Home Michezo PIGO KWA WAKENYA, SPORTPESA YASITISHA UDHAMINI

PIGO KWA WAKENYA, SPORTPESA YASITISHA UDHAMINI

by Jamhuri

Kampuni ya mchezo wa kamari nchini Kenya, SportPesa, imesitisha udhamini wake wa michezo kutokana na uamuzi wa serikali kuongeza ushuru hadi asilimia 35 kutoka kwa asilimia 7.5.
Akizungumza na waandishi wa habari Jumanne, mkurugenzi mkuu na mwanzilishi wa SportPesa Ronald Karauri amesema wamelazimika kujiondoa kwa sababu hawawezi kudhamini michezo kama watatozwa ushuru wa asilimia 35.
Miongoni mwa michezo itakayoathiriwa na uamuzi wa SportPesa ni kandanda, ndondi na raga.
Kwa upande wa kandanda, kampuni hiyo hudhamini ligi kuu ya Kenya, timu za Gor Mahia, AFC Leopards na Nakuru All Stars pamoja na ligi ya Super 8.
“Sasa sisi tunaachia serikali mzigo huo wa kudhamini kandanda na michezo mingine. Kama wataweza ama hawataweza ni juu yao,” anasema Karauri.
Kampuni hiyo ilipotangaza nia yake mwaka jana, afisa mkuu wa KPL Jack Oguda aliambia BBC kwamba hatua hiyo itakuwa pigo kubwa kwa soka Kenya.
Bw Karauri ameambia mwandishi wa BBC John Nene kwamba wamejaribu kila njia kuzungumza na wakuu wa serikali lakini hawakuelewana. Juhudi zao za mahakama kuingilia kati zimeambulia patupu.
“Mtu wa mwisho ambaye tunatarajia atatusaidia ni Rais Uhuru Kenyatta. Hivi sasa tunafanya mpamgo tukutane naye tumwelezee kwa undani kuhusu uamuzi wetu,” anasema Karauri.
Licha ya uamuzi huo, Karauri amesema wataendelea kufanya kazi nchini Kenya, na kwamba hawataondoka.
Rais wa chama cha ndondi cha Kenya John Kameta amesikitishwa na uamuzi huo wa SportPesa lakini amelaumu serikali kwa kuongeza ushuru hadi asilimia 35.
“Hatuna budi ila kusimamisha ligi ya ndondi msimu huu kwa sababu sisi wenyewe hatutaweza kugharamia ligi yetu, ni pesa nyingi sana zinahitajika na kwa sasa hatuna mdhamini mwingine,” amesema Kameta.
Miongoni mwa sababu za serikali kuongeza ushuru ni kupunguza idadi ya vijana wanaocheza kamari siku hizi.
Serikalia ingali haijazungumzia kuhusu uamuzi wa SportPesa kusitisha udhamini wake wa michezo nchini Kenya.
Udhamini wa SportPesa kwa klabu za nje ya Kenya hautaathirika.
Kampuni hiyo kwa sasa hudhamini klabu za Uingereza, Everton an Hull City.
Mwaka jana Sportpesa waliingia Tanzania na kuanza kudhamini Simba inayocheza ligi kuu Tanzania na pia timu ya taifa ya Serengeti Boys.
SportPesa ni moja ya kampuni kubwa zaidi za mashindano ya kubashiri matokeo ya mechi Afrika Mashariki.
Kodi hiyo ya juu iliidhinishwa na serikali kama moja ya njia za kuzuia watoto na vijana wa umri mdogo kujihusisha na mashindano hayo ya ubashiri wa matokeo.
Wakenya waliorodheshwa kuwa miongoni mwa watu wanaoshiriki sana katika mashindano ya bahati nasibu Afrika kusini mwa jangwa la Sahara na utafiti uliofanywa karibuni.
Utafiti huo ulionesha theluthi mbili ya Wakenya wa kati ya miaka 17 na 35 wamewahi kushiriki.
Wengi hutumia simu zao za rununu kubashiri matokeo ya ligi za nyumbani na ligi za nje, sana Ulaya.
Kumekuwepo na wasiwasi kuhusu athari ya uraibu huo kwa vijana. Wazazi na viongozi wa kidini walikuwa wameiomba serikali kcuhukua hatua.
Bunge lilikuwa awali limependekeza kodi iwe 50%, lakini rais akapendekeza kodi hiyo ipunguzwe na mwishowe ikafikia 35%.

You may also like