Rais Dkt.Mwinyi ateua viongozi mbalimbali

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt.Hussein Ali Mwinyi amefanya uteuzi wa viongozi mbalimbali.

Hayo ni kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo Agosti 30, 2022 na Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi Zanzibar, Mhandisi Zena A.Said ambapo uteuzi huo unaanza leo.

Mosi, Rais Dkt.Mwinyi amemteua Issa Suleiman Ali kuwa Mkurugenzi wa Idara ya Uendeshaji na Utumishi katika Wizara ya Uchumi wa Buluu na Uvuvi.

Kabla ya uteuzi huo,Bw.Issa alikuwa Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Uendeshaji na Utumishi katika wizara hiyo.

Pili, Rais Dkt.Mwinyi amemteua Dkt.Ali Said Nyanga kuwa Mkurugenzi wa Afya Kazini katika Ofisi ya Rais, Kazi, Uchumi na Uwekezaji.

Dkt.Nyanga kabla ya kuteuliwa na Rais Dkt.Mwinyi alikuwa Mkurugenzi wa Kinga na Elimu ya Afya katika Wizara ya Afya.

Tatu, Rais Dkt.Mwinyi amemteua Mohamed Jaffar Jumanne kuwa Mkurugenzi wa Idara ya Uendeshaji na Utumishi katika Ofisi ya Rais, Kazi, Uchumi na Uwekezaji.

Bw.Mohamed kabla ya kuteuliwa na Rais Dkt.Mwinyi alikuwa Afisa Mwandamizi katika Wakala wa Usajili Biashara na Mali Zanzibar katika Wizara ya Biashara na Maendeleo ya Viwanda.

Nne, Mheshimiwa Rais Dkt.Mwinyi amemteua Dkt.Bill Mruma Kiwia kuwa Kamishna wa Idara ya Mashirikiano Kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPP) katika Ofisi ya Rais, Kazi, Utumishi na Uwekezaji.

Kabla ya kuteuliwa na Rais Dkt.Mwinyi, Dkt.Bill alikuwa Msaidizi wa Rais katika Masuala ya Uchumi.

Tano,Rais Dkt.Mwinyi amemteua Dkt.Abdulhamid Yahya Mzee kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Kampuni ya Maendeleo ya Mafuta na Gesi Asilia (ZPDC) katika Wizara ya Uchumi wa Buluu na Uvuvi.

Dkt.Mzee ni Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi mstaafu wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ).