Na Mwandishi Wetu,JamhuriMedia

Mabingwa Watetezi wa Ligi Kuu Soka Tanzania Bara, na Michuano ya ASFC, Young Africans SC wamethibitisha kuwa wataweka kambi ya maandalizi ya msimu ujao wa mashindano jijini Dar es Salaam katika hosteli za Avic Town, Kigamboni.

Akizungumza jijini Dar es Salaam katika Mkutano na Waandishi wa Habari, Msemaji wa Klabu hiyo, Haji Sunday Manara amesema wamechelewa kurejea kufanya maandalizi ya msimu ujao kutokana na kuwapa muda wa mapumziko Wachezaji wao ambao walikuwa na msimu mrefu wa mashindano wa 2021-2022.

“Uongozi na Benchi la Ufundi ulitoa muda wa mapumziko kwa wachezaji wote, ukiangalia wengine wanatoka mbali, kusafiri peke yake ni muda wa siku mbili, mfano kama Golikipa Djigui Diarra anayeenda nchini Mali hadi kufika Bamako ni safari ndefu”, amesema Manara.

“Lakini tuliwapa ‘Program’ kuweke miili yao ‘fit’ kwa ajili ya kujiandaa na msimu unaokuja ii wakajiandae wakirudi warudi wawe vizuri kwa ajili ya msimu ujao wa mashindano wa 2022-2023”, ameeleza Manara.

Pia, Manara amesema wana jumla ya wachezaji 14 wa kigeni licha ya kanuni za kuwa na wachezaji wa kigeni kutaka kuwa na wachezaji 12 pekee, amesema wanamrudisha mchezaji Chiko Ushindi kwenye klabu yake ya zamani ya TP Mazembe ya DR Congo ambapo walimchukua kwa makubaliano maalum.

Aidha, amethibitisha kuwa wachezaji wa timu hiyo, watakaporejea kambini watakaa meza moja na mshambuliaji Yacouba Sogne ambaye anasumbuliwa na majeraha muda mrefu na bado hajawa ‘fit’ asilimia 100.

Hata hivyo, wamethibitisha kuwaacha wachezaji wao wa ndani, ambao ni Deus Kaseke, Yassin Mustapha, Balama Mapinduzi na Paul Godfrey (Boxer) huku wakithibitisha kuwasajili wachezaji watano wa kigeni ambao ni Joyce Lomalisa Mutambala, Bernard Morrison, Stephane Aziz Ki na Lazarous Kambole.

Kuhusu, Siku ya Mwananchi, Yanga SC wamesema wataanza maandalizi ya Wiki hiyo Agosti Mosi mwaka huu huku kilele cha Wiki hiyo kikiwa Agosti 8 kwa matukio mbalimbali likiwemo tukio la kutambulisha Wachezaji ambao wataitumikia Klabu hiyo msimu ujao wa mashindano. “Kwenye kilele cha wiki ya Mwananchi tunacheza na mabingwa wenzatu, tutawataja baadae”, amesema.

By Jamhuri