Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia

Mkurugenzi Mtendaji Hospitali ya Taifa Muhimbili Prof. Mohamed Janabi ameishauri jamii kujikinga na magonjwa yasiyoambukiza kwa kuweka utaratibu mzuri wa kula na kufanya mazoezi mara kwa mara kwa kuwa magonjwa hayo yamekuwa tishio ambapo yanachangia idadi kubwa ya vifo vinavyotokea ulimwenguni.

Prof. Janabi ameyasema hayo leo wakati akifungua mafunzo maalum ya kutambua magonjwa ya moyo na namna ya kufanya vipimo vya moyo kwa kutumia kifaa maalum kiitwacho Echocardiography.

Prof. Janabi ameongeza kuwa inakadiriwa watu milioni 17.9 wamefariki mwaka 2019 kutokana na magonjwa ya moyo ambapo asilimia 85 ya magonjwa hayo yalitokana na mshtuko wa moyo uliopelekea kiharusi ambapo yanaathri kwa kiasi kikubwa nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara, Tanzania ikiwemo.

“Ni vizuri tukafanya uchunguzi wa afya zetu mara kwa mara kwa baadhi ya magonjwa haya hususani shinikizo la damu halina dalili za moja kwa moja lakini kama utafanya upimaji itasaidia kubaini changamoto na kuanza matibabu mapema” amesema Prof. Janabi

Kwa upande wake Mratibu wa mafunzo hayo, Prof. Pilly Chillo amesema mafunzo hayo yamelenga kuwajengea uwezo wataalam mbalimbali namna ya kufanya vipimo na kuwabaini wagonjwa wenye changamoto za magonjwa ya moyo hivyo kurahisha huduma katika maeneo yao ya kutolea huduma.

Mafunzo hayo ya wiki nne yamehusisha washiriki kutoka Somalia, Gambia, Eswatini, Zanzibar na wenyeji Tanzania ambapo yameshirikisha washiriki 45 wa mataifa husika.

By Jamhuri