Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Mlele

Mbunge wa Jimbo la Kavuu na Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Geophrey Pinda amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan kutokana na uwekezaji mkubwa unaofanyika kwenye hospitali ya Halmashauri ya Mpimbwe (Tupindo) mkoani Katavi.

Pinda ametoa shukrani hizo Februari 27, 2024 alipotembelea na kukagua shughuli zinazofanyika katika hospitali hiyo iliyopo kitongoji cha Tupindo kata ya Mbede wilaya ya Mlele mkoa wa Katavi.

Amesema, uwekezaji uliofanyika katika hospitali hiyo hasa vile vifaa vya X-Ray na Utra Sound utachangia kwa kiasi kikubwa kuongezeka kwa wagonjwa kutoka nje ya halmashauri hiyo wakiwemo wale wa Sumbawanga vijijini katika maeneo ya finga, Mtowiza na Muze.

“Nichukue fursa hii kumshukuru sana Rais wetu Mhe, Dkt Samia Suluhu Hassan, amekuwa mama wa kuangalia maisha ya watanzania hususan wananchi wa Mpimbwe kwa kutoa fedha nyingi katika maeneo mbalimbali ikiwemo eneo hili la sekta ya afya, tunataka shida zote ziishie Mpimbwe”. Alisema Mhe. Pinda

”Kutokana na uwepo vifaa vya kisasa, tuna uhakika huduma za afya zinaendelea kuimarika na niwatake muimarishe usafi katika maeneo yanayozunguka hospitali” aliongeza Mbunge huyo wa jimbo la Kavuu.

Mganga Mfawidhi wa hospitali ya Halmashauri ya Mpimbwe (Tupindo) Dkt Rio Ernest hospitali amesema, hospitali hiyo kwa sasa inavyo vitengo mbalimbali vyenye vifaa vya kisasa kwa ajili ya kuhudumia wagonjwa na kuvitaja kuwa ni kitengo cha Afya ya kinywa, Macho, Mionzi, Wazazi, Maabara pamoja na Wagonjwa wa nje na ndani.

‘’Hospitali hii pia inacho kitengo cha dharura chenye vifaa mahsusi kwa wagonjwa wa dharura huduma ambazo kwa sasa zimeungamishwa na wagonjwa wa dharura suala linapunguza ufanisi katika idara hiyo’’. Alisema Dkt Rio

Hata hivyo, ameeleza kuwa, pamoja na uwekezaji mkubwa uliofanyika zipo changamoto kadhaa kama vile uchache wa watumishi jambo alilolieleza kuwa linalopelekea baadhi ya vitengo kutofanya kazi kwa saa 24 na kutolea mfano wa vitengo vya Famasia, Mionzi na Maabara.

Ameitaja changamoto nyingine kuwa ni barabara za ndani ya hospitali sambamba na ukosefu mitaro ya kutoa maji ndani ya eneo la hospitali. Pia ukosefu wa uzio unaosababisha usalama kwa wagonjwa, watoa huduma na mali za hospitali.

Mkurugenzi wa halmashauri ya Mpimbwe Bi. Shamim Mwariko alimueleza Mbunge wa jimbo la Kavuu na Naibu Waziri wa Ardhi Mhe, Pinda kuwa, uwelezaji uliofanyika katika hospitali hiyo kumesababisha kuongezeka kwa mapato ya hospitali.

‘’Kuongezeka vifaa kumesababisha kuongezeka wateja na hivyo kuchangia ongezeko la kasi la mapato ya hospitali ambapo mwaka jana Julai 2023 yalikuwa milioni 2 na sasa hivi tunakusanya milioni saba’’ alisema Shamim

Hospitali ya halmashauri ya Mpimbwe (Tupindo) ilianza kutoa huduma mwaka 2020 na kwa sasa hospitali hiyo inaendelea kukua kwa kasi kutokana na uwekezaji mkubwa unaofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan.