Na Mussa Augustine,JamhuriMedia

Mwenyekiti wa Chama Cha Wananchi (CUF),Profesa Ibrahim Lipumba amelitaka Baraza Kuu la Uongozi Taifa la chama hicho kujadili na kuweka mapendekezo yenye tija ya namna ya kudhibiti hali ya mfumuko wa bei ya vyakula nchini.

Profesa Lipumba ametoa maelekezo hayo wakati wa ufunguzi wa kikao cha Baraza Kuu la Uongozi Taifa la Chama cha CUF kilichofanyika katika ofisi za chama hicho Buguruni jijini Dar es Salaam.

Aidha profesa Lipumba amesema kuwa hali ya mfumuko wa bei ya vyakula iliyopo kwa sasa imezidi kuwafanya Watanzania waishi katika maisha magumu ambapo kila mmoja analalamika kwamba gharama ya maisha imepanda sana hususani gharama ya vyakula.

“Baadhi ya watu wamekuwa wakisema wananchi wale mihogo badala ya mikate wakati mihogo na viazi bei zake zimepanda,nakwa kawaida wananchi wanaokula mikate ni wachache waishio mijini,asilimia kubwa ya Watanzania wanakula vyakula vya ndani ambavyo ni mihogo na viazi” amesema Profesa Lipumba.

Katika hatua nyingine Profesa Lipumba ameseama kuwa licha ya Serikali kuruhusu mikutano ya hadhara ya vyama vya siasa lakini jambo la msingi ambalo linatakiwa kutiliwa mkazo nakutekelezwa haraka ni kuundwa kwa tume huru ya uchaguzi ambayo itasimamia uchaguzi wa Serikali za Mitaa utakaofanyika 2024 na Uchaguzi Mkuu wa 2025.

Aidha alitolea mfano uchaguzi wa Serikali za Mitaa wa mwaka 2019 ambao uligubikwa na mazingira ya ukiukwaji mkubwa wa taratibu za uchaguzi nakupelekea viongozi waliopatikana kupitia uchaguzi huo kukosa sifa za kuwa viongozi.

“Naomba wajumbe wa baraza hili kuu la Uongozi Taifa mtoe mapendekezo yenye tija katika kuishauri serikali kuhakikisha imetekeleza ombi la vyama vya siasa la kuundwa kwa tume huru ya uchaguzi ambayo itasaidia kusimamia uchaguzi wa Serikali za Mitaa utakaofanyika mwakani hilo ndilo jambo la kupewa kipaumbele kwa haraka” amesema Profesa Lipumba.

By Jamhuri