Miezi kadhaa nyuma nilikuwa safarini katika moja ya miji iliyopo Nyanda za Juu Kusini. Nilipofika stendi kuna kitu kimoja kilinivutia na nikaamua kukitafakari kwa umakini zaidi.

Hapo stendi nilikuta benki fulani ikiwa imeweka bango lao (mwavuli) sambamba na mabango ya makampuni ya simu yanayotoa huduma za fedha kwa simu (mobile banking). Ingawa hili la mabenki kuingia mtaani kwa ajili ya kutafuta wateja limekuwa ni jambo la kawaida siku hizi; watu wengi watakubaliana na mimi kwamba si kitu kilichokuwa kimezoeleka huko nyuma.

Hapo zamani benki zilijipambanua na kuonekana kana kwamba ni kwa ajili ya kundi fulani la wateule katika jamii. Kundi hili la wateule lilionekana ni la wale watu wenye fedha nyingi, wafanyabiashara, wasomi na wafanyakazi. Ingawa vianzio vya kufungua akaunti havikuwa vikubwa, lakini utamaduni wa kihuduma na mazingira ya benki vilijiweka katika hali ya kuwatenga sehemu kubwa ya wanajamii. Watu wengi waliamini kuwa unapoenda benki ni lazima uwe msafi na uwe katika haiba ya aina fulani.

Nadhani hata wahudumu wa mabenki nao waliamini kuwa benki si mahali pa kila mtu; hili ungeweza kulithibitisha namna ambavyo wangekupokea ikiwa ungeenda ukiwa umevaa kihohehahe. Nyakati hizo mtu aliona ni afadhali kuweka fedha zake chini ya godoro kuliko kupeleka benki. Ukiacha hilo la benki kuonekana kama za watu fulani, pia kulikuwa na changamoto kubwa sana ya foleni katika mabenki mengi. Kwenda benki ilikuwa ni kama utumwa hasa unapofikiria namna ambavyo utatumia muda mwingi wa hadi saa nne ukisubiri kuhudumiwa.

Kipindi ambacho mabenki yanatamba namna hii kulikuwa bado hakujaibuka hizi benki za simu. Ujio wa benki za kwenye simu zinazoendeshwa na makampuni ya simu yameyatingisha mabenki na bila shaka yameyaamsha kutoka usingizini. Ujio wa benki za simu umefanikisha kuwajumuisha wanajamii wengi ambao waliwekwa kando na utamaduni (usio rasmi) wa mabenki.

Nimepata kumsikia mkurugenzi wa benki moja kubwa nchini akieleza namna ambavyo benki za simu zilivyowapa changamoto hasa katika ukusanyaji wa akiba za wateja (deposits). Mkurugenzi huyo alitahadharisha kuwa kama hatua za makusudi zisipochukuliwa benki (yake na nyingine) zitajikuta kwamba hazina wateja wa kipato cha chini na cha kati.

Sababu kubwa ni kwamba wote wanaona kuwa benki za simu ndiyo rafiki kuliko utamaduni wa mabenki. Ninachopongeza kuhusu benki hiyo ni kwamba mkuu huyu alikuwa akiyasema haya wakati akitambulisha mikakati yao ya kushirikiana na makampuni haya ya simu pamoja na kuanza mbinu za kuwafuata wateja watarajiwa (potential customers) na waliopo huko huko mitaani.

Hadi sasa mabenki mengi yameshazinduka kutoka usingizini na yameendelea kufanya bidii katika kurekebisha matatizo ya foleni, kupunguza utamaduni hasi katika kuhudumia uliokuwa unawafanya watu wengi waogope kufika benki, pamoja na kuungana kihuduma na makampuni ya simu yenye kutoa huduma za kibenki. Unapoona benki zinaingia mitaani kutafuta wateja, hayo ni mapinduzi makubwa sana katika sekta ya fedha.

Pamoja na kwamba mabenki mengi yanaungana na makampuni haya (ya simu), changamoto inayoendelea kuwapo ni gharama kubwa za kuendesha huduma zenye muunganiko wa mabenki na makampuni ya simu. Mathalani, benki nyingi zinahamasisha uweke akiba kwa kupitia simu yako. Ninapoweka fedha katika simu yangu ninapotaka kuzipeleka katika akaunti yangu ninakatwa fedha.

Nitakapotaka kuchukua fedha hiyo nitakatwa gharama ya kuitoa kutoka akaunti ya benki kuja akaunti ya simu na nitakatwa tena ninapotaka kuitoa kutoka kwenye akaunti ya simu kuja mkononi. Wengi hujiuliza, kuna haja gani nikatwe mara tatu? Ndiyo maana watu wengi huamua kutunza fedha zao katika akaunti za simu zao. Kuna idadi kubwa sana ya watu ambao wametelekeza akaunti zao tangu ujio wa benki za simu.

Tumaini kubwa la watu kwa mabenki limebaki si katika kuweka akiba bali katika kupata mikopo. Katika hili la mikopo bado mabenki mengi yamebaki kuwa na taratibu ambazo si rafiki sana kwa wakopaji hasa wa uchumi wa chini. Bado mikopo katika mabenki imeendelea kupata sura ya kwamba ni kwa ajili ya wateule wachache katika jamii. Kama ilivyokuwa kwa matumizi ya benki, kuna kundi kubwa sana la jamii limetupwa nje linapokuja suala la mikopo.

Unapoomba mkopo benki; benki nyingi huwa zina urasimu ambao si rafiki sana kwa biashara nyingi za Kitanzania. Zile taratibu za kukamilisha masharti ya mikopo mara nyingi huchukua muda mwingi kiasi kwamba mkopo unaweza kutolewa wakati ambao biashara uliyokuwa unaifukuzia imeshakupita. Fikiria kwamba unataka kulima mwezi wa kumi na moja, unajaza fomu unapeleka kila kitu na unaeleza na mpango wako wa biashara; halafu benki wanakuja kukupitishia mkopo mwezi Januari wakati msimu umeshaisha!

