LINDI
Na Aziza Nangwa
Mganga Mkuu wa Hospitali ya St. Walburg’s Nyangao, Dk. Masanja Kasoga, anaiomba serikali na wadau kuwawezesha na kuongeza madaktari bingwa wa mifupa, ubongo na mishipa ya fahamu kutoka Taasisi ya Mifupa Muhimbili (MOI).
Uongozi wa hospitali hiyo uliamua kupeleka huduma za kibingwa za upasuaji mifupa baada ya kuona kuna changamoto kubwa kutokana na ajali za pikipiki na mamba.
Kabla ya kuanza huduma za kibingwa za mifupa, uongozi wa hospitali hiyo uliingia mkataba na MOI ili kuwasaidia wagonjwa wa mifupa huku lengo likiwa ni kuwasaidia wananchi wa mkoa huo badala ya kwenda Dar es Salaam kutibiwa.
Akizungumza mjini hapa hivi karibuni na Gazeti la JAMHURI, Dk. Kasoga, anasema ushirikiano wao na MOI una mafanikio makubwa katika kutatua changamoto za matibabu ya wagonjwa wanaohitaji huduma ya kutibiwa hospitalini hapo.
“Tunafurahia sana ushirikiano uliopo kati yetu na MOI lakini bado tuna chngamoto ya uwezeshaji wa kupata wataalamu zaidi kutoka kwao na vifaa vya kutosha,” anasema.
Vilevile anasema uwepo wa madaktari bingwa katika maeneo hayo utawasaidia wananchi wa Lindi kupunguza hatari ya vifo na rufaa kwenda MOI.
“Kwa sasa MOI wamekuwa na msaada mkubwa katika eneo la madaktari wa mifupa kwa tiba dawa na mazoezi, wanafanya hivyo kila siku kwa kuwatumia madaktari bingwa,” anasema.
Pia anasema kwa sasa hospitali hiyo ina upungufu wa madaktari 16, waliopo wanane ni wa kawaida na mabingwa ni 12 lakini bado wamefanya jitihada za kuhakikisha wanapata wengine bingwa kwa kuongeza ufanisi wa utoaji huduma kwa kuwasomesha wawili katika vyuo mbalimbali.
Anasema kwa hali ilivyo wangependa pia kupatiwa madaktari wa moyo kwa sababu asilimia 25 ya wagonjwa wanaotibiwa hospitalini hapo wanakutwa na tatizo la ugonjwa huo.
Kuhusu mikakati yao, anasema kwa sasa ni kuomba serikali na wadau kutatua changamoto za watumishi, vifaa, jengo la chumba cha wagonjwa walio katika uangalizi maalumu (ICU), jengo la dharura, huduma ya hewa tiba (oksjeni) na nyumba za watumishi.
JAMHURI limepata nafasi ya kutembelea hospitali hiyo kujionea namna gani huduma za kibingwa za mifupa zinavyosaidia wananchi kutatua changamoto za magonjwa ya mifupa.
Naye Ofisa Utawala wa hospitali hiyo, Charles Laizer, anasema wazo la kupeleka huduma za kibingwa lilitolewa na uongozi wa hospitali baada ya kuona kuna changamoto kubwa ya rufaa kwa wagonjwa wa mifupa.
Anasema wagonjwa wengi waliokuwa wakifika hospitalini hapo kutibiwa walikuwa wamevunjika vibaya kwa ajali na walihitaji huduma za haraka za upasuji wa mifupa.
“Wagonjwa wengi wanaoletwa hapa kwetu wanakuwa wamepata ajali za pikipiki au kujeruhiwa na mamba, tulikuwa tunawaandikia rufaa ya kwenda kutibiwa MOI kwa sababu hatuna wataalamu hao,” anasema.
Laizer anasema kabla ya kupeleka huduma hizo uongozi wa hospitali ulipitia lengo la serikali linavyohitaji katika sekta ya afya la kufikisha matibabu ya kibingwa pembezoni, hasa vijijini ziwe karibu na wananchi.
Anasema baada ya kupitia lengo hilo ndipo wakaamua kushirikiana na MOI ili kuwasaidia wagonjwa na kupunguza rufaa.
“Kabla ya kuanza kazi ya upasuaji mwaka 2019 Mkurugenzi Mtendaji wa MOI, Dk. Respicious Boniface, alituma timu ya wataalamu kuja kuangalia mazingira ya hospitali kama miundombinu na vifaa vya kisasa vinavyohitajika viko salama ndipo walipoanza kazi na sisi,” anasema.
Laizer anasema kuwapo kwa huduma za MOI ni msaada mkubwa kwa serikali na wananchi kwa sababu imepunguza msongamano wa kupeleka wagonjwa, kwa kuwa kundi kubwa la waathirika ni watu wa hali ya chini na ndio watumiaji wa usafiri wa pikipiki.
“Huduma zinazotolewa za kibingwa zimeweza kutekeleza ilani ya CCM inayotaka huduma za afya ni kuhakikisha maisha ya Watanzania wengi wenye vipato vya kawaida yameokolewa kutokana na kuimarishwa kwa utoaji wa huduma za matibabu ya kibingwa hapa nchini,” anasema.
Laizer anasema baada ya mpango huo kuanza walifanikiwa kuwavuta wadau mbalimbali kutoka nje ya nchi kwa kushirikiana na wa ndani kuwawezesha vifaa vya kisasa, ukarabati wa jengo la upasuaji na nyumba za watumishi.
Pia anasema hospitali hiyo kwa sasa imekuwa mkombozi kwa mikoa ya Mtwara, Ruvuma, Dar es Salaam na Msumbiji kwa kuwa wagonjwa wa matatizo ya mifupa wanapenda kutibiwa hapo kwa sababu ya ubora wa huduma.
Kwa upande wake, Muuguzi Kiongozi wa hospitali hiyo, Faraja Kilewa, anasema majukumu yake ni kuhakikisha wagonjwa waliofika kupata matibabu katika hospitali hiyo wanapata huduma stahiki kutoka kwa madaktari na wauguzi.
Anasema kazi yake nyingine ni kuhakikisha wauguzi wanapata mafunzo ya mara kwa mara ili kuwawezesha kutoa huduma nzuri kwa wagonjwa, ikiwamo kuwakumbusha viapo vyao.
Kwa upande wake, Dk. Kulwa Joseph, kutoka MOI, anasema kazi ya kwenda kufanya upasuji kwa wagonjwa wa mifupa ilianza mwaka 2019 baada ya hospitali hiyo kupeleka pendekezo kwao la kutaka huduma zao ziwepo Lindi.
Dk. Joseph anasema amekuwa akipokea wagonjwa wenye matatizo ya mifupa kutokana na changamoto ya ajali za bodaboda na kujeruhiwa na mamba kutokana na msimu wa mavuno na kuanguka katika miti.
“Kwa kweli wagonjwa wanaoathirika katika kadhia hii ni watu wa hali ya chini, ni vema serikali ikabuni mikakati mbadala ya kuwafanya wawe salama hasa katika mto huo wenye mamba wengi,” anasema.
Katika hatua nyingine, Dk. Boniface anasema MOI imekuwa mkombozi kwa kupunguza rufaa kwa wagonjwa wa mifupa kutoka Kanda ya Kusini baada ya kila wiki kuwapelekea huduma huko huko.
Anasema huduma za kibingwa zilianzishwa katika hospitali hiyo na Hospitali ya St. Benedict Ndanda Mtwara kwa lengo la kupunguza rufaa na vifo kwa wananchi tofauti na miaka ya nyuma wagonjwa walikosa huduma hizo kwa haraka.
Anasema mpango wa kusogeza huduma katika Hospitali ya St. Walburg’s Nyangao ni moja ya mikakati yao katika kuongeza matibabu ya kibingwa ya mifupa katika Kanda ya Kusini na ndiyo maana walipopelekewa ombi walilikubali.
“Tangu tuanze huduma za kibingwa za mifupa katika Kanda ya Kusini tumeweza kupunguza msongamano wa wagonjwa kuja MOI lakini pia madaktari wetu wameweza kuwajengea uwezo wenzao wa Nyangao,” anasema.
Dk. Boniface anasema huduma za kibingwa wanazozitoa kwa kushirikiana na madaktari wa Lindi zimekuwa mkombozi kwa wananchi wa hali za chini waliokuwa wakishindwa kumudu gharama za kwenda MOI.
Pia anasema wamekuwa wakitoa madaktari bingwa kila wiki wakibadilishana kwa ajili ya kwenda kuwajengea uwezo madaktari na wauguzi wa Nyangao ili baada ya muda waweze kutoa huduma hizo bila kuwategemea madaktari wa MOI.
“Lengo la taasisi ni kupanua huduma za kibingwa za mifupa katika kanda zote ili madaktari waliopo katika maeneo hayo waweze kufanya tiba za kibingwa katika maeneo yao badala ya kuwapa wagonjwa rufaa,” anasema.
Vilevile anasema mpango huu ni kuwaondolea gharama kubwa wagonjwa wanaohitaji matibabu ya kibingwa katika hospitali hizo na ndiyo maana wameridhia kutoa madaktari bingwa kwenda hospitali za Kanda ya Kusini kufanya tiba za kibingwa za mifupa.
Anasema lengo la MOI kusogeza huduma za kibingwa ni kuipunguzia serikali gharama za kupeleka wagonjwa nje ya nchi kupata matibabu ya mifupa.
Anasema kwa sasa MOI inaona umuhimu wa kuwapatia elimu ya kuwajengea uwezo na mafunzo ya kutosha madaktari na wauguzi wa kanda katika baadhi ya mikoa kama ilivyo kwa Lindi ili iwe rahisi kwao kuwakusanya wagonjwa na kuwapatia tiba za mifupa huko huko.
Anasema wagonjwa wengi wanaokwenda kutibiwa katika taasisi yao ni wale wenye matatizo ya kichwa, nyonga, mishipa ya fahamu na migongo.
Katika hatua nyingine, anasema wana mikakati ya kuongeza wataalamu zaidi katika vitengo vya kichwa na migongo kila wiki kwenda mikoani kutoa huduma za kibingwa kama kutakuwa na uwezeshaji wa kutosha.