Na Mwandishi Wetu

Jumla ya Dola za Marekani 700,000 (sawa na Sh bilioni 1.6) zimepatikana katika uzinduzi wa harambee ya kampeni ya GGML Kili Challenge iliyoongozwa na Rais mstaafu Dk. Jakaya Kikwete kwa lengo la kukusanya Sh bilioni 2.3 fedha zitakazotumika kuendeleza.

Tanzania bila UKIMWI, inawezekana! Msemo huo ulikuwa wa Rais Mstaafu Dk. Jakaya Kikwete

Dk. Kikwete alisema Serikali yenyewe haiwezi kutokomeza janga la Ukimwi bila kuwepo kwa ushirikiano kati yake na sekta binafsi ili kuhakikisha katika kipindi cha miaka saba iliyosalia kufikia 2030, hakuna kifo chochote kitokanacho na janga hilo.

Mkurugenzi Mtendaji wa GGML, Terry Strong (kushoto) akimkabidhi zawadi Rais mstaafu Jakaya Kikwete kutokana na mchango wake kwenye Kampeni ya GGML Kili Challenge iliyoanzishwa na kampuni hiyo mwaka 2002 kwa kushirikiana na TACAIDS. Jana Alhamisi Kikwete ameshiriki katika uzinduzi wa harambee ya kampeni hiyo kwa mwaka huu jijini Dar es salaam

“Hamasa inatakiwa kuendelea kutolewa kwa ukubwa kwa sababu tumetoka mbali, tumepunguza vifo vitokanavyo na Ukimwi kutoka 72,000 mwaka 2016 hadi 54,000 mwaka 2021,” alisema na kuongeza kuwa;

“Tatizo bado ni kubwa, suala la msingi tuhakikishe fedha zinazokusanywa kupitia kampeni ya GGM Kili challenge zinawafikia walengwa husika.”

Akizungumzia katika kampeni hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa GGML, Terry Strong mbali na kuishukuru Serikali kwa kuunga mkono kampeni hiyo, alisema wakiwa wadau wa mapambano hayo ya UKIMWI na VVU, GGML imepokea msaada ambao uliiwezesha Kili Challenge kupiga hatua kubwa hadi kufikia kuwa mfuko wa kimataifa, wenye kushirikisha wapanda mlima na waendesha baiskeli kutoka mabara yote na zaidi ya nchi 20.

Alisema kampeni hushirikisha wapanda mlima Kilimanjaro kwa njia ya miguu na njia ya baiskeli ili kuhamasisha jamii kuchangia fedha za kutunisha mfuko wa mapambano ya Ukimwi pamoja na juhudi za kutokomeza maambukizi ya janga hilo.

Kwa upande wake Makamu Rais wa AngloGold Ashanti- GGML anayeshughulikia miradi endelevu Ghana na Tanzania, Simon Shayo amesema tangu kuanzishwa kwa kampeni hiyo makundi mbalimbali yamefaidika ikiwa kuazishwa kwa kituo cha kulea watoto yatima na wanaoshi katika mazingira magumu – Moyo wa Huruma kilichopo Geita.

Alisema katika kundi la kwanza la watoto waliolelewa kwenye kituo hicho sasa wamefikia elimu ya chuo kikuu ikiwamo wawili ambao wanasomea udaktari.

Alisema pia wameanzisha vituo vya maarifa katika maeneo hatarishi kwa maambukizi ya VVU, Manyoni na Segera ambavyo vinatoa elimu kuhusu VVU/ Ukimwi kwa madereva wa malori ya masafa marefu kwani pia ni kundi hatarishi kwa janga hilo.

Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), Ummy Hamis Nderiananga (kulia) akimkabidhi zawadi maalumu Rais mstaafu Jakaya Kikwete kwa kutambua mchango wake muhimu katika kampeni ya GGML Kili Challenge ambayo ilianzishwa na Kampuni ya GGML mwaka 2002 kwa kushirikiana na TACAIDS kwa lengo la kutokomeza VVU/ UKIMWI.

“Chochote ambacho mtatoa au mlichowahi kutoa kinalenga kufikia sifuri tatu yaani kupunguza kabisa kwa kufikia asilimia sifuri ya maambukizi mapya, sifuri ya unyanyapaa pamoja na sifuri katika vifo vitokanavyo na UKIMWI,” alisema.

Wakati huo huo  Mkurugenzi Mkuu wa TACAIDS, Dk. Leonard Maboko alisema fedha zinaokusanywa hupelekwa pia kwa asasi zisizo za serikali zinazoendeleza mapambano dhidi ya VVU/ Ukimwi.

Alitolea mfano kuwa kwa mwaka 2019/2020, jumla ya Sh milioni 550 zilitolewa kwa asasi hizo 20 huku nane kati yake zikiwa zinaongozwa na wanaoshi na VVU.

Alisema mapambano dhidi ya VVU bado yanahitaji hasa ikizingatiwa misaada kutoka nje imepungua hivyo juhudi za Watanzania na wadau wengine zinahitajika ili kufikia malengo yaliyoweka na Serikali kufikia sifuri tatu mwaka 2030.

Rais mstaafu Dk. Jakaya Kikwete (katikati) na Mkurugenzi Mkuu wa TACAIDS, Dk. Leonard Maboko (kushoto kwake) wakimkabidhi hundi ya Sh milioni 100 Mwenyekiti wa Mfuko wa Udhamini wa kudhibiti UKIMWI -ATF, Carorine Mdundo(wa tatu kushoto) zilizotolewa na Kampuni ya GGML kupitia Kampeni ya GGML Kili Challenge. Wengine wanaoshuhudia kushoto ni Makamu Rais wa AngloGold Ashanti- GGML anayeshughulikia miradi endelevu Ghana na Tanzania, Simon Shayo na Mkurugenzi Mtendaji wa GGML, Terry Strong.

Katika harambee hiyo GGML walitoa dola za Marekani 500,0000.Zoezi hilo la kupanda mlima linatarajiwa kuanza tarehe 14 Julai na kushuka tarehe 20 Julai mwaka huu.

Wengine wanaoshuhudia kushoto ni Makamu Rais wa AngloGold Ashanti- GGML anayeshughulikia miradi endelevu Ghana na Tanzania, Simon Shayo na Mkurugenzi Mtendaji wa GGML, Terry Strong.

By Jamhuri