Rais ampandisha cheo aliyekataa rushwa

Meneja wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Kilimanjaro, Msafiri Mbibo, ameteuliwa kuwa Naibu Kamishna Mkuu wa Mamlaka hiyo.

Taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu, Gerson Msigwa, imesema uteuzi huo uliofanywa na Rais John Magufuli, umeanza Machi 31, mwaka huu.

Desemba, mwaka jana, Gazeti la JAMHURI liliandika habari iliyohusu Mbibo kukataa rushwa. Baadaye Januari, mwaka huu wakati wa mkutano wa TRA na wafanyabiashara, Rais Magufuli alimpongeza kwa ujasiri wake na kumwagiza Kamishna Mkuu wa TRA, Charles Kichere, “kumtazama” vizuri.

Habari iliyompaisha Mbibo ilihusu kuhukumiwa kwa Meneja Fedha wa kampuni za ujenzi za Dott Services (TZ) Ltd na General Nile Company for Roads and Bridges/Dott Services JV, Suresh Kakolu, kulipa faini ya Sh milioni 1, hivyo kukwepa kifungo cha miaka mitatu jela kwa kosa la kutoa rushwa.

Kakolu alikiri kosa la kumhonga Mbibo dola 2,000 za Marekani (Sh milioni 4.6 kwa viwango vya kubadilisha fedha Desemba, mwaka jana).

Kakolu alikamatwa na makachero wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Novemba 15, mwaka jana katika ofisi za TRA mkoani Kilimanjaro.

Ilielezwa kuwa alitoa kiasi hicho cha fedha kwa Mbibo ili apitishiwe maombi ya msamaha wa kodi wa Sh bilioni 6.604.

Kampuni hizo mbili zilikuwa zikidaiwa kodi hiyo kuanzia mwaka 2013 hadi Oktoba, mwaka jana. Alifikishwa mahakamani Novemba 16.

Mbele ya Hakimu Mkuu Mkazi Mfawidhi, Sophia Massati, alisomewa mashtaka na Mwendesha Mashtaka wa TAKUKURU, Rehema Mteta, kwa kosa moja la kutoa rushwa ya dola 2,000 za Marekani kinyume cha Kifungu 15(1), (b) na Kifungu kidogo (2) cha Sheria ya TAKUKURU Na. 11 ya mwaka 2007.

Alikana mashtaka na kuachiwa kwa dhamana hadi Novemba 30, mwaka jana alipokiri kosa lake na kuhukumiwa kwenda jela miaka mitatu au kulipa faini hiyo. Mshtakiwa alilipa faini.

Baada ya hukumu hiyo, Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Kilimanjaro, Holle Makungu, aliliambia JAMHURI kuwa dola 2,000 serikali imezitaifisha.