Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia,Dar

Jeshi la Polisi nchini limewatia mbaroni watuhumiwa 167 ‘Panya road’ ,katika operesheni maalumu inayoendelea katika Jiji la Dar es Salaam ambao wanatuhumiwa kushiriki katika vitendo mbalimbali vya uhalifu.

Akizungumza leo Septemba 24,2022 ,Kamishna wa Operesheni na Mafunzo kutoka Jeshi la Polisi Awadhi Haji amesema kuwa watuhumiwa wamekuwa wakijihusisha na vitendo hivyo kwa kutumia silaha za jadi kama mapanga, nondo na visu.

“Hivi vitendo vinafanywa na kundi la wahalifu wenye umri wa miaka 14 hadi 30 na kuwa kwenye makundi ya watu 10 hadi 30 hupora na kuvunja nyumba nyakati za usiku hivyo katika operesheni yetu tumefanikiwa kuwakamata watuhumiwa hao 167,”amesema.

Amesema kuwa, katika operesheni hiyo wamefanikiwa kukamata mali zilizoibiwa katika maeneo mbalimbali ya Dar es Salaam ambazo ni televisheni 23, redio, kompyuta za mezani mbili pamoja na spika mbili za sabwoofer.

Amesema watuhumiwa waliokamatwa wamekutwa na mapanga 19 , vifaa vya kuvunjia , mikasi minne, nondo saba na jeki mbili

Katika operesheni hiyo pia Polisi wamekamata magari matatu aina ya Toyota Carina namba T 314 BVY,Toyota Noah namba T 218 BYS,Toyota Noah namba T 260 BEP.

Pikipiki tano ambazo ni aina ya Boxer MC 913 DEH, Boxer MC 405 CVM, MC 856 DFY, MC 206 DDK na pikipiki moja isiyokuwa na namba walizokuwa wakizitumia wahalifu kubeba zana za kufanyia uhalifu pamoja na kusafirisha mali za wizi baada ya uporaji.

Kamanda amesema kuwa, hivi sasa hali ya Jiji la Dar es Salaam ni shwari na wananchi wanaendelea na shughuli zao kama kawaida bila hofu yoyot