Na Immaculate Makilika, MAELEZO
Miaka 27 baada ya kifo cha Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, Kiswahili kinaendelea kupanua wigo wake duniani.
Kutoka lugha iliyotumika kuunganisha Watanganyika katika harakati za kudai uhuru, sasa kinatumika katika diplomasia, elimu na majukwaa ya kimataifa, huku kikifungua fursa mpya za kiuchumi.
Mchango wa Mwalimu Nyerere katika kukikuza Kiswahili umeendelea kuwa sehemu muhimu ya historia ya lugha hiyo. Kupitia matumizi yake katika harakati za kudai uhuru wa Tanganyika miaka ya 1950, aliweza kutumia lugha hiyo kuwaunganisha watu wa makabila mbalimbali, licha ya tofauti zao za lugha na tamaduni.
Akizungumza kuhusu mchango huo, mbobezi wa masuala ya sheria, mhadhiri na mwandishi wa vitabu, Profesa Abdallah Jumbe Safari, anasema Mwalimu Nyerere alikitumia Kiswahili kwa ufasaha katika harakati za ukombozi na kukifanya nyenzo ya kuhamasisha umoja wa kitaifa.
Profesa Safari anasema Mwalimu hakutegemea hotuba pekee, bali pia alitumia ushairi katika kuwasilisha ujumbe wa ukombozi. Anataja matumizi ya mashairi katika mijadala ya wakati huo, akiwahusisha Rais wa Kwanza wa Zanzibar, Hayati Sheikh Abeid Amani Karume, na mshairi maarufu Shaaban Robert.
Akifafanua dhana ya mshikamano katika mapambano ya ukombozi, Profesa Safari anatoa mfano wa shairi linalotumia picha ya kamba kukata jiwe, ambapo jiwe linafananishwa na mkoloni na kamba na wananchi walioungana kupinga utawala wa kikoloni.
Upendo wa Mwalimu Nyerere kwa Kiswahili ulionekana pia katika kazi zake za maandishi na tafsiri. Alitafsiri tamthilia za William Shakespeare, zikiwamo The Merchant of Venice na Julius Caesar, na kuandika vitabu vyake kwa Kiswahili, vikiwamo Tujisahihishe.
Jitihada hizo zilichangia kukipa Kiswahili nafasi kubwa katika elimu, uandishi na mijadala ya kijamii, sambamba na kukifanya kuwa nyenzo ya kuimarisha utambulisho wa taifa.
KWA HABARI ZA KINA ZAIDI SOMA GAZETI LA JAMHURI LA OKTOBA 20 -26, 2026


