Chanzo cha ugomvi kati ya Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla, na Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Profesa Adolf Mkenda, kimejulikana.

Desemba 31, mwaka jana Rais John Magufuli akiwa mapumzikoni katika Hifadhi ya Taifa ya Kisiwa cha Rubondo mkoani Geita aliwapa siku tano viongozi hao kupatana, vinginevyo angetengua uteuzi wao.

Uchunguzi uliofanywa na JAMHURI umebaini kuwa chanzo cha ugomvi huo ni matumizi mabaya ya fedha unaofanywa na Waziri Kigwangalla, kupitia ‘utangazaji utalii’.

Miongoni mwa hayo ni matumizi yasiyo sahihi ya mali zilizo chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii, zikiwamo ndege.

Katika matukio mawili ya hivi karibuni, waziri huyo ameagiza moja ya ndege za Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) imfuate msanii mmoja (jina tunalo) Kigoma ili ashiriki tamasha jijini Arusha.

Katika tukio la pili, Dk. Kigwangalla aliamuru ndege ya TANAPA imfuate mwanahabari mmoja jijini Dar es Salaam na kumpeleka Arusha, Rubondo, Katavi na baadaye akarejeshwa Arusha. Ndege hiyo ilitakiwa imchukue mwanahabari huyo saa 2 asubuhi katika Uwanja wa Julius Nyerere, lakini alitokea saa 9 alasiri huku ndege ikiendelea kumsubiri kwa muda wote huo.

Wageni wake, wakiwamo wasanii wakiwa katika majiji kama Arusha hulazwa katika hoteli za kifahari za kuanzia hadhi ya nyota nne. 

Chanzo cha habari kinasema Profesa Mkenda amekuwa haridhishwi na matumizi ya fedha hizo, na amekuwa akitaka taratibu zifuatwe ili kunusuru fedha za umma, lakini na yeye mwenyewe kama mtendaji mkuu na ofisa masuuli wa wizara abaki salama. 

Dk. Kigwangalla, kama alivyowahi kufanya aliyekuwa Waziri wa Maliasili na Utalii wa mwisho katika Awamu ya Nne, Lazaro Nyalandu, amekuwa akiagiza apewe fedha nyingi ili kuwalipa wasanii kwa kigezo cha kuwatumia kuhamasisha utalii ndani na nje ya nchi.

Kwa kigezo hicho amekuwa akitumia makundi ya wasanii kuzunguka huku na kule nchini kufanya shughuli hiyo. Wasanii hao huzuru hifadhi za taifa na pia hushiriki matamasha mbalimbali. 

Hivi karibuni alipeleka kundi la wasanii kukwea Mlima Kilimanjaro, lakini ni mmoja tu aliyefanikiwa kufika kileleni. Wengine, licha ya kushindwa, waliendelea kulipwa fedha kwa muda wote uliopangwa. 

Imeelezwa kwamba Waziri Kigwangalla amekuwa akiagiza apewe fedha kutoka katika taasisi kuu zilizo chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii. Taasisi hizo ni Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), Wakala wa Misitu Tanzania (TFS), Mamlaka ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro (NCAA), na Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA). Mapato ya taasisi hizo kwa mwaka ni takriban Sh bilioni 500.

“Kuna makundi ya wasanii yanapelekwa kwenye maeneo mbalimbali ya hifadhi, gharama zake ni kubwa. Waziri anadai gharama zibebwe na wizara, sawa; lakini kuwe na utaratibu, yeye hataki. Unakuta anaagiza zitolewe Sh milioni 170, zitolewe Sh milioni 80; mara zitolewe Sh milioni 100 na kadhalika. Hizi fedha ni nyingi na kwa maana hiyo lazima kuwe na utaratibu wa kifedha wa kuziomba na kuzitoa.

“Mbaya zaidi, fedha hizo hutakiwa zilipwe na wakuu wa taasisi kwa maelekezo ya waziri. Huo si utaratibu. Kule kwenye taasisi wakisema hawana mamlaka ya kufanya malipo bila maelekezo ya katibu mkuu, mgogoro huanzia hapo.

“Katibu Mkuu anapoambiwa anang’aka na kutaka fedha zisitolewe bila kufuata mfumo wa malipo kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu. Waziri akishajua katibu mkuu amekwamisha malipo kwa sababu hizo, basi ugomvi unalipuka,” kinasema chanzo chetu.

JAMHURI limeelezwa kuwa baada ya Waziri Kigwangalla kuona anakwamishwa na katibu mkuu, alianza kutumia utaratibu wa kumwagiza msaidizi wake kuwasiliana moja kwa moja na wakuu wa taasisi hizo ili wafanye malipo.

“Hilo nalo lilionekana kuwa ni ukiukwaji wa taratibu, kwa sababu msaidizi wa katibu hana mamlaka ya kuwasilisha maelekezo ya kufanyika malipo. Utoaji fedha za umma una taratibu zake,” kinasema chanzo chetu.  

