Wiki iliyopita niliandika sehemu ya kwanza ya makala hii nikieleza dalili ninazoziona kuwa mwanasiasa mkongwe wa Kenya, Raila Amolo Odinga, anakuwa Rais wa Kenya mwaka 2021. Odinga ambaye Wakenya wengi wanamwita “Baba”, amefahamika na kuwa kipenzi cha karibu makabila yote ya Kenya kwa sasa. 

Baada ya makala hiyo, nimepokea ujumbe mfupi na simu nyingi kwa kiwango cha kushangaza. Baadhi ya watu wameamua kuniandikia barua pepe na hapa katika sehemu ya pili nimelazimika kuchapisha ujumbe wa msomaji aliyeniletea e-mail neno kwa neno kwani unaendana na nilichopanga kukiandika. Endelea…

 

Raila Amolo Odinga ni mwanasiasa mwenye ushawishi na mwenye mbinu ambazo zinambeba sana katika harakati zake za kuitawala Kenya, tena kwa mara ya pili, baada ya kuwa kiongozi mshirika katika serikali ya mseto, alipokuwa na mamlaka sawa na aliyekuwa Rais wa nchi hiyo, Mwai Emilio Kibaki.

Ndoa yake ya lazima na Kibaki ndiyo ilituliza vurugu kubwa za baada ya uchaguzi wa mwaka 2007, ambazo baadaye zilisababisha kwa mara ya kwanza duniani Rais aliyepo madarakani, Uhuru Kenyatta, kusimama kizimbani katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu wa Kivita (ICC), yenye makao makuu yake katika mji wa The Hague, nchini Uholanzi. 

 

Vurugu hizi zilisababisha kubuniwa wadhifa usio wa kikatiba; wa waziri mkuu ili kuokoa jahazi la Kenya na kuepusha kambi ya Odinga kulalamika kuwa amepokwa ushindi na Rais Kibaki, aliyejiapisha kibabe usiku. 

Kuna mambo kadhaa ya kihistoria ambayo Odinga ameyabuni, kuyasimamia na kuyafanikisha akiwa nje ya Ikulu. Mwanasiasa huyo ametelekeza taaluma yake ya Uandisi Mitambo (Mechanical Engineering), na kujikita katika siasa, akivaa sawasawa viatu vya baba yake mzazi, Jaramogi Oginga Odinga, mwasisi wa harakati za uhuru wa Kenya na Makamu wa Kwanza wa Rais. 

 

Kabila lake la Kijaluo ndilo huonekana kama kizingiti kwenye milango ya Ikulu, na baada ya kuona hivyo amekuwa akibuni siasa za kubadilikabadilika ambazo zimemweka katika vitabu vya historia ndani na nje ya nchi yake. 

Mambo aliyobuni na kufanikisha ni kukibomoa na kukiondoa madarakani Chama kikongwe cha KANU, kilichopigania uhuru wa nchi hiyo. Mbinu hizo hizo ndizo anaonekana kuzitumia kuibomoa serikali ya sasa ya Jubilei ambayo iliundwa na muungano wa vyama vya The National Alliance (TNA), cha Uhuru Kenyatta na United Republic Party (URP) cha William Ruto.

 

Tayari amepenya na kuingia kwenye muungano huo, ambao unajulikana kama UHURUTO, na kuugawa katika mapande mawili yanayopigana madongo. Ndani ya serikali kwa sasa kuna kambi ya Uhuru inayomkubali Odinga, na ngome ya Ruto inayomponda Odinga.

Jambo la pili ni kufanikisha kuandikwa kwa Katiba bora, iliyounda taasisi huru na kuweka mifumo ya wazi ya kupatikana viongozi waandamizi wa kitaifa. Viongozi hawa hupatikana kwa mchujo wa kiusaili na si kuteuliwa tu na rais.

 Wakenya wameshuhudia uteuzi wa rais mara nyingi ukikataliwa na Bunge, jambo ambalo ni nadra katika nchi nyingi za Kiafrika, ikiwamo Tanzania.

 

 Odinga akibebwa na kazi ya Katiba bora ya mwaka 2010 ambayo ni kazi ya mikono yake, amekuwa mwanasiasa wa pekee, ambaye amesimama mahakamani na kufakiwa kutenguliwa kwa matokeo ya urais yaliyotangazwa kuwa Uhuru Kenyatta ameshinda kupitia sanduku la kura. Tena akiwa Rais anayetetea kiti chake, baada ya kumaliza muhula wake wa kwanza ofisini.

Pia ni kiongozi pekee barani Afrika aliyejiapisha mwenyewe nje ya mfumo rasmi wa kikatiba, bila kushtakiwa kwa uhaini. Mamlaka ziliishia kumalizia hasira zake kwa mwanasiasa mtata, aliyedaiwa kushuhudia kiapo hicho, Wakili Miguna wa Miguna.

Pamoja na Rais Kenyatta kushinikizwa amkamate kwa uhaini, alimtafuta kwa faragha na kuunda naye ushirika ambao unaonekana kuileta pamoja Kenya, iliyokuwa inaelekea kutumbukia tena katika machafuko.  Maafikiano haya yamezaa ‘utakatifu’ ambao Wakenya wameubatiza jina la kimombo, handshake.

 

Odinga ametokea wapi hadi kufanikisha haya? Yeye na kundi lake waliounda NARC – vuguvugu la kitaifa la Upinde wa Mvua, baada ya kuibwaga serikali ya KANU na kukamata dola, waliweka mikakati ya kuijenga Kenya mpya wakimtanguliza Kibaki kama kiranja wao?

Please follow and like us:
Pin Share