wanaharakati. Mwisho, anashauri  vijana kujielimisha kwa kina kihistoria, kiuchumi, sayansi na maendeleo kwa ujumla kwa kusoma vitabu na taarifa mbalimbali zinazotokea kwa muda. Kila kizazi kina jukumu lake, ni sisi wenyewe wenye kuandika historia yetu.
  Kamwe  hatuwezi kulikamilisha jukumu la kukikomboa kizazi chetu kiuchumi  kama tutakuwa na hofu ya kupambana na maovu katika jamii. Hakuna njia rahisi ya kuufikia uhuru popote duniani.
  Kuna siku yaja wakulima, wavuvi, wafugaji na wafanyakazi watazinduka, na barua yangu kwako haitakuwa na maana tena kwa sababu wanyonge wenyewe watachukua kalamu yao kuiandika historia yao wenyewe.
 
Mwandishi wa barua amejitambulisha kuwa ni msomaji wa gazeti, ambako sasa atakuwa mmoja wa wachangiaji katika moja ya kurasa atakazopangiwa baadaye. Ni Mwanafunzi wa Chuo Kikuu Dodoma, anapatikana kwa anwani [email protected] au 0788 375449

By Jamhuri