‘Ukosefu wa mtaji umesababisha kushindwa kufikia ndoto yangu’

Na Mwandishi Wetu,JamhuriMedia,Arush

Kwa mujibu wa sera ya maendeleo ya wanawake na jinsia ya mwaka 2000, inaonesha kuwa idadi ya wanawake ni kubwa kwa takribani asilimia 52 zaidi ya wanaume ambayo ni asilimia 48 huku wanawake wengi wakiripotiwa kuishi vijijini.

Kwa kawaida shughuli za wanawake za kujitaftia riziki hutegemea mahali walipo kijiografia, umri wao ,mila na desturi, viwango vya elimu na rasilimali zilizopo na silimia 90 ni wazalishaji mali katika sekta za kilimo, ufugaji na uvuvi na asilimia 10 hujihusisha na uchimbaji wa madini, viwanda vidogo vidogo na ujenzi.

Kwa upande wa sekta ya kilimo kwa hivi sasa wanawake wengi wanakabiliwa na tatizo la nyenzo duni, ukosefu wa mitaji, ujuzi mdogo na kutokuwa na milki ya ardhi.

Theresia Gaudance ni mwanamke anayejishughulisha na kilimo cha biashara cha mbogamboga kama vile mchicha, mnafusaro na chainizi. Ni muda mrefu sasa tangu ameanza kufanya kazi hiyo ya uzalishaji mali na amepata faida mbalimbali ikiwemo kusomesha watoto wake na kuwagharamikia mahitaji yote ya msingi ili waweze kwenda shule na kuhakikisha wanapata elimu bora.

Theresia amesema kuna baadhi ya changamoto ambazo hadi sasa zimekuwa kikwazo katika kufikia ndoto za mafanikio yake; ‘changamoto kubwa ni kukosa mitaji itakayowezesha kumiliki maeneo makubwa zaidi na kuongeza uzalishaji hivyo naiomba serikali itusaide kutupatia mikopo yenye riba nafuu ili kutusaidia sisi wanawake.’

Katika jitihada za kuwainua wanawake hasa katika sekta ya kilimo, Afisa Kilimo wa Halmashauri ya Mji wa Babati Daniel Luther amewaasa wanawake wanaojishughuliha na kilimo kwenye maeneo mbalimbali wajiunge na vikundi vya kijamii taasisi za fedha kama vile saccos ili kupata mikopo na mafunzo wezeshi kuhusu kilimo bora na chenye tija.

Kwa hivi sasa usawa wakijinsia ni sera zinazopewa kipaumbele kwa lengo la kujenga umoja na mshikamano katika jamii, hivyo wanajamii wanapaswa kudumisha umoja na mshikamano kwa makundi haya mawili makubwa katika jamii yani wanawake na wanaume.