NIT yanunua ndege za kufundishia marubani

Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) kimenunua ndege mbili ambazo zitaanza kutumika kufundisha Marubani ndani ya nchi ili kupunguza gharama za masomo ya fani hiyo.

Hayo yamesemwa na Mkuu wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) Prof. Zakaria Mganilwa,wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu Utekelezaji wa Shughuli mbalimbali za Chuo hicho na mwelekeo wa utekelezaji wa bajeti kwa mwaka wa fedha 2022/2023 leo Novemba 3,2022 jijini Dodoma.

Prof.Mganilwa ameeleza lengo la kununuliwa kwa ndege hizo mbili ni kukiwezesha chuo hicho kuanza kutoa mafunzo ya Urubani nchini.

“Ndege hizi mbili za injini moja zitakuwa zinatumika kwa ajili ya kujifunza lakini pia badae zitanunuliwa nyingine mbili za njini mbili kwani ni lazima rubani aendeshe ndege ya injini moja na baadae injini mbili ili aweze kuajiriwa na mashirika ya ndege”amesema Prof. Mganilwa

Hata hivyo amesema kutokana na chuo hicho kuanza kutoa mafunzo ya Urubani nchini kutasaidia kupunguza gharama kubwa za kusomesha watu nje ya nchi
Na kuongeza “Hivi sasa tuna ndege 400 zilizosajiliwa na Mamlaka ya Usafiri wa Anga ambapo asilimia 60 ya Marubani ni wageni, hivyo ndege hizi zitakapofika vijana wa kitanzania wenye sifa za kusomea Urubani watafundishwa na kupata ajira ndani ya nchi na Kwa uwekezaji huu unaofanyika, tuna matumaini kuwa Shirika la Ndege la Tanzania litaweza kuwa Shirika bora kwa Afrika,” Prof.Mganilwa

Prof. Mganilwa amesema chuo hicho pia kimeanza kutoa kozi ya ufundi wa kutengeza na kusanifu Meli ili kuepuka changamoto iliyowahi kujitokeza hapo awali ya kufa kwa shirika la Meli nchini.

Aidha amesema kuwa Serikali imekopa takriban Sh49 bilioni kutoka kwa Benki ya Dunia kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha umahiri cha mafunzo ya taaluma za usafiri wa anga na Operesheni za Usafirishaji ambacho kina majukumu ya kutayarisha wataalam wa sekta ya usafiri wa anga.

“Fedha hii imegawanywa katika upande wa ujenzi wa miundombinu kwa ajili ya kufundishia Wataalam ambapo jumla ya majengo matano yatajengwa Dar es Salaam kwa gharama ya Sh21 bilioni na baadae tutajenga majengo mkoani Kilimanjaro kwa sababu lazima marubani wafundishiwe ndani ya viwanja vya ndege,”amesema.

Kwa upande wake Msemaji Mkuu wa Serikali na Mkurugenzi Mkuu wa idara ya Habari -MAELEZO Gerson Msigwa,amesema kutokana na serikali kuwekeza katika miradi mkubwa ya kimkakati chuo hicho kitakuwa msaada mkubwa katika uzalishaji wa rasilimali watu.

“Safari inayofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita ya kuwekeza kwenye maeneo muhimu ya uchumi itategemea sana kuwa na wataalam wetu wa ndani kwani hatuwezi kunufaika na thamani ya miradi yetu kama tunategemea wataalam kutoka nje,”Amesema Msigwa.