Kuna siku nilikuwa eneo moja la katikati ya Victoria na Makumbusho jijini Dar es Salaam, tukijadili mambo mbalimbali likiwamo la matokeo ya uchaguzi mdogo wa Jimbo la Arumeru Mashariki. Hapo kuna mtu aliibua hoja ya hali aliyonayo Rais Jakaya Kikwete kwa sasa.
Pasipo kuumauma maneno, yule bwana alieleza wazi kuwa hivi sasa Rais Kikwete hana imani na kundi lolote ndani ya CCM, na yupo radhi hata kukabidhi nchi kwa upinzani kwani ndiyo itakayokuwa salama yake.

Yule bwana alizidi kutupasha kuwa ndani ya CCM kuna makundi mawili na kila kundi JK ameliumiza vilivyo, na kukabidhi nchi kwa CCM anahisi naye pia atakuja kuumizwa mbele ya safari.

Nikaona hapa kuna jambo la kuzungumzwa na kupima ukweli wake. Unapozungumzia Chama Cha Mapinduzi (CCM) unazungumzia chama kilichoshika dola (uongozi wa nchi yetu), na ndiyo chama pekee kilichobeba maisha ya Watanzania wote kwa sasa hadi hapo uchaguzi mwingine mkuu utakapoitishwa.

Ni ukweli ulio wazi kuwa wanachama wengi wa CCM ya sasa, hususani viongozi wa ngazi mbalimbali, wana kasoro za kutokuwa waadilifu, wawajibikaji kwa vitendo na uzalendo kwa chama hicho na Watanzania kwa ujumla.

Matokeo yake tunashuhudia maisha ya Watanzania yakiwa magumu sana. Watanzania wanaishi pasipo na matumaini kutokana na matatizo kama vile kupanda kwa gharama za maisha, kunakosababishwa na mfumuko wa bei, ukosefu wa ajira. Waliobahatika kuwa nayo wanalipwa mshahara usiokidhi.

Wananchi kuporwa haki zao (mathalani ardhi), matatizo ya umeme, elimu duni. Kiukweli matatizo ni mengi mno ambayo Mtanzania ametwishwa msalaba.

Nimejiuliza sana kushamiri huku kwa matatizo haya yote ndani ya jamii zetu, hususani tangu Awamu ya Nne iingie madarakani kumesababishwa na nini? Chanzo cha haya yote ni nini?

Mosi; msamiati wa neno ‘makundi hasimu’ ulianza kusikika na kuvuma mara baada ya Awamu ya Nne inayoongozwa na Rais Kikwete kuingia madarakani.

Ni kwa mara ya kwanza masikio ya Watanzania yanasikia na macho yanaona uwepo wa makundi mawili hasimu ya wapambanaji dhidi ya ufisadi, huku midomo yao ikiwa na punje za ufisadi, pamoja na kundi la watuhumiwa wa ufisadi wasiothibitishwa ufisadi wao.

Makundi haya yalizidi kupamba moto mara baada ya msamiati mwingine usio na tija wa kujivua gamba kuasisiwa. Kuliibuka hali ya wale ambao ni wapambanaji wa ufisadi kupata fursa ya kiuongozi katika ngazi za juu za chama, na kuitumia fursa hiyo kudhalilisha majukwaani na hata kwenye vyombo vya habari kundi jingine, kwa kuwaambia ‘laivu’ waondoke katika chama, jambo ambalo ni kinyume kabisa na makubaliano yao.

Jionee mpango huu wa viongozi wa chama kuamua kutenda mambo kinyume na utaratibu wa chama, lakini cha kushangaza viongozi wakuu wa chama akiwamo Mwenyekiti wa CCM (Taifa), Jakaya Kikwete (ambaye ni sawa na Baba wa chama kwa sasa), akikaa kimya pasipo kutoa karipio kwao. 

Hakika huu ni mpango wa Kikwete wa kuhakikisha anaongeza mpasuko katika chama, viongozi na wanachama wavurugane ili dhamira yake ya kukabidhi chama upinzani itimie.

