Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia

Kufuatia uwekezaji mkubwa uliofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan Hospitali ya Taifa Muhimbili-Mloganzila itafanya huduma ya kibingwa na Bobezi ya Upandikizaji figo kwa wagonjwa watano kuanzia Octoba 2 hadi 6, 2023.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi Msaidizi wa Huduma za Upasuaji, Dkt. Godlove Mfuko upandikizaji huo ni wa kisasa ambapo utahusisha kutoa figo kutoka kwa mchangiaji kwa kutumia njia matundu (Hand Assisted Laparascopic Nephrectomy), utaalamu ambao kwa hapa nchini unafanyika MNH-Mloganzila pekee ukilinganisha na hospitali zingine ambazo humfanyia upasuaji mchangiaji.

Dkt. Mfuko ameongeza kuwa upandikizaji huu unaohusisha kutoa figo kutoka kwa mchangiaji kwa kutumia matundu madogo unamsaidia mchangiaji kutokua na kovu kubwa, kupona mapema na kurudi katika majukumu yake mapema zaidi ukilinganisha na upandikizaji uliozoeleka ambao mchangiaji hufanyiwa upasuaji.

“Hii ni mara ya pili kwa hospitali yetu kupandikiza figo kwa njia ya matundu, hapo awali tuliwafanyia wagonjwa watatu ambao kwa sasa wanaendelea vizuri na mpango wetu ni kufanya upandikizaji wa aina hii kila mwezi” amebainisha Dkt. Mfuko.

Dkt. Mfuko amebainisha kuwa upandikizaji huu umewezekana kutokana na Serikali kuwajengea uwezo wataalamu wetu wa ndani, kununua vifaa tiba na kujenga miundombinu wezesheshi katika kutoa huduma za upandikizaji figo MNH Mloganzila jambo ambalo limesaidia kupunguza gharama kwa wagonjwa kwa zaidi ya asilimia 50 endapo wagonjwa hao wangepelekwa nje ya nchi kwa upandikizaji.

Upandikizaji huu wa figo unafanywa na wataalamu wa ndani kwa kushirikiana na mtaalamu kutoka nchini Korea Kusini Prof. Park Kwan Tae chini ya Taasisi ya Korea Foundation for International Health Care (KOFIH).