Rais Magufuli ainusuru Burundi

MagufuliiTanzania imeinusuru Burundi kushambuliwa na majeshi ya Umoja wa Afrika (AU) baada ya kushauri na kusikilizwa kuwa pande zinazokwaruzana zichukue mkondo wa mazungumzo badala ya kuendelea na vita inayoweza kuiingiza nchi hiyo katika mauaji ya kimbari.

Waziri wa Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, Balozi Dk. Augustine Mahiga, ameliambia JAMHURI mwishoni mwa wiki kuwa Rais wa Tanzania, Dk. John Pombe Magufuli aliamua kufufua mazungumzo ya amani nchini Burundi mara tu baada ya kuteua Baraza la Mawaziri.

“Tulipomaliza kuapishwa pale Ikulu, ghafla Mheshimiwa Rais akaniambia anza kazi. Kazi yangu niliianzia pale Ikulu. Akasema kuna shida pale Burundi, tukaingia kwenye chumba na Mkuu wa Majeshi, Mkuu wa Usalama wa Taifa na wajumbe wengine, akasema ni lazima mpate jibu jinsi ya kumaliza mgogoro wa Burundi,” alisema Balozi Mahiga.

Baada ya mazungumzo hayo yaliyofanyika Ikulu Desemba 12, 2015 Balozi Mahiga na wajumbe waliohudhuria kikao hicho walishauriana na kukubaliana kuwa Tanzania iwasiliane na Uganda kwa nia ya kufufua Kamati ya Usuluhishi iliyokuwa ikiongozwa na Rais Yoweri Kaguta Museveni.

Wakati hayo yakiendelea, Rais Magufuli aliwasiliana na Rais Museveni, kisha akawasiliana na Rais Pierre Nkurunziza wa Burundi, kumsihi achague mkondo wa mazungumzo baada ya Azimio la Baraza la Usalama na Amani la Umoja wa Afrika ambalo amesema iwapo lingetekelezwa lingeleta machafuko zaidi na shida ya majeshi ya Afrika kupambana na Waafrika wenzao na hatimaye kuuana, jambo asilopenda kuona likitokea.

“Ingawa hata sisi ni wanachama wa Baraza lile, lakini tulikuwa tangu mwanzoni tume-express reservation. Na bahati nzuri, tulivyofika mahala fulani, tukaona bado kuna nafasi ya mazungumzo, na siyo tu kupeleka jeshi, na kama kutakuwa na umuhimu wa kupeleka majeshi ya aina fulani kwa madhumuni fulani, itokane na mazungumzo ya amani,” amesema Balozi Mahiga.

Anasema mkataba wa AU kifungu cha 4(h) kinaruhusu AU kuingilia nchi mwanachama bila kibali chake yanapokuwapo mauaji ya kimbari, uhalifu dhidi ya binadamu, uhalifu wa kivita na ukatili dhidi ya binadamu. Hata hivyo, kabla ya kufikia uamuzi huo, inabidi Baraza la Usalama na Amani la Umoja wa Afrika, lipate baraka za mkutano wa marais wa nchi za Afrika, kisha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, ndipo waweze kufanya huo uvamizi. “Kufikia hapo ni mpaka muone kuwa ile nchi imeshindwa kulinda watu wake, au yenyewe ni chanzo cha mgogoro huo, basi hapo Afrika kwa umoja wake, inaruhusiwa kuingilia bila kibali,” ameongeza Balozi Mahiga.

AU ilitaka wapelekwe askari 5,000 kwa kutumia Brigedi ya Afrika Mashariki, jambo ambalo lingeleta mgogoro zaidi kwani Rwanda inayotuhumiwa kutoa mafunzo kwa waasi wa Burundi, nayo ni sehemu ya nchi wanachama zinazounda Brigedi hiyo. Rwanda katika hatua hiyo ilijitoa, na hili bado lingeendeleza mgogoro zaidi.

Burundi nayo imejitetea kuwa hakuna mauaji ya kimbari nchini humo na ikasema Afrika ikiamua kuivamia itakuwa haiitendei haki wala heshima kwani yenyewe imetoa askari 6,000 wanaolinda amani nchini Somalia, hivyo isingependeza kulipwa ubaya kwa wema.