Ukimya wa Rais Kikwete unaonyesha kubariki vitendo vyao na wakati huo huo tunamuona akicheka na kila kundi, jambo linaloacha maswali mengi yakiashiria malengo ya kuchochea zaidi vurugu za kisiasa ndani ya CCM –  JK anaongeza mpasuko na hatimaye dhamira ya kukabidhi nchi upinzani itimie.

Pili; kwa muda mrefu sasa Rais Kikwete amekuwa akifanya teuzi zake kwa kuyapambanisha makundi haya katika sehemu moja. Matokeo ya haya ni kuona Waziri kutokuwa na ushirikiano na Naibu Waziri wake au Katibu Mkuu wake, kutokana na wawili hao kuwa na malengo tofauti.

Hali hiyo imeendelea kudumishwa na Rais Kikwete hadi kwenye ofisi za mikoa, wilaya na hata kwenye bodi mbalimbali.

Matokeo ya kuwachanganya watu wenye mitazamo tofauti ni kushuhudia kudorora kwa utendaji kazi, kiwango cha maendeleo chanya kutokupatikana, na hatimaye nchi yetu kuzidi kuwa masikini na watu wake nao kuwa masikini zaidi.

Ngoja nikupe mfano hai wa upande wa uteuzi wa Wizara mbalimbali. Kila uteuzi wa Wizara wamechanganya watu wenye dhamira mbalimbali. 

Tuchukilie mfano wa Wizara ya Kazi na Maendeleo ya Vijana ambako Waziri ni Dk. Gaudensia Kabaka (mfuasi wa kundi la Wapambanaji – kumbuka alivyomjibu Lowassa juu ya suala la ajira), na Naibu wake ni Dk. Makongoro Mahanga ambaye ni mfuasi wa wanaowaita mafisadi.

Matokeo ya Rais Kikwete kuwapambanisha watu hawa ni kushuhudia tatizo la ajira kwa vijana likizidi kukua badala ya kupungua. Ajira nchini limekuwa ni tatizo kubwa linalozidi kukua kila kukicha. Kwa mujibu wa utafiti uliofanyika inaonyesha kwa mwaka 2010 tatizo la ajira nchini lilikua kwa asilimia 12 na kwa mwaka huu tatizo hili limefikia asilimia 15.

Ukizitazama hizo takwimu, utagundua kuwa tatizo linazidi kukua badala ya kupungua kwa kadri siku zinavyosonga mbele huku waathirika wakubwa katika hili wakiwa ni kundi la vijana.

Vijana wanaoathirika zaidi ni wale wenye umri wa kati ya miaka 15 hadi 24 ambao ndiyo nguvu kazi ya taifa. Na kwa wastani vijana wapatao 850,000 huingia katika soko la ajira kila mwaka na wanaopata ajira rasmi ni asilimia tano tu ambao ni sawa na vijana 40,000. Kati ya hao wanaoingia katika ajira ya kilimo ni asilimia 30 na huku asilimia 35 wakiajiriwa katika sekta isiyo rasmi.

Hata ukijaribu kuangalia ukubwa wa tatizo ulivyo kwa kulinganisha takwimu kwa mujibu wa Bara la Afrika, wasio na ajira ni asilimia 21, wakati hapa nchini ni asilimia 30 ndiyo wasio na ajira. Hali hii ni ishara tosha kuwa tupo kwenye hali mbaya.

Huo ni mfano mmoja tu unaoonyesha kudorora kwa maendeleo. Ukichunguza kwenye Wizara nyingine, utagundua mambo ni yale yale yanayotokana na ‘mafahali wawili’ kukaa zizi moja, hali inayozaa utendaji wao kuwa ni wa maneno matupu kwani ndani mwao kunawaka moto.

