Na: OWM–TAMISEMI, Dar es Salaam
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OWM–TAMISEMI), Mhe. Prof. Riziki Shemdoe, amesema Serikali imekuja na suluhu ya haraka ya kupunguza msongamano na kutatua kero za muda mrefu katika eneo la biashara la Kariakoo, kwa kuanza ujenzi wa soko jipya la wafanyabiashara wadogo wadogo (wamachinga) katika eneo la Kigogo Sambusa, litakalokamilika ndani ya miezi sita ijayo.
Akizungumza jijini Dar es Salaam, Oktoba 19, 2026, katika kikao cha pamoja na viongozi wa wafanyabiashara wa Kariakoo, Wamachinga na viongozi wa Mkoa wa Dar es Salaam, Prof. Shemdoe amesema hatua hiyo inalenga kutoa ahueni ya haraka kwa wafanyabiashara na kuboresha mazingira ya biashara Kariakoo, wakati Serikali ikiendelea na mipango ya kukamilisha mradi mkubwa wa soko la kudumu unaohusishwa na uendelezaji wa Bonde la Msimbazi.
“Lengo la Serikali ni kupunguza msongamano uliopo Kariakoo. Ujenzi wa tuta katika eneo la Kigogo Sambusa unaanza mara moja na ukikamilika, Halmashauri ya Jiji la Ilala itaanza ujenzi wa soko. Tunataka eneo hili liwe tayari ili Wamachinga waweze kuhamia na kufanya biashara zao kwa amani,” amesisitiza Prof. Shemdoe.
Prof. Shemdoe amesema mradi wa soko hilo utagharamiwa kupitia asilimia tano (5%) ya mapato ya ndani ya Halmashauri ya Jiji la Ilala, hivyo amemshukuru sana Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuridhia sheria ya kuruhusu mapato ya asilimia tano (5%) ya ndani yaliyolindwa yatumike kwa ajili ya uimarishaji wa miundombinu ya biashara ikiwemo ujenzi wa masoko.
Ili kuhakikisha mradi unakamilika kwa wakati, amewaelekeza Katibu Mkuu wa OWM–TAMISEMI, Katibu Tawala wa Mkoa wa Dar es Salaam (RAS) na Mkuu wa Wilaya ya Ilala kusimamia kikamilifu utekelezaji wake, huku akiahidi kurejea eneo hilo baada ya mwezi mmoja kukagua maendeleo ya ujenzi.
Aidha, Prof. Shemdoe amesisitiza kuwa wakati ujenzi wa soko hilo la wamachinga ukiendelea Kigogo Sambusa, suala la kuwapanga wamachinga katika Soko la Kariakoo litaendelea ili kariakoo iweze kupitika, hivyo amemuomba Mwenyekiti wa Wamachinga Soko la Kariakoo kuipa Serikali ushirikiano katika suala hilo.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa wafanyabiashara wa maduka ya Kariakoo, Bw. Severine Mushi, akizungumza kwa niaba ya wafanyabiashara wenzake, amepongeza jitihada za Serikali na kueleza kuwa wafanyabiashara wako tayari kuendelea kulipa kodi na kuchangia pato la Taifa, iwapo mazingira ya biashara yataboreshwa.
Naye, Mwenyekiti wa Wamachinga Soko la Kariakoo, jijini Dar es Salaam, Bw. Steven Lusinde, ameishukuru Serikali inayoongozwa na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuwezesha fursa za mikopo kwa wafanyabiashara wadogo, huku akiiomba Serikali kudhibiti urasimu na vitendo vya ujanja-ujanja katika ugawaji wa maeneo mapya ya biashara.
Kukamilika kwa soko hilo kunatarajiwa kupunguza msongamano Kariakoo, kuboresha mazingira ya biashara, kupunguza migogoro ya mara kwa mara kati ya wamiliki wa maduka na wafanyabiashara wa mtaani, pamoja na kuongeza makusanyo ya kodi kwa Serikali.










