Wiki iliyopita tuliishia katika eneo linaloonyesha kuwa nchini Tanzania hakuna chama kinachoweza kuunda muungano na kikasimamisha mgombea kama walivyotaka wanasiasa wa upinzani mwaka 2015 kupitia Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA). Kwa Kenya, hili linawezekana. Wamelifanya mara kadhaa na limekuwa na matokeo ya aina yake. Endelea…

Wenzetu kule Kenya wana kitu kinaitwa sympathy vote, yaani kura za huruma. Ni huruma ileile iliyowasaidia Uhuru na Ruto kukamata dola wakiwa na kesi mahakamani.

Ilibidi Odinga, Waziri Mkuu (mstaafu) pekee katika nchi ya Kenya, asubiri hadi mwaka 2017 alipoingia tena kwenye kinyang’anyiro na kubwagwa tena katika uchaguzi uliotenguliwa na mahakama ya juu.

Akichagizwa na alichokiita safari ya Canaan, alipeleka ushahidi na vielelezo vilivyowashawishi majaji wakabubali kuwa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC), chini ya uongozi wa Wakili Msomi, Wafula Chebukati, ilifanya makosa yaliyovuruga uchaguzi.

Likiongozwa na Wakili Mwandamizi mwenye mbwembwe nyingi, James Orengo, aliyekuwa tayari amenyakua useneta wa Kaunti ya Siaya, jopo la mawakili lilisema Kenyatta hakushinda, bali alibebwa na kina Chebukati. Kwa sasa Orengo ndiye Kiongozi wa Walio Wachache katika Bunge la Seneti. Hata hivyo, safari ya Canaan ya Odinga iliishia gizani baada ya sharti lake la kuibomoa IEBC kabla ya uchaguzi wa marudio kugonga mwamba.

 Kenyatta aliingia ulingoni mwenyewe, akapiga kampeni mwenyewe na kukishinda kivuli chake alichokuwa anashindana nacho.

Odinga hakukubali ushindi na akakataa kumtambua Kenyatta, alianzisha mashambulizi mapya na kuibuka mshindi, baada ya Rais Kenyatta kukutana naye faragha kabla ya kutangaza hadharani kumaliza uhasama wao na kuamua kushirikiana kuijenga Kenya.

Kabla ya kujiapisha kuwa Rais wa Wananchi, aliweka mikakati ya kuhujumu uchumi imara  wa nchi hiyo na kuwataka wafuasi wake zaidi ya milioni sita kususia bidhaa za makampuni yanayomilikiwa na Rais Kenyatta na washirika wake Ruto, maziwa ya paketi ya ng’ombe – Brookside yanayozalishwa na familia ya Kenyatta yalidodea madukani.

Hakuishia hapo, aliwataka wafuasi wake kujitokeza hadharani na kuharibu laini ya Kampuni ya simu ya Safaricom iliyokuwa ikipeperusha matokeo ya uchaguzi uliompa ushindi Kenyatta.

Aliwataka wafuasi hao wasuse na kujiunga na kampuni yenye upinzani mkubwa na Safaricom, Airtel Kenya. Jitihada zake zilijibu baada ya Kampuni ya Safaricom kutangaza kupata hasara kubwa ndani ya kipindi kifupi.

Alihakikisha anavuruga mji wa kitalii na wenye bandari wa Mombasa na kusababisha baadhi ya hoteli za kitalii kufungwa. Hujuma hizi zikichagizwa na Odinga kujiapisha kuwa Rais wa Wananchi, zimesababisha Kenyatta kusalimu amri na kukubali kufanya kazi pamoja na Odinga.

Alimpiga chenga mshirika na makamu wake, Ruto, na kukutana faragha na Odinga, kabla ya kutangaza ushirikiano kwenye ngazi za jumba la Harambee, ilipo ofisi ya rais.

Kwa sasa Odinga si msaliti, bali ni Mkenya, mzalendo wa kweli, na amekwisha kushirikishwa katika matukio kadhaa ya kitaifa japo hana wadhifa wowote serikalini. Makubaliano ya hao wawili yamemtia kiwewe Ruto ambaye alijua ndiye mrithi wa Rais Kenyatta mwaka 2022.

Kuna mambo makuu matatu yanayomtia kiwewe Ruto na wapambe wake, ambao wanazunguka nchi nzima na kumwaga pesa kama njugu kwenye mikutano ya hadhara na harambee ili kuungwa mkono mwaka 2022.

 Kubwa zaidi ni tetesi kwamba Tume ya Pamoja ya Odinga na Kenyatta ya kutekeleza vipaumbele vinne walivyodai vya kuiokoa Kenya, itaibuka na wazo la kuitisha kura ya maoni kubadili mfumo wa utawala. Inasemekana itapendekezwa kubuniwa wadhifa wa Waziri Mkuu Mtendaji, na abakie rais asiye na meno kama ilivyo nchini Ujerumani.

Jambo la pili, ukimya wa Rais Kenyatta kuhusu ama atamuunga mkono au hataunga mkono mbio za Ruto za kumrithi mwaka 2022.

Kama hilo halitoshi, uamuzi wa Rais Kenyatta kumulika utajiri wa viongozi wakuu wa umma akiwemo yeye mwenyewe, ndio umemchosha zaidi Ruto aliyetajirika ghafla. Kura za maoni zilizotolewa hivi karibuni na kampuni moja jijini humo zimemtaja Ruto kama mwanasiasa fisadi namba moja nchini humo, akifuatiwa na Gavana wa Kirinyaga, ambaye alifutwa kazi ya uwaziri kutokana na tuhuma za kifisadi katika wizara inayoshughulika na huduma za vijana – National Youth Service (NYS), Anne Waigui.

Wawili hao (Ruto na Waigui) wanahaha kusafisha majina yao huku Rais Kenyatta akiwa kimya. Jambo jingine linalomtia tumbo joto ni kitendo cha Odinga kujipenyeza kwenye Mkoa wa Bonde la Ufa, ambako ni ngome kubwa ya Ruto anayeungwa mkono na kabila lake la Wakalenjini.

Unajua Odinga amefanya nini? Usikose nakala ya JAMHURI wiki ijayo kwa mwendelezo wa makala hii.

Please follow and like us:
Pin Share