KAMPALA

Na Mwandishi Maalumu

Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) inaitazama Uganda kama fursa muhimu ya kiuchumi kwa Tanzania kupitia huduma za bandari.

Akizungumza mjini hapa wiki iliyopita akiwa na maofisa waandamizi wa mamlaka hiyo waliokuwa katika msafara wa ziara ya siku mbili ya Rais Samia Suluhu Hassan nchini Uganda, Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Eric Hamissi, anasema ofisi hiyo ipo katika hatua za mwisho za kuanza kutoa huduma.

Hamissi anasema kuanzishwa kwa ofisi hiyo mpya kunakusudia kuongeza ushawishi wa matumizi ya bandari za Dar es Salaam na Mwanza katika kuhudumia shehena za Uganda, malighafi za viwandani na kuwezesha bidhaa zinazozalishwa nchini humo kufika katika masoko sehemu mbalimbali duniani.

Katika siku ya pili ya ziara yake Uganda, Rais Samia ametembelea makao makuu ya Kampuni ya Roofing Group inayoongoza kwa kuzalisha vifaa vya ujenzi nchini humo na kuwa na masoko katika nchi mbalimbali barani Afrika.

Kupitia ziara hiyo, Rais Samia anaelezea utayari wa Tanzania kushirikiana na taasisi za Uganda katika kukuza biashara baina ya nchi hizi mbili na kuikaribisha kampuni hiyo kufanya uwekezaji hapa nchini na kuahidi kuipa ushirikiano wa hali na mali ili Tanzania nayo inufaike na fursa zinazoambatana na uwekezaji huo.

Mwenyekiti Mtendaji wa Roofing Group, Dk. Sikander Lalani, ameishukuru Tanzania kwa kuwezesha biashara ya kampuni hiyo kufanyika kwa ufanisi kupitia huduma za bandari za Dar es Salaam na Mwanza; Shirika la Reli Tanzania TRC), Kampuni ya Huduma za Meli (MSCL) na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).

Pamoja na mambo mengine, Februari, 2022 Roofing Group na kampuni za uchukuzi za Tanzania zilisaini makubaliano ya kibiashara (SLA). 

Makubaliano hayo yanatajwa kuongeza kiwango cha shehena za Uganda zinazopita Tanzania kutoka asilimia mbili ya sasa hadi kufikia wastani wa asilimia 30.

Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa Masoko na Uhusiano wa TPA, Nicodemus Mushi, anasema kuwapo kwa ofisi hiyo kutawezesha huduma za bandari kupatikana kwa ukaribu zaidi nchini humo. 

“Kuwapo kwa ofisi mpya mjini Kampala kutatuongezea uwezo zaidi wa kuhudumia wateja wetu kutoka pale walipo nchini mwao, hivyo kurahisisha shughuli zote za kuhudumia shehena, iwe inaingia au inatoka Uganda kupitia bandari zetu nchini Tanzania,” anasema Mushi.

Vilevile anasema ufunguzi wa ofsi hiyo ni mwendelezo wa juhudi kubwa zinazofanywa na TPA kuimarisha matumizi ya bandari za Tanzania kwa nchi jirani ambazo hazina bandari.

Anasema kwa sasa tayari TPA ina ofisi katika majiji ya Kigalı nchini Rwanda, Bujumbura nchini Burundi, Lubumbashi nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na Lusaka nchini Zambia.

Anasema katika kuhakikisha ofisi hiyo mpya inafunguliwa, TPA inashirikiana kwa karibu na Balozi wa Tanzania nchini Uganda ambaye ni mtekelezaji mkuu wa dhana ya diplomasia ya kiuchumi ambayo jukumu lake kubwa ni kufanikisha biashara kati ya Tanzania na mataifa jirani.

“Mabalozi wetu katika nchi hizo shughuli zao nyingi zina uhusiano na shughuli za bandari na lojistiki. Wakati mabalozi wetu wanashughulika na diplomasia ya kiuchumi, sisi TPA tutakuwa tunajihusisha na usafirishaji, lojistiki na uwezeshaji biashara,” anasema Mushi.

Uamuzi wa kufungua ofisi mjini Kampala ni matokeo ya ziara ya siku tatu ya Rais Yoweri Museveni wa Uganda nchini Tanzania mwaka jana. Katika ziara hiyo, Rais Museveni alipata nafasi ya kutembelea Bandari ya Dar es Salaam.

Rais Samia na Rais Museveni wamekubaliana kuwapo kwa haja ya kufungua ofisi ya TPA Kampala ili kurahisisha usafirishaji wa mizigo kutoka bandari za Dar es Salaam, Tanga na Mwanza hasa kipindi hiki cha ujenzi wa bomba la mafuta ghafi kutoka Hoima nchini Uganda hadi Chongoleani mjini Tanga.

Katika hatua nyingine, Mushi, anasema uwapo wa TPA mjini Kampala unatarajiwa kuharakisha usafirishaji wa bidhaa na huduma zinazohitajika katika ujenzi wa bomba jipya la mafuta na utarahisisha gharama ya kufanya biashara kati ya Tanzania na Uganda huku Bandari ya Mwanza ikitumika kupitisha sukari ya Uganda kufikia masoko ya Tanzania na nchi nyingine jirani.

Pia katika kuhakikisha bandari za Ziwa Victoria zinawezeshwa kushindana kibiashara, anasema TPA imefanya ukarabati wa Bandari ya Mwanza Kusini ambayo ni maalumu kuhudumia meli za mizigo na Bandari ya Mwanza Kaskazini inayojihusisha na kusafirisha abiria.

Anasema maboresho hayo yamesababisha usafirishaji wa mizigo kutoka Dar es Salaam kwenda Uganda kupitia ukanda wa Kati wa Tanzania kuwa bora zaidi na kuwezesha kukua kwa biashara kati ya Tanzania, Uganda na Sudan Kusini.

Anasema maboresho ya Bandari ya Mwanza Kusini yalihusisha pia kufufua mfumo wa usafirishaji makasha hadi Port Bell nchini Uganda na maeneo mengine kwa kutumia vivuko vya mabehewa. 

Aidha, anasema njia ya kati ya reli kuanzia Bandari ya Dar es Salaam hadi Mwanza hadi Port Bell inaaminika kusafirishia shehena na ina gharama nafuu zaidi kuliko njia zote.

Anasema TPA inafanya kazi kwa karibu na TRC na MSCL kwa ajili ya kuweka mifumo bora ya usafirishaji wa mizigo kutoka ņa kuingia Uganda kupitia bandari za Tanzania.

“Msisitizo wa Serikali ya Awamu ya Sita ni kuongezeka kwa shehena ya mizigo ya Uganda inayopitia bandari zetu za Dar es Salaam, Tanga na Mwanza na tunatekeleza maagizo ya serikali na kuhakikisha tunaingia katika soko la Uganda,  hivyo kukuza uchumi,” anasema Mushi.

Pia anasema shehena ya Uganda kupitia Bandari ya Dar es Salaam iliongezeka hadi tani za metriki 191,282 mwaka 2020/2021 kutoka tani za metriki 140,269 zilizorekodiwa mwaka uliotangulia.

By Jamhuri