Nssf
Nssf

Shirika la Hifadhi ya Jamii (NSSF) limeanza utekelezaji wa maagizo ya Rais John Magufuli kwa kuhakiki waliokuwa wafanyakazi wa migodi na ajira za muda mfupi.

 Akizungumza mwishoni mwa wiki, Meneja Kiongozi wa Matekelezo (Chief Manager Compliance and Data Management), Cosmas Sasi, amesema mbali na NSSF kuendelea kulipa mafao mbalimbali kwa wanachama wake kwa wakati, imeanza kazi ya kuhakiki wafanyakazi waliokuwa na ajira za muda mfupi.

Amesema mfuko unaendelea kupokea na kuhakiki madai mbalimbali kutoka kwa wanachama ambao ajira zao zimekoma na walikuwa kwenye ajira za muda maalumu kwenye sekta mbalimbali kama vile madini, viwanda, ujenzi, kilimo na nyingine.

“Madai yote yanayothibitishwa kuwa ni halali baada ya kuhakikiwa, mwanachama atalipwa mafao yake,” amesema.

Hatua hii imekuja siku chache baada ya Rais Magufuli kutoa maelekezo katika mkutano kati ya viongozi wa vyama vya wafanyakazi, Mamlaka ya Usimamizi na Udhibiti wa Sekta ya Hifadhi ya Jamii, watendaji wakuu wa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii na Chama cha Waajiri uliofanyika Desemba 28, 2018 Ikulu, jijini Dar es Salaam.

Sasi amesema NSSF inaendelea kulipa mafao mbalimbali kwa wanachama wake kwa wakati.  Katika Mafao ya Uzeeni amesema takriban NSSF hulipa Sh bilioni 5 kila mwezi “kwa wastaafu wetu kuanzia Julai, 2018.”

Kwa pensheni ya mwezi Desemba, 2018 NSSF imelipa Sh bilioni 4.83 kwa wastaafu 18,631 waliokuwemo kwenye daftari la wastaafu. Kwa upande wa malimbikizo ya mafao hadi kufikia Julai, 2018  Sh bilioni 108 zilikuwa zinadaiwa kwenye shirika. Kati ya kiasi hicho shirika limelipa Sh bilioni 85 kwa wanachama waliokuwa na madai mbalimbali baada ya uhakiki kukamilika, kiasi kilichobaki cha Sh bilioni 23 kitalipwa baada ya uhakiki unaondelea kukamilika.

Meneja Kiongozi Uhusiano na Elimu kwa Umma (Chief Manager Public Relations and Education), Lulu Mengele, amesema mfuko ulianza kuhakiki wastaafu wake Desemba 1, 2018 na uhakiki unaendelea kwenye ofisi mbalimbali za NSSF zilizoko mikoa yote ya Tanzania Bara.

“Wastaafu ambao hawajajitokeza kuhakiki wanaombwa wafike kwenye ofisi zetu 65 zilizoko katika maeneo mbalimbali katika mikoa yote Tanzania Bara. Kwa upande wa wastaafu wanaoishi Zanzibar watahakikiwa kwenye ofisi za ZSSF. Wastaafu wanatakiwa kuwa na picha, Kitambulisho cha Taifa au cha Mpiga Kura na kadi ya benki.

“Malipo ya pensheni kwa wastaafu ambao hawatahakikiwa yatasitishwa mwishoni mwa mwezi  wa Januari, 2019. Malipo ya wastaafu yatafanyika moja kwa moja kwenye akaunti za wastaafu ili kumrahisishia mstaafu kupata malipo yake ya pensheni kwa haraka na bila usumbufu. Zoezi la uhakiki litakuwa endelevu ili kuboresha taarifa zilizokuwepo kwenye daftari la wastaafu.

“Shirika linasisitiza kwa wafanyakazi na maofisa utumishi kuhakikisha madai yanayoletwa kwenye mfuko ni sahihi na mtu atakayebainika kuleta madai ya kughushi atachukuliwa hatua za kisheria ikiwemo kupelekwa mahakamani kwani hilo ni kosa la jinai,” amesema Lulu.

By Jamhuri