Kwa mpango huu unaoendeshwa na Rais Kikwete, ni dhahiri wanaoumia ni wananchi wa kawaida wasio na hatia na malumbano yao ya kisiasa. Na kwa hakika huu utakuwa uthibitisho mwingine ninaoamini kuwa Rais Kikwete ana dhamira ya kukabidhi nchi kwa upinzani.

Tatu; kitendo cha Rais Kikwete kukaa kimya katika kuyashughulikia matatizo ya Watanzania.

Mara kadhaa tumesikia wananchi wakilia na matatizo mbalimbali kama vile kuporwa ardhi zao, uhaba wa mafuta nchini, na lile sakata la mgomo wa madakatari lililogharimu uhai wa wananchi ambao serikali iliyopo madarakani walikula kiapo cha kutunza mali, uhai na usalama wa raia wake.

Lakini jambo la kushangaza Rais Kikwete amekuwa kimya kuyatolea ufafanuzi. Ni kwamba hakuwa na taarifa za matukio hayo ama wananchi wanapoumia huwa ni furaha kwake? Kama huu si mpango mkakati wa kupandikiza chuki kwa wananchi ili waichukie CCM na wainyime kura, basi tuuiteje?

Hali hii inanifanya niamini hata huu mgawo wa umeme unaoendelea haujasababishwa na tatizo la kiufundi ndani ya Tanesco, isipokuwa ni muendelezo wa hujuma za kupandikiza mbegu ya chuki kwa wananchi na hatimaye wainyime kura CCM.

Hakika, mpango wa Kikwete hauna tija! Kwa mwendo huu, Rais Kikwete asitarajie kukumbukwa hata kidogo kutokana na kujidhihirisha wazi kuwa anafurahia umasikini wa Watanzania!

Nne; kitendo cha Rais kuwasikiliza zaidi wapinzani kuliko kundi jingine lolote. Imefikia hatua kwa Kikwete kutokuwa hata na muda wa kuwasikiliza wanachama na viongozi wa CCM ambao ndiyo hasa waliobeba mustakabali wa taifa letu kwa sasa.

Katika hili ipo mifano mingi, ila nitakuthibitishia kwa mfano mmoja tu. Mfano wenyewe ni kwenye harakati nzima za kuelekea kuipata Katiba mpya.

Katika mchakato wa kuandika mswada wa katiba hiyo mpya, Rais kikwete aliweza kupata muda wa kukutana na vyama vya upinzani na kuchukua mawazo yao, lakini alishindwa kufanya hivyo kwa upande wa CCM.

Sote tunajua Rais Kikwete alikutana na vyama vya Chadema, NCCR-Mageuzi na CUF lakini hatukuwahi kusikia mkutano wa Rais Kikwete na CCM. Hii ni hujuma kwa CCM!

Sisemi kwamba wapinzani wasisikilizwe, la hasha. Ila Rais Kikwete anapofanya hivi kwa chama kilichoshika dola, anatarajia nini kwa mustakabali wa Taifa?

Nikijaribu kuyatafakari yale niliyoyasikia, ninagundua na kuamini kuwa ni kweli Rais Kikwete amedhamiria kuiangusha CCM na hata pia kujipambanua waziwazi kuwa yeye ndiye chanzo cha umasikini wa Watanzania.

Nahitimisha makala haya kwa kuikumbuka kauli iliyowahi kutolewa na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, aliposema:

Nanukuu “Kutokana na umri wake mkubwa, watu wengi wenye kasoro wamejiingiza na kukichafua chama hiki. Sasa kimekuwa kama kokoro ambalo wakati mwingine hubeba viumbe visivyohitajika. Tunao watu wa ajabu ndani ya CCM ambao hawafanani na CCM.” mwisho wa kunukuu.

Manyama1961@gmail.com

Manyama Manyama amejitambulisha kuwa ni msomaji wa Gazeti la JAMHURI. Je, wewe unayo mawazo ya kuiendeleza nchi hii? Usisite kutuandikia kama alivyofanya Manyama. Mhariri.

1284 Total Views 3 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!