Hakimu wa Mahakama ya Wilaya ya Iringa, John Mpitanjia anayeendesha kesi inayomkabili Mwanafunzi wa Chuo Kikuu Dar es Salaam (UDSM), Abdul Nondo amekataa kujitoa katika kesi hiyo kwa maelezo kuwa, ushahidi wa mtuhumiwa anayetaka ajitoe haujajitosheleza.

Katika maombi ya msingi, Mei 15, 2018 Nondo aliiandikia barua Mahakama hiyo akitaka hakimu anayesikiliza shauri lake, ajotoe kwani anamtilia shaka na na hana imani naye.

Akitoa maamuzi ya maombi hayo Mei 16, 2018 Hakimu Mpitanjia amesema mahakama ni chombo cha mwisho cha kutenda haki hivyo
itaangalia usawa kwa pande zote mbili ikiwa ni sambamba na kutoa haki kwa wakati bila kufungamana na upande wowote.

Baada ya kutoa muamuzi huo hakimu aliamuru upande wa jamuhuri kuendelea kutoa ushahidi wa mashahidi waliobaki katika kesi hiyo.

Katika kesi ya msingi, Nondo anakabiliwa na mashtaka mawili ambapo, shtaka la kwanza ni kuchapisha taarifa za uongo mtandaoni Machi 7, 2018 akiwa eneo la Ubungo Dar es Salaam na kuzisambaza kupitia mtandao wa kijamii wa Whatsapp kwamba yupo hatarini.

Katika shtaka la pili, wakili huyo amesema Nondo ametoa taarifa za uongo kwa mtumishi wa umma Mafinga alipokuwa anatoa taarifa kwa askari kwenye Kituo cha Polisi Mafinga kwa kusema kuwa alitekwa na watu wasiojulikana Dar es Salaam na kupelekwa kiwanda cha Pareto Mafinga.

Baada ya kusomewa mashtaka hayo, mtuhumiwa alikana.

By Jamhuri