Hakuna sheria maalumu ya jumla nchini Tanzania inayozilazimisha kampuni kuchangia miradi mbalimbali ya kijamii. 

Licha ya sheria kuwa kimya juu ya kile kinachopaswa kufanywa na kampuni na wadau wa sekta za ziada katika kuwajibika kwa jamii kupitia CSR, zipo kampuni na taasisi ambazo zimekwenda mbali sana katika kujaribu kushughulika na changamoto na mahitaji ya kijamii.

Ingawa taasisi za kifedha si sehemu ya sheria ya rasilimali za taifa, lakini Benki ya NMB imeamua kuingia katika suala hilo kwa utashi wake binafsi. Benki hiyo imetunga sera rasmi kuhusiana na huduma kwa jamii ambayo inataka itenge na kutoa asilimia moja ya pato lake baada ya makato ya kodi ili zielekezwe katika kusaidia kutatua changamoto na kuunga mkono miradi ya kijamii.

“CSR ya NMB kimsingi imelenga kusaidia sekta za elimu, afya na uwezeshaji katika majanga. Kupitia sera hiyo, benki imekwisha kutumia takriban Sh bilioni 4 kusaidia miradi ya kijamii katika miaka minne iliyopita. Kwa kufanya hivyo, NMB imeongeza nguvu katika juhudi za serikali kukabiliana na changamoto za kijamii na kujenga misingi imara ya utoaji wa huduma bora kwa mamilioni ya Watanzania,” anasema Ruth Zaipuna, Mkurugenzi Mtendaji Mkuu wa NMB.

 Utekelezaji wa ahadi ya elimu bure ulisababisha ongezeko kubwa la wanafunzi katika shule na kwa mantiki hiyo kukawa na mahitaji makubwa ya miundombinu, vifaa vya kujifunzia na vifaa vya kufundishia ili kuziwesha shule kutoa elimu nzuri.

Kwa kutambua umuhimu wa hilo na kwa kuiunga mkono serikali, NMB ikaja na misaada kupitia CSR, ambayo hadi sasa imewanufaisha zaidi ya wanafunzi 93,000 wa shule za msingi na sekondari nchini kote.

Kupitia sera hiyo, hadi sasa Benki ya NMB imefanikiwa kuchangia jumla ya madawati 31,150 na kompyuta 1,150 katika takriban shule 623.

“Kwa mantiki hiyo, tunapokaa chini kuangalia namna tulivyofanikiwa, tunajisikia furaha tunapogundua kwamba zaidi ya wanafunzi 93,000 kote nchini wanakaa kwenye madawati yaliyotolewa na benki yao pendwa. Pia tumechangia maktaba. Tumejenga vyoo na majiko kwa baadhi ya shule kupitia mpango maalumu wa wafanyakazi kuwajibika kwa jamii (CSR Staff Initiative Program),” anasema Ruth Zaipuna, Mkurugenzi Mtendaji Mkuu wa NMB.

Wakati mamlaka zikijikita katika ujenzi wa vyumba vya madarasa ili kukabiliana na ongezeko la wanafunzi, NMB imekuwa ikitoa vifaa na kuezeka majengo ya taasisi za umma zaidi ya 369.

Kama ilivyo katika elimu, michango ya NMB katika sekta ya afya ni vifaa kama vya uchunguzi, vitanda vya kulaza wagonjwa, vitanda vya kujifungulia wajawazito na vifaa vya ujenzi, vyote vikilenga kuisaidia na kuipa nguvu serikali katika kuwezesha upatikanaji wa vifaa tiba na huduma bora za afya kote nchini.

Katika eneo la kukabiliana na majanga na madhara yake, NMB imekuwa mstari wa mbele kusaidia watu ambao wamekumbwa na majanga ya asili nchini. Mathalani, waathirika wa mafuriko yaliyotokea mwaka 2016 wilayani Hai, Kahama na Geita, waliwezeshwa kama ilivyokuwa kwa mikoa ya Iringa na Lindi mwaka huohuo.

Mwaka 2017, wakati Tanzania ilipokumbwa na janga la asili, lililowaacha maelfu ya Watanzania wakihitaji misaada, NMB iliwashika mikono waathirika hao, ikitumia jumla ya Sh milioni 90 kuwasaidia watu waliokumbwa na mafuriko Kilosa, mkoani Morogoro na wale waliokumbwa na kipindupindu Zanzibar, na janga la moto wilayani Mugumu, mkoani Mara.

888 Total Views 4 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!