Fedha zinazochotwa kutoka kwenye taasisi hizo zinatumika kugharimia usafiri, malazi na posho za wasanii. Hata hivyo, baadhi ya waliozungumza na JAMHURI wanasema kinachofanywa na Wizara ya Maliasili na Utalii katika kuwatumia wasanii kinavuka mipaka ya ‘utangazaji utalii’, badala yake kuna mkakati wa kisiasa kwa ajili ya siku zijazo. 

“Ninachoweza kukuhakikishia ni kuwa kuna mpango wa watu kuwania nafasi kubwa zaidi mwaka 2025, kwa hiyo kinachofanyika sasa ni kuwavuta wasanii ili wawe karibu nao kwa ajili ya mwaka 2025. Hili halina ubishi kwa sababu tumo humu tunajua mengi. Kinachofanywa sasa ni kujenga mtandao wa kuungwa mkono na ndiyo maana unaona wanaotumika hapa ni wasanii na watu wa online,” kinasema chanzo chetu na kuongeza:

“Angalia hata wajumbe wa bodi, baadhi yao wanateuliwa kwa sababu ni marafiki wa wakubwa wizarani.”

Mwanzoni mwa Desemba, mwaka jana wasanii saba walifanya ziara katika baadhi ya hifadhi kwa kile kilichoelezwa kuwa ni sehemu ya kujionea vivutio ili kuvitangaza, hivyo kuhamasisha wageni na wenyeji kutalii.

Ziara hiyo ilianzia katika Hifadhi ya Taifa ya Burigi – Chato na kuendelea hadi hifadhi za taifa za Ibanda – Kyerwa na Rumanyika – Karagwe. Kiongozi mkuu wa msafara alikuwa Dk. Kigwangalla mwenyewe. Wasanii wa muziki na maigizo (Bongo Movie) walioshiriki ni Steve Nyerere, Dude, Richie, Shilole, Ebitoke, Shetta na mwakilishi kutoka Muziki AT (Zanzibar).

Baadaye walizuru Hifadhi ya Taifa ya Rubondo. 

Rais Magufuli akizungumza na wahifadhi wa Rubondo, alisema: “Ninafahamu, watendaji wenu wa juu, Katibu Mkuu na Waziri kila siku wanagombana, ninawatazama taratibu na nilishampa kazi Katibu Mkuu Kiongozi awaite na awaeleze, lakini wasipobadilika nitawaondoa…Siwezi kuwa na watendaji ambao nimewateua mwenyewe halafu wanagombana, na kuna mambo mengi hayaendi. Katibu Mkuu hamheshimu waziri na waziri hataki kwenda na katibu mkuu, siwezi kuvumilia hilo.

“Leo nawaambia wajirekebishe na ikiwezekana wajirekebishe ndani ya siku tano, wawe wanasalimiana na wanazungumza, mimi ninafahamu, nina vyombo, ninajua nani hafai zaidi,” alisema Rais Magufuli. 

Baada ya kauli ya Rais Magufuli, Waziri Kigwangalla kupitia akaunti yake ya Twitter alisema: “Kazi ya urais ni ngumu sana. Tulioteuliwa na Mheshimiwa Rais kumsaidia utendaji/usimamizi wa maeneo mbalimbali hatupaswi kumuongezea Rais frustration nyingine zaidi. Sisi kwenye wizara yetu, baada ya kikao na Chief Secretary (Katibu Mkuu Kiongozi) tulimaliza tofauti zilizokuwepo na sasa hali ni shwari!”

Gazeti la JAMHURI limemtafuta Dk. Kigwangalla kwa njia zote za mawasiliano ili kupata maoni yake, lakini hakupokea simu wala kujibu maswali aliyoandikiwa. Katibu Mkuu, Profesa Mkenda, hakuwa tayari kuzungumza.

Wizara yenye vishawishi

Wizara ya Maliasili na Utalii inatajwa kuwa miongoni mwa wizara zenye vishawishi na fitina nyingi. Mara kadhaa viongozi wenye ‘roho nyepesi’ za kujipatia ukwasi wamekuwa hawadumu. Lakini pia wale wanaokuwa na ‘mioyo migumu’ ya kukataa kushiriki magenge ya ufisadi wamekuwa wakiandamwa kwa kuundiwa fitina ambazo hatimaye huwaondoa madarakani.

Kuanzia mwaka 2006, Wizara ya Maliasili na Utalii imeongozwa na mawaziri saba kwa vipindi vinane. Alianza Anthony Diallo, akafuata Profesa Jumanne Maghembe, Shamsa Mwangunga, Ezekiel Maige, Balozi Khamis Kagasheki, Lazaro Nyalandu, Jumanne Maghembe (mara ya pili) na sasa ni Dk. Hamis Kigwangalla. 

Kwa kipindi hicho makatibu wakuu waliopitia wizara hii ni Salehe Pamba, Blandina Nyoni, Dk. Ladslaus Komba, Maimuna Tarishi, Meja Jenerali Gaudence Milanzi, na sasa ni Profesa Mkenda.

Idara ya Wanyamapori inayotajwa kuwa yenye vishawishi vya kila aina, haikuwa nyuma kwenye pangua pangua za wakurugenzi wake.

Kuanzia mwaka 2016 idara hiyo imeongozwa na Emmanuel Severe, Erasmus Tarimo, Obeid Mbangwa, Profesa Alexander Songorwa, Paul Sarakikya, Herman Keraryo na sasa ni Dk. Maurus Msuha.

Kigwangalla kama Nyalandu

Nyalandu anayetajwa kuwa miongoni mwa mawaziri walioifaidi vilivyo Wizara ya Maliasili na Utalii, alifikia hatua ya kuwa na vyumba maalumu katika hoteli za kitalii katika majiji ya Dar es Salaam na Arusha vilivyolipiwa na taasisi za NCAA na TANAPA. Malipo hayo hayakuzingatia kama amelala, au la.

Ofisini kwake kwenye Jengo la Mpingo, alionekana kwa nadra; na hata alipotaka kuzungumza na waandishi wa habari, alitumia hoteli za kitalii ambazo malipo yake huanzia Sh milioni 3 kwa saa kadhaa. Alifanya hivyo ilhali wizarani kwake kukiwa na ukumbi wa kisasa wenye viyoyozi na huduma zote za kuendeshea mikutano. 

Mara kadhaa alitumia ndege za taasisi zilizo chini ya wizara yake kwa ajili ya shughuli binafsi zisizokuwa na uhusiano na kazi zake za ofisi. 

Kama Kigwangalla, alitumia wasanii kwenye shughuli mbalimbali, lakini nyuma ya mpango huo ikabainika kuwa kulikuwa na mkakati wa kuvuna fedha. Wakati fulani alilazimisha malipo ya Sh milioni 500 kutoka TANAPA kwa ajili ya kudhamini shindano la urembo. 

Miaka ya mwisho ya uongozi wake alisafiri na msanii wa filamu za Tanzania, Aunty Ezekiel Grayson, nchini Marekani na kukaa huko kwa siku 14 kwa gharama za Wizara ya Maliasili na Utalii.

Walikwenda huko kwa kile kilichoelezwa kuwa ni mapumziko, na wakati huo huo kumtumia kutangaza vivutio vya utalii ili kuvutia watalii wengi kuja nchini Tanzania.

Binti huyo wa mwanasoka mahiri wa zamani aliyechezea Simba na Yanga kwa nyakati tofauti, Ezekiel Grayson (Jujuman), alilithibitishia JAMHURI kwa kusema: “Nilikuwa Marekani na Nyalandu.”

Kiasi cha fedha kilichotumiwa kwenye utangazaji huo wa kitalii kilikuwa siri, lakini chanzo chetu cha habari kilisema: “Ni pesa ndefu (fedha nyingi), inawezekana zikafikia hata Sh milioni 100 au zaidi.” 

Nyalandu alikuwa nchini Marekani pamoja na msanii huyo ilhali Rais Jakaya Kikwete naye akiwa huko huko, lakini akiwa hana taarifa za uwepo wake. 

Hatua hiyo inatajwa kuwa ilimkasirisha Rais Kikwete, hasa kwa kuona Nyalandu amekuwa akienda Marekani karibu kila wiki, hivyo kuacha vikao vya Bunge Maalumu la Katiba. 

Aunty alikiri kuwapo Marekani kwa wiki mbili kuanzia Septemba 10, 2014, akitangaza shughuli za utalii zilizoandaliwa na vijimamboblog.spot. 

“Tulikuwa na Waziri Nyalandu na sehemu kubwa ya bajeti ya kutangaza utalii ilitolewa na serikali. Kwenye ile party (hafla) tulialikwa na waziri ili nasi tuelezee utalii wa nchi,” anasema Aunty.

Anaendelea kusema: “Baadaye tukasikia Rais Kikwete naye yupo Marekani na tukaenda kuungana naye kabla ya kurejea nchini. Tulirudi Tanzania Septemba 24.”

Msanii huyo alipoulizwa kama ana uhusiano wowote wa ‘kijamii’ na Waziri Nyalandu, aling’aka na kusema kilichompeleka ni shughuli za kutangaza utalii tu. 

Aunty anasema hakuwa msanii pekee aliyekwenda na Nyalandu huko ughaibuni: “Tulikuwa wasanii wawili, mimi na (anataja jina). Hebu ngoja, nitakutajia hoteli na ukumbi ambao tulikuwa tukitangazia utalii.” Jina la msanii huyo tunalihifadhi.

By Jamhuri