Alhamisi hii Tanzania inafanya kumbukizi ya kifo cha Rais wa Kwanza wa Zanzibar, mwanamapinduzi Sheikh Abeid Amani Karume, ambaye sasa anatimiza miaka 50 tangu alipouawa kwa kupigwa risasi Aprili 12, 1972.

Huo ndio uliokuwa msiba wa kwanza mzito kwa taifa huku taarifa za kifo chake zikitikisa misingi ya Muungano uliokuwa ukikaribia kutimiza miaka minane tangu kuasisiwa kwake.

Sheikh Karume na Mwalimu Julius Nyerere ndio waasisi wa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar uliozaa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tunayoifahamu hadi sasa.

Ndani ya wiki moja, taifa linawakumbuka waasisi hawa kwa namna mbili tofauti; Alhamisi (kesho kutwa) ni kumbukizi ya miaka 50 ya kifo cha Sheikh Karume, wakati Jumatano ya wiki ijayo ni kumbukizi ya miaka 100 ya kuzaliwa Mwalimu Nyerere.

Aidha, Jumanne ya wiki ijayo ni kumbukizi ya msiba mwingine mkubwa kwa taifa uliotokea Aprili 12, 1984, wa aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Moringe Sokoine. Hakika siku saba zijazo ni za aina yake kwa taifa letu.

Ni jambo la kujivunia kwamba wakati Sheikh Karume akitimiza miaka 50 kaburini, walau mengi kati ya aliyokuwa akiyatamani kuyashuhudia yamefanyika au yanaendelea kufanyika.

Pamoja na misukosuko ya hapa na pale iliyolikumba taifa ndani ya miaka 50 iliyopita, Tanzania imebaki kuwa moja, yenye watu wamoja wanaopendana, huku pia kukiwa na viashiria vyenye mwanga mwema katika maendeleo ya kiuchumi na ya kidemokrasia.

Wakati taifa likifanya kumbukizi ya miaka 50 ya kifo cha Sheikh Karume, ni vema wananchi na viongozi wote wa serikali – Tanzania Bara na Zanzibar tukajitafakari ni namna gani tunamuenzi baba huyu wa taifa.

Turejee hotuba na maandiko yake sambamba na kauli alizozitoa wakati wa kupigania uhuru, wakati wa mapinduzi na miaka minane aliyoishi ndani ya Muungano; kisha kutazama maeneo ya kuboresha kwa kuifanya Zanzibar na Tanzania kuwa bora zaidi.

Hatuna shaka kabisa na utawala wa Awamu ya Nane wa Zanzibar chini ya Dk. Hussein Ali Mwinyi, tukiamini kwamba 

sera na falsafa yake ya sasa ya Uchumi wa Buluu vitakwenda sambamba na ndoto za waasisi wote wa Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar kwa manufaa ya Wazanzibari na watu wote duniani.

Mungu aendelee kumpumzisha Sheikh Abeid Amani Karume na wanamapinduzi wote waliotangulia mbele ya haki. AMINA.

Mungu Ibariki Tanzania.

By Jamhuri