Waziri alisema kama ipo haja ya kupeleka jeshi nchini Burundi, ni vyema jeshi hilo likaenda kwa maafikiano na Serikali ya Burundi, na ikiwezekana jeshi hilo liende kufanya kazi ya kipolisi badala ya jeshi kwa kulinda miundombinu ya msingi, kuwanyang’anya silaha wenye silaha kinyume cha sheria na kuwahamasisha wanaopingana wakazungumze badala ya vita. Pia amesema askari 5,000 ni wengi mno, kwenda Burundi hivyo akasema hatua yoyote ya kupeleka jeshi ni bora ikatokana na majadiliano.

Alirejea tatizo la tafsiri ya kisheria katika Mkataba wa Arusha, ambapo Kifungu cha 96 cha Katiba ya Burundi kinasema Rais atakaa madarakani mihula miwili kwa kuchaguliwa na wananchi, huku kifungu kingine kikiruhusu Rais kuchaguliwa na Bunge katika kipindi cha mpito. Nkurunziza, amegombea kipindi cha tatu kwa maelezo kuwa kipindi cha kwanza alichaguliwa na Bunge hivyo hakuchaguliwa na wananchi suala lililoibua mgogoro mkubwa.

Balozi Mahiga amesema Rais Jakaya Kikwete kipindi akiwa madarakani baada ya taarifa za Burundi kuwa na dalili za kuwapo mauji ya kimbari kwa madai kuwa huenda walikuwa wanalengwa Watutsi pekee katika mauaji hayo, aliitisha kikao kwa kutumia kofia ya Tanzania kuwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na marais hao walipokutana wakamteua Rais Museve kuwa msuluhishi wa mgogoro huo.

Hata hivyo, wakati Rais Nkurunziza akiwa kwenye majadiliano hayo, lilifanyika jaribio la kumpindua chini ya Jenerali Godefroid Niyombare, mapinduzi ambayo hayakufanikiwa. Balozi Mahiga anasema hili liliongeza uhasama na kumfanya Rais Nkurunziza asione sababu ya kuzungumza na watu au vikundi vilivyokuwa na nia ya kumuua kupitia mapinduzi.

Kwa bahati mbaya, baada ya Rais Museveni kuanzisha mchakato wa mazungumzo, jukumu hilo alilikabidhi mikononi mwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Uganda, Dk. Crispus Kiyonga ambaye naye kutokana na kwamba Kamati yake ilifanya kazi wakati Tanzania na Uganda zikiwa kwenye mchakato la uchaguzi mkuu, Kamati hiyo haikupata fursa ya kutoa taarifa juu ya maafikiano yaliyofikiwa.

Katika hali hiyo, Burundi ilijiona kama imepuuzwa na majirani zake na ikaanza kutoa shutuma za wazi kuwa Rwanda inashiriki kutoa mafunzo kwa waasi. Akasema pia kilikuwapo kikundi cha Mbonelakule, ambacho kilianza kutesa watu na hali hiyo ikawa inatoa ishara za mauaji ya kimbari.

Pamoja na hayo yote, Burundi imeshiriki mazungumzo ya kwanza mjini Entebbe, Uganda mwezi uliopita yakishirikisha makundi ya waasi na wa ndani na nje, lakini Serikali ya Burundi imesisitiza kuwa aina ya washiriki kwenye mazungumzo hayo wanapaswa kufahamika, na kwamba Januari 6, iliyokuwa imepangwa mazungumzo yafanyike Arusha, Serikali ya Rais Nkurunziza haikuipendelea kwa kuona kuwa huenda ina lengo la kuleta mazungumzo ya Arusha Awamu ya Pili suala linalotonesha vidonda vilivyoanza kupona.

Hadi sasa, amesema Serikali ya Tanzania inawezesha mazungumzo hayo chini ya Msuluhishi Rais Yoweri Museveni, na imefanya juhudi kubwa ikiwamo Rais John Magufuli kumwandikia barua Mwenyekiti wa AU, Dk. Nkosazana Dlamini Zuma, aliyekubali ombi la Rais Magufuli kusitisha upelekaji wa majeshi Burundi kwa nia ya kuruhusu mkondo wa mazungumzo uchukue nafasi.

Balozi Mahiga amesema kwa sasa bado wanaendelea kushauriana na anaamini baada ya muda si mrefu ufumbuzi wa kudumu utapatikana nchini Burundi, lakini si kwa njia ya mtutu bali kwa njia ya mazungumzo.