Huu ndiyo huwa mwanzo wa wafanyabiashara wengi kuanza kufikiria kutumia mikopo nje ya lengo kuu. Matokeo yake ni kuyumba kibiashara ama kushindwa kabisa kurejesha mkopo. Na hata kama ukifanikiwa unakuwa umefanikiwa katika uelekeo ambao hukuukusudia. Ukifuatilia taratibu na masharti ya benki utagundua kuwa benki nyingi ni marafiki wa matajiri ama tuseme marafiki wa watu ambao tayari wameshajikwambua. Benki nyingi hazipo tayari kukopesha fedha kwa biashara zinazoanza ila zina utayari mkubwa linapokuja suala la kukopesha biashara zinazoendelea.

Unapoambiwa na benki nenda kalete rekodi za kimahesabu maana yake wanakutaka ukalete maendeleo yako ya nyuma. Huwezi kupeleka rekodi ya maendeleo kama hujawahi kuwa na maendeleo. Unapoambiwa lete dhamana kwa ajili ya mkopo hii ina maana kuwa benki wanataka kukueleza hivi; “Hatukopeshi hohe hahe hata kama una wazo zuri, bali tunakopesha mwenye nacho ili ashindwapo kurejesha tusipoteze fedha zetu”

Natambua kuwa kuna mazingira na baadhi ya mabenki ambayo huwa yapo tayari kukopesha fedha kwa kutumia wazo peke yake. Hata hivyo wote mtakubaliana na mimi kwamba mazingira kama haya ni machache sana na hata benki zilizopo tayari kufanya hivyo ni chache mno. Unaposikia benki wamempa mtu fedha uwe na uhakika kwamba wametoa kwenye mkono wenye mchuzi, maana “mkono mtupu haulambwi”.

Mbali na urasimu wa upatikanaji mikopo lakini bado kumeendelea kuwapo na changamoto la riba kubwa ambazo wakati mwingine zinawakaba wafanyabiashara. Hili la riba sina ugomvi nalo sana kwa sababu  hadi unaamua kuchukua mkopo ina maana unakuwa umeshapiga hesabu ya urudishaji. Ni vema nieleweke kwamba hatuzihukumu benki kwa namna zinavyofanya kwa sababu wanachokiangalia ni uhakika wa fedha zao kurudi. Hakuna benki inayokopesha kwa urafiki usio na maslahi. Kazi ya benki ni kuzalisha fedha kwa kuuza fedha kupitia bidhaa mbalimbali ikiwamo hii mikopo ya aina mbalimbali.

Upo msemo wa Kiswahili usemao maji yanayotiririka ukiyabana ni lazima yatatafuta mkondo mwingine na yakishindwa yatabomoa ama kupasua ulipoyabania. Kutokana na utamaduni wa mabenki linapokuja suala la mikopo; hivi sasa mitaani kumeibuka mifumo mingi rasmi na isiyo rasmi inayomimina mikopo kwa watu wenye kiu ya kujikwamua kiuchumi. Kuna uwepo wa taasisi za ushirika Saccos, kuna taasisi binafsi zinazotoa mikopo, kuna vikundi vya Vicoba, lakini pia kuna watu ambao wanakopesha fedha kienyeji pasipo leseni wala vibali.

Katika hizo taasisi na watu wanaokopesha kienyeji, chenye riba ndogo kushinda mabenki mengi ni Vicoba na Saccos kwa sehemu fulani. Taasisi binafsi pamoja na watu binafsi wote wana riba kubwa na wakati mwingine za kutisha; kwa sababu wengi (hawa wanaokopesha) pia wanakopa katika mabenki.

Huu ujio wa Vicoba na mahali pengine watu wanaita “mchezo” na wengine wana majina tofauti tofauti, nao nikiutafakari ninaona unaweza kuyatingisha mabenki kama yasipopitia upya taratibu za mikopo hasa kwa watu wa hali za chini.

Siku hizi ni kawaida kukutana na vikundi ambavyo watu wanachangishana na kisha kukopeshana kwa riba kidogo sana ya hadi asilimia mbili tu. Kuna vikundi vingi tu katika maeneo mengi ambavyo mwanakikundi anaweza kukopa hadi milioni tano pasipo kuhitaji kuweka dhamana ama masharti makubwa yoyote. Kukopeshana laki tano, milioni moja ni kawaida sana kuanzia mitaani hadi kwa watu wa makazini.

Uwepo wa mitindo hii ya wananchi kujiunga na kufanya bidii za kukopeshana ni mzuri sana na kwa sisi wachumi tunasema ni uamsho wa kiuchumi! Kinachofanya niyape ole mabenki ni umuhimu wake katika uamsho huu wa kiuchumi. Bado mabenki yana nafasi kubwa sana katika kuamsha, kurekebisha na kupaisha uchumi wetu. Kama watu mtaani wanavumbua njia nzuri za kukopesha kwa utaratibu mzuri na kwa riba ndogo kwa nini mabenki yasifuatie mkondo huu?

Sekta ya fedha na suala la kujikomboa kiuchumi linakimbia kwa kasi mno duniani pote (zaidi sana katika Dunia ya Tatu), hivyo mabenki nayo yanatakiwa yawe kiongozi wa ubunifu na si kuburuzwa na bunifu kila wakati. Bado nina imani na tumaini kubwa kwa nafasi ya mabenki kwenye uchumi wetu na hasa mikopo, yaamke, yapitie upya taratibu za mikopo na riba zao.

[email protected], 0719 127 901

By Jamhuri