Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Katavi

Mbunge wa Jimbo la Kavuu na Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Geophrey Pinda amemlilia Waziri wa Ujenzi Innocent Bashungwa kufuatia ucheleweshaji ujenzi wa barabara ya km 70 kutoka Kibaoni- Sitalike katika halmashauri ya Mpimbwe wilayani Mlele mkoani Katavi.

Barabara hiyo inayojengwa na Kampuni ya Kichina ya China Railway Seventh Gruop Co ltd ujenzi wake uliianza mwishoni mwa mwaka 2022 na kutarajiwa kukamilika mwaka huu.

Mhe Pinda alitembelea eneo la Barabara hiyo tarehe 3 Februari 2024 akiwa katika ziara ya jimboni kwake Kavuu kukagua shughuli za maendeleo pamoja na kuwajulia hali wale wananchi wa jimbo lake waliopatwa na ugonjwa wa kipindupindu.

Kwa mujibu wa Mbunge huyo wa jimbo la Kavuu barabara hiyo ya Kibaoni- Sitalike ujenzi wake ulitakiwa uwe umefikia asilimia 50 lakini mpaka kufikia sasa ujenzi huo unasuasua.

” Barabara hii ni muhimu sana kwa wananchi wa jimbo la Kavuu na halmashauri nzima ya Mpimbwe kwa kuwa ni ya kimkakati kwa uchumi wa wana Mpimbwe” alisema Mhe. Pinda.

Amemuaomba Waziri wa Ujenzi Mhe. Innocent Bashingwa kuitupia jicho la karibu barabara hiyo kutokana na umuhimu wake lakini pia kuwaokoa wananchi wa jimbo lake la Kavuu kutokana na adha wanayoipata wanapoitumia barabara higo.

Halmashauri ya Mpimbwe mkoani Katavi ni moja ya eneo la uzalishaji mazao mbalimbali ya kilimo kama vile Mpunga, mahindi, ufuta na alizeti na kukamilika kwa barabara hiyo itakuwa kichocheo kikubwa cha usafirishaji mazao hayo na kuwezesha wananchi kuinuka kiuchumi.