Nondo feki zazua balaa Siha

Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Tanzania (Takukuru) imeanza uchunguzi kuhusu tuhuma zinazoikabili kampuni moja ya uuzaji wa vifaa vya ujenzi mkoani Kilimanjaro, inayodaiwa kuiuzia serikali nondo feki zisizo na ubora.

Kampuni hiyo ambayo kwa sasa jina lake tunalihifadhi baada ya mkurugenzi wake kutopatikana, ilishinda zabuni ya kuuza nondo kwa ajili ya ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Siha lakini baada ya Kamati ya Ulinzi na Usalama ya mkoa kubaini udhaifu wa nondo hizo ilisimamisha ujenzi kwa muda.

Baada ya ujenzi huo kusimamishwa, zilichukuliwa sampuli za nondo hizo na kupelekwa kwa wataalamu wa ubora na baadaye kubainika kuwa hazikuwa na ubora unaostahili hivyo serikali kusitisha kandarasi hiyo.

Mbali na nondo hizo, vilevile matofali yaliyotumika katika ujenzi huo yamebainika kutokuwa na ubora na kuondolewa eneo la mradi kupisha uchunguzi.

Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari, Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Kilimanjaro, Holle Makungu, amesema baada ya kubainika kwa upungufu huo iliamuliwa nondo na matofali hayo kuondolewa eneo la mradi na wazabuni kutakiwa kurejesha fedha walizopewa na serikali.

Makungu amebainisha hayo wakati akitoa taarifa ya utelekezaji wa majukumu ya taasisi hiyo katika kipindi cha miezi mitatu kuanzia Januari hadi Machi mwaka huu, iliyojikita katika mambo kadhaa, ikiwamo uendeshaji wa mashauri, uchunguzi, miradi ya maendeleo na udhibiti wa haraka.

Aidha, Takukuru imeagiza wazabuni hao waliohusika na udanganyifu huo wa kuiuzia serikali nondo na matofali yasiyokuwa na ubora wasipewe zabuni hiyo tena na Halmashauri ya Wilaya ya Siha.

Takukuru pia imemwondoa katika usimamizi wa ujenzi huo mhandisi aliyekuwa akisimamia mradi huo na imeanzisha uchunguzi dhidi yake, akihusishwa na makosa ya uhujumu uchumi pamoja na wote waliohusika katika kadhia hiyo, wakiwamo wazabuni hao.

Ujenzi wa hospitali hiyo ya wilaya unahusisha majengo sita likiwamo la utawala, jengo la mionzi, duka la dawa, jengo la kufulia nguo, jengo la kuhifadhi maiti pamoja na jengo la huduma ya mama na mtoto. Tayari serikali imekwisha kutoa Sh bilioni 1.5 kwa ajili ya ujenzi huo.

Makungu katika taarifa yake amezitaka mamlaka za umma zinazohusika na ununuzi wa kiwango kikubwa cha fedha, na idara zote za serikali kutoa taarifa kwa PPRA kuhusu makandarasi na wazabuni  wasiotekeleza miradi kwa mujibu wa mikataba kuondolewa kwenye kundi la wazabuni wanaoruhusiwa kufanya kazi na serikali.

“Utaratibu wa kutoa taarifa PPRA kwa makandarasi wanaopoteza sifa kutokana na ulaghai katika zabuni na utoaji wa huduma ndani ya muda mfupi utawezesha kuwa na makandarasi waadilifu na utaiwezesha serikali kuwa na uhakika wa miradi inayotekelezwa kwa ubora,” amesema.

Kwa upande mwingine, Takukuru ilifuatilia malalamiko ya wananchi juu ya watumishi wasiokuwa waaminifu wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), ambao wanadaiwa kuwashinikiza wananchi wasiokuwa na vyeti vya kuzaliwa kupeleka viapo.

Katika taarifa yake, Makungu amesema kuwa watumishi hao wamekuwa wakitoa masharti hayo kama kigezo cha kupata kitambulisho kisha kuwaelekeza kwa mawakili wasio waaminifu ambao huwajazia viapo hivyo bila hata ya kuwepo anayemuapisha na kisha kujipatia pesa ambazo hugawana na maofisa hao wa NIDA.

“Uchunguzi umeanzishwa dhidi ya wanaojihusisha na ulaghai huo na hatua za kisheria dhidi yao zitachukuliwa  kwa wote waliohusika, na nipende kuwafahamisha wananchi wa Mkoa wa Kilimanjaro kuwa hawahitaji kuwa na kiapo cha wakili kwa ajili ya vitambulisho vya taifa,” amesema.

Amefafanua kuwa NIDA makao makuu wanafahamu kuwa Watanzania wengi hawana vyeti vya kuzaliwa, hivyo waliandaa utaratibu mzuri wa kuhakikisha vitambulisho hivyo vinapatikana bure kwa kuandaa fomu maalumu ambazo zinapaswa kujazwa na viongozi wa serikali wa eneo ambalo mwombaji wa kitambulisho cha taifa anatoka.

Katika uchunguzi huo, Takukuru imefanikiwa kuwanasa maofisa wa NIDA Wilaya ya Moshi ili kusaidia uchunguzi kutokana na baadhi ya vitambulisho vya taifa kuwa mikononi mwa matapeli wasio watumishi wa mamlaka hiyo ambao wamekuwa wakijipatia pesa isivyo halali.

Makungu amesema katika taarifa yake kuwa Aprili 9, mwaka huu walipokea taarifa kutoka kwa mwananchi mmoja akieleza kuwa anadaiwa rushwa ya Sh 100,000 na ofisa wa NIDA ili apewe kitambulisho chake kinyume cha Kifungu cha 15 cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa ya mwaka 2007.

Amesema mtego uliandaliwa na makachero wa Takukuru na kufanikiwa kumtia mbaroni Hemed Adinan anayedaiwa kujitambulisha kama ofisa wa NIDA na baada ya upekuzi alikutwa na vitambulisho vingine vya NIDA ambavyo havijawafikia walengwa.

“Uchunguzi unaonyesha kuwa Hemed Adinan ni mwalimu wa Shule ya Sekondari ya Kiusa iliyopo Manispaa ya Moshi, uchunguzi zaidi unaendelea ili kubaini watumishi wa NIDA wanaohusika kumpa vitambulisho hivyo,” amesema.

Kwa mujibu wa Makungu, kitendo hicho kinakiuka Kifungu cha 31 cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa na mara uchunguzi utakapokamilika hatua za kisheria zitachukuliwa kwa wote watakaobainika kujihusisha na uvunjaji huo wa sheria.