bodi ya misitu*Atumia mamilioni kugharimia viongozi 54 wa kidini
*Awalaza hoteli ghali, awalipa Sh 660,000 kwa siku
*Mpango mzima umelenga mbio za urais mwaka huu
 
Na Mwandishi Wetu

Siku kadhaa baada ya Sheikh Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhadi Mussa Salum, kujitokeza kumtetea Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu, kwenye vyombo vya habari, umepatikana ushahidi wa kiektroniki ukiwaonesha wawili hao wakiwa katika Hoteli ya Serena jijini Dar es Salaam.
  Kwenye ushahidi huo, anaonekana Sheikh Salum akiwa amevaa koti na kanzu yenye rangi ya njano iliyofifia pamoja na mtu mwingine aliyevaa kaunda suti. Mtu huyo hakujulikana mara moja, lakini inaaminika kuwa ni mmoja wa wasaidizi wake wa karibu. Tukio hilo lilitokea alasiri ya Machi 17, mwaka huu.
Baada ya kuingia Serena, walikwenda moja kwa moja kuketi bustanini. Wanaonekana wakihudumiwa juisi yenye rangi iliyoshabihiana na ya matikiti maji.


Mkanda huo unaonesha kuwa baada ya dakika takribani 20, Waziri Nyalandu aliwafuata na kuketi nao kwa dakika kadhaa kisha akaondoka kwenda katika duka la kubadilishia fedha ndani ya hoteli hiyo.
  Uchunguzi unaonesha kuwa Nyalandu alirejea dukani hapo mara mbili kisha akaingia duka jingine ambako baadaye alionekana akitoka akiwa ameshika bahasha kubwa.


 Alikwenda moja kwa moja kumkabidhi Sheikh Salum bahasha hiyo ambayo haijulikani ilikuwa ina ujumbe gani. Sheikh Salum aliipokea na kuiweka katika mfuko wa ndani wa koti lake.
Siku mbili baadaye, Sheikh Salum alijitokeza kwenye vyombo vya habari akimtetea Nyalandu na kumshutumu Kinana akisema kwamba lawama zake kwa Waziri huyo aliyemwita mchapakazi hodari, ni za kumkatisha tamaa.
 Kwa upande wake, Sheikh Salum amezungumza na JAMHURI na kusema hakumbuki lini alikwenda katika Hoteli ya Serena.


“Sikumbuki nilikwenda lini, sikumbuki kama nilishakutana na Waziri Nyalandu,” amesema.
 Utetezi wa Sheikh Salum kwa Nyalandu umekuja baada ya Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Abdulrahman Kinana, kumtuhumu Waziri huyo kwa utendaji kazi usioridhisha.
Katibu Mkuu wa Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA), Sheikh Suleiman Lolila, ameulizwa kuhusu kauli ya Sheikh Salum dhidi ya Kinana na kusema: “Bado nipo huku Rufiji, nikishapata hizo taarifa nitakuwa kwenye nafasi ya kulizungumza hili jambo.”
Kwenye ziara zake mikoani, Kinana amekuwa akikutana na malalamiko ya wananchi yanayohusu Wizara ya Maliasili na Utalii. Anamtuhumu Nyalandu kwa kushindwa kwenda kutatua migogoro hiyo, badala yake anasema Waziri amekuwa akizurura na kushindia katika hoteli za kitalii.


Inaelezwa kwamba kuna migogoro ya aina hiyo katika wilaya 52 za Tanzania Bara; na kwamba hakuna hata mgogoro mmoja ambao Nyalandu ameutatua. Pamoja na Kinana, wengine waliojitokeza hadharani kumsema Nyalandu kwa utendaji kazi hafifu ni Mbunge wa Ismani na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi. Waziri huyo anasema wananchi wa Isimani wamemwandikia barua sita ambazo zote hajazijibu.
  Ushirika wa Nyalandu na Sheikh Salum unatajwa kuwa ni mwendelezo wa Waziri huyo wa kuhakikisha anajiimarisha katika ‘kila idara’. Tayari ameshakuwa rafiki mkuu wa Msemaji Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Peter Msigwa; na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira, James Lembeli.
Nyalandu na matumizi ya viongozi wa kidini
Hivi karibuni, Sheikh Salum alikuwa miongoni mwa viongozi wa madhehebu ya Kiislamu na Kikristo waliogharimiwa na Nyalandu kwa safari ya siku mbili katika Hifadhi ya Taifa ya Tarangire.


 Habari za uhakika zinasema Nyalandu na Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii walihakikisha zinapatikana shilingi zaidi ya milioni 150 za kugharimia sehemu ya ziara hiyo. Kiasi cha fedha kilitoka Mamlaka ya Hifadhi za Taifa (TANAPA) kwa amri ya viongozi wakuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii. Kiasi hicho cha fedha ni tofauti na kingine kilichotolewa na taasisi na wadau wengine kwa maelekezo ya Nyalandu.
  Tangu Februari, mwaka jana TANAPA haina Bodi, hali inayomfanya Nyalandu amtumie Katibu Mkuu, Dk. Adelhelm Meru, kwa ajili ya uchotwaji fedha kutoka Mamlaka hiyo.
  Kwa mujibu wa Nyalandu, maudhui ya ziara hiyo ni kuwapa ‘somo’ viongozi hao wa kiroho ili waweze kushiriki vilivyo kwenye mapambano dhidi ya ujangili.


  Hata hivyo, watu walio karibu na Nyalandu wanasema ziara hiyo iliandaliwa kimkakati na Waziri huyo, ili kutafuta kuungwa mkono na viongozi hao kwenye safari yake ya kuwania urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Viongozi wa Kanisa Katoliki hawakuitikia mwaliko huo. Baadhi yao ni Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Eusebius Nzigilwa, na Padri Christian Likoleo ambao walikuwa miongoni mwa waalikwa.
 Nyalandu alihakikisha wageni wake wanaandaliwa usafiri wa ndege wa Dar es Salaam-Arusha-Dar es Salaam. Alihakikisha wanapata malazi kwenye hoteli ya hadhi ya nyota nne na tano katika hoteli ghali ya Sopa Lodge. Mjini Arusha, walilazwa na kupewa huduma zote za kibinadamu katika hoteli zenye hadhi.
Kadhalika, Nyalandu alihakikisha viongozi hao wa kiroho, kila mmoja anasaini Sh 660,000 kwa kila siku, kwa siku zote walizokuwa huko kama fedha za kujikimu.


  “Huu ni mwaka wa Uchaguzi Mkuu, makundi yanayotaka urais ndiyo hivyo tayari yameanza kuwakamata viongozi wa dini hasa madhehebu haya yanayojiita ya kiroho na baadhi ya viongozi wa dini ya Kiislamu.
 “Hawa wameletwa ili wamuunge mkono mgombea urais, na kila mmoja atakuwa ana bei yake…hawawezi kulipwa sawa kwani inategemea mvuto na ushawishi wa kiongozi mhusika,” amesema mtoa taarifa wetu.
Akizungumza katika hafla ya chakula cha usiku pamoja na viongozi hao katika Hoteli ya Sopa Tarangire, Nyalandu alisema ziara hiyo haina maslahi ya kisiasa kwa mtu wala chama chochote.
“Ziara hii haina faida ya kisiasa kwa chama chochote, kazi ya kulinda wanyama haiwezekani kufanywa na Serikali pekee, tuwalinde wanyama wetu kwa pamoja,” akasema.

2